WAMBURA NA WENZAKE WATABAKI LINI NA KOFIA MOJA?

WAMBURA NA WENZAKE WATABAKI LINI NA KOFIA MOJA?

778
0
KUSHIRIKI

NA AYOUB HINJO

UONGOZI ni kipawa cha kipekee sana, tofauti na mambo mengine ambayo mtu anaweza kuyachukulia kwa urahisi zaidi. Hata katika vitabu vya dini, imekuwa ikielezwa jinsi Mungu alivyomteua Samuel kuwa mfalme wa Israel.

Ni jambo kubwa ambalo hapa nchini limeonekana kama jambo la mchezo na mara huchukuliwa kawaida sana na kusahau kuwa, wamebeba hatima za watu ambao waliwachagua na kuwaamini wanaweza kuwasaidia kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa maendeleo mazuri.

Hata katika mchezo huu wa mpira wa miguu kumekuwa na mambo mengi yanayofanyika nje ya uwanja. Dhamana ya mpira wa Tanzania ipo mikononi mwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kwa miaka mingi imekuwa kama ‘fashion’ kuona kiongozi kuwa na vyeo zaidi ya viwili ambavyo vyote vinahusika na jambo moja, nikimaanisha soka.

Mifano ipo mingi sana, Rais wa TFF wa awamu iliyopita, Jamal Malinzi, alikuwa pia Mwenyekiti wa Soka wa Mkoa wa Kagera. Yaani kwa akili ya kawaida tu ni jambo la ajabu, japo katiba ilimruhusu kufanya hivyo.

Malinzi kilimshinda nini kubaki kuwa rais tu na kwenda kugombea tena uenyekiti wa chama cha mkoa? Majukumu aliyokuwa nayo hayamruhusu kufanya hivyo.

Kwani kwa wakati ule hakukuwa na watu walioweza kukaa kwenye kiti hicho? Nadhani ni tamaa ya madaraka ya uongozi tu ilitawala kwenye kichwa cha Malinzi.

Malinzi ulikuwa mfano hai ambao karibu kila mdau wa soka hapa nchini alijua na kulaani kitendo hicho cha kujilimbikizia madaraka katika uongozi.

Hata sasa wapo baadhi ya viongozi ambao wanafanya kazi wakiwa na vyeo viwili au zaidi, lakini kumekuwa hakuna mabadiliko yoyote ya maendeleo ambayo wamefanya.

Michael Wambura ni Makamu wa Rais wa TFF, lakini pia ni Mwenyekiti wa Soka wa Mkoa wa Mara. Anafanyaje maamuzi yake katika hili? Kwani Mkoa wa Mara umekosa watu ambao wataweza kusimama na kuongoza mpira kwenye mkoa huo? Siamini katika hilo.

Clement Sanga ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga, lakini pia ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, bado haitusaidii kwa upande mwingine. Anawezaje kutatua matatizo ya klabu na timu nyingine? Hakuna kitu kama hicho, kama tunahitaji maendeleo ya soka ya nchi hii.

Salum Chacha naye anaingia kwenye kundi hili. Ni Katibu wa Chama cha Soka Kagera, pia anakaa kwenye kiti cha uongozi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi. Licha ya umahiri wake wa kazi, lakini bado ni ngumu kufanya hivi vyote kwa wakati mmoja.

Mifano ya maendeleo iko hai katika nchi zilizoendelea kuliko sisi, hakuna ubabaishaji kama huu katika maendeleo ya soka. Kwa wenzetu hakuna mambo kama haya.

Mwenyekiti wa Soka wa Mkoa Dar es Salaam, Almas Kasongo, pia ni Mjumbe wa Bodi ya Ligi. Bado haitusaidii kwa chochote katika nchi hii. Sijui Kasongo anatudanganya wapi kuhusu maendeleo ya soka katika mkoa huu wa Dar es Salaam, hakuna maendeleo chanya zaidi ya kuzidi kupiga hatua kurudi nyuma.

Tunashindwa kuiga mambo mazuri ambayo yataleta mwanga na tumaini jipya la maendeleo ya mpira huu. Uliona wapi Sepp Blatter, aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kisha akawa na urais wa soka wa nchi fulani? Hii huwa inatokea bongo tu, ambako hatujali sana hatima za watu waliowapa mamlaka ya kuwa sehemu hizo.

Kwa vyovyote hakuna maendeleo yatakayofanyika katika mfumo huo wa uongozi. Tutaaminishana kwa muda tu, lakini tutasimama hapa hapa na kuishia kulalamika tu.

Binafsi naona ni kama hakuna malengo ya dhati kimaendeleo zaidi ya kuangalia upatikanaji wa sehemu au nafasi za uongozi na inawezekana isiwe kwa maendeleo ya mpira nchini.

Ahadi tele, hakuna utekelezaji. Mipango mingi iliyojaa hadithi, migogoro isiyokwisha na klabu utafikiri nayo inamiliki klabu. Sasa kiongozi wake mkuu, kuwa pia kiongozi wa mkoa au sehemu nyingine katika eneo hilo ni jambo la kuchekesha

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU