SHERIA YA MTOTO YAKWAMA KUMLINDA LULU

SHERIA YA MTOTO YAKWAMA KUMLINDA LULU

767
0
KUSHIRIKI

*Aonekana mkomavu, atupwa jela miaka miwili

NA KULWA MZEE NA PATRICIA KIMELEMETA

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka miwili jela Msanii, Elizabeth Michael maarufu Lulu, baada ya kujiridhisha kwamba alimuua Steven Kanumba bila kukusudia.

Hukumu hiyo ilisomwa jana na Jaji Sam Rumanyika, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wanne wa upande wa Jamhuri na utetezi wa mshtakiwa, huku akisema: “ushahidi wa mazingira unaweza kumtia hatiani pale ambapo ushahidi wote unamnyooshea kidole mshtakiwa peke yake mwanzo mwisho”.

Akianza kusoma hukumu hiyo, Jaji Rumanyika alisema mshtakiwa alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili mwaka 2012, akishtakiwa kwa kumuua Steven Kanumba Aprili 7, mwaka huo, tukio lililotokea Sinza Vatican.

Alisema Jamhuri ilikuwa na mashahidi wanne na mshtakiwa kwa upande wake, alijitetea mwenyewe pamoja na kielelezo cha Josephine Mushumbuzi.

“Jamhuri kwa upande wake imejikita katika ushahidi wa mazingira, hapakuwepo hata chembe ya ushahidi wa moja kwa moja, mshtakiwa alikubali kwamba yeye ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu ambaye alikuwa mpenzi wake kwa miezi minne.

“Katika mazingira hayo ya mshtakiwa kuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu, sheria inamtaka kutoa maelezo ya kina kuhusu kifo cha marehemu na akishindwa yeye ndiye anakuwa muuaji.

“Ushahidi wa mazingira unaweza kumtia hatiani pale ambapo ushahidi wote unamnyooshea kidole mshtakiwa peke yake mwanzo mwisho … ushahidi wa shahidi wa kwanza ni kwamba kulikuwa na mzozo, ushahidi huo mshtakiwa alikubali kwamba kweli kulikuwa na mzozo akapigwa na marehemu.

“Mwingine anaweza kusema kapigwa au kulikuwa na ugomvi, tafsiri ya ugomvi ni ile kurushiana maneno ya kejeli, dharau, kizembe, kwa aliyeanzisha alikuwa na nia ya kumuudhi mwenzake… hilo si la msingi sana, kwa maoni yangu kutokana na tafsiri hiyo basi kuanguka ni miongoni mwa matukio yanayotazamiwa kutokea katika ugomvi,” alisema Jaji Rumanyika.

Jaji Rumanyika alieleza kuwa mshtakiwa katika utetezi wake alisema marehemu alikuwa kalewa na kwa msingi huo mlevi kati ya mambo anayofanya ni kuanguka ovyo.

“Kuhusu hili mshtakiwa alijikanganya, anasema marehemu alimfukuza akammudu kumkamata, akafanikiwa kumrudisha chumbani kwa kumburuza, lakini hakusema wakati akimfukuza na kumburuza kama alikuwa akianguka.

“Maelezo ya Josephine Mushumbuzi si taarifa ya hospitali, hayakuwa na hadhi ya cheti cha hospitali na mahakama haikuwahi kuambiwa Mushumbuzi naye alikuwa miongoni mwa madaktari wa uchunguzi.

“Daktari wa familia na mshtakiwa walitakiwa kueleza historia ya maradhi ya marehemu, kwa sababu alikuwa mpenzi wake kwa miezi minne lakini hawakufanya hivyo.

“Mazingira yanakinzana na hekima ya kawaida….hata pale marehemu alipoendelea kumpiga mshtakiwa, akaenda kiwango cha kutaka kumuua kwa panga mshtakiwa hakurudishia wala kutaka kumsukuma…ni kama mshtakiwa alichukua taratibu za kwenye biblia… akipiga shavu la kushoto mgeuzie na shavu la kulia…. Lakini hayo hakusema katika utetezi wake,” alisema.

Alisema mshtakiwa alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu, hivyo alitakiwa kuelezea nini kilitokea.

“Tunabakia na watu wawili wa kusema kwa kina kuhusiana na tukio hili ambao ni mshtakiwa na marehemu…Marehemu hata akifufuka kwa muujiza, mahakama haitasikiliza muujiza.

“Pengine anaweza akatokea mtu mwingine akasema Aprili 7, 2012 , wakati tukio likitokea mshtakiwa alikuwa na umri wa miaka 17, hakuwa mtu mzima..kwa umri huo anaweza kusema asingeweza kujua mabaya.

“Hili lina mazingira yake makuu matatu, moja…alikuwa mtoto aliyefikia hatua fulani akiitwa mke na alikubali. Pili, mtoto wa aina yake mshtakiwa alithubutu na kuamua ndivyo sivyo kwa matakwa yake.

“Anajiamulia wapi aende na tatu, mtoto wa aina yake mshtakiwa anaamua kwenda matembezini usiku wa manane, akamtembelea mpenzi wake na kisha akaendelea na matembezi yake.

“Mshtakiwa huyu si wale watoto waliolengwa kulindwa katika sheria ya mtoto… Kama mtoto anaweza kufanya ya watu wazima na akajiamini kuyafanya ni mkomavu.

“Sitaki kuwa wa kwanza kuonyesha kushindwa … Kifo cha marehemu Kanumba kimetokana na mshtakiwa, kifo kinachotokana na ugomvi hupelekea aina hii ya mashauri,” alisema Jaji Rumanyika.

Jaji Rumanyika aliendelea kusema, sheria ya kuua bila kukusudia ina lengo la kudhibiti vitendo hivyo na kwamba katika mashauri mengi muuaji si lazima ithibitike.

“Kwa kuwa mshtakiwa kasema marehemu alikuwa na wivu usio na msingi, wivu huo ndio ulisababisha kupigwa ….hakuna mchezo usio na kanuni…mapenzi ni mchezo basi wivu ndio kanuni zake.

“Kama aliamua kuingia katika mchezo basi afuate kanuni, wivu wa maendeleo huzaa maendeleo, lakini wivu wa mapenzi huzaa maangamizi. Mshtakiwa alijua marehemu ana wivu, basi alipoanza kushukiwa kuhusu simu alitakiwa kwa kanuni ya mapenzi aache simu lakini yeye aliamua kama noma na iwe noma.

“Kutokana na ushahidi huo, mahakama inamtia hatiani mshtakiwa chini ya kifungu namba 195 ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu,” alisema Jaji Rumanyika na kuwataka mawakili wa pande zote kusema lolote dhidi ya mshtakiwa.

Akimtetea mshtakiwa apunguziwe adhabu, Wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala, aliomba mahakama impe kifungo cha nje, pia apewe adhabu ndogo kwa sababu anategemewa na mama yake pamoja na mdogo wake.

Alisema mshtakiwa alipata fundisho, hivi sasa kabadilika, anasoma na amekuwa balozi katika taasisi mbalimbali.

Kibatala aliomba apunguziwe adhabu pia kwa sababu baada ya tukio hilo kutokea, alikaa gerezani miezi 10 mpaka alipopewa dhamana Oktoba mwaka 2013.

Kibatala alimaliza kuomba nafuu ya mahakama, upande wa Jamhuri wao waliomba apewe adhabu ili iwe fundisho kwa watu wengine.

Kipindi chote baada ya kutiwa hatiani, Lulu alikuwa hatulii kizimbani…mara anapandisha dera lake na kulishusha…mara anafunga mikono maeneo ya tumboni, kifuani na wakati mwingine alikuwa akipeleka mikono yake yote miwili katika mashavu yake.

Baada ya maelezo hayo ya mawakili, Jaji Rumanyika alihitimisha hukumu yake kwa kusema: “Vitu vya kuangalia ni vingi, wahalifu ni mazao ya jamii…lazima mahakama izingatie matakwa ya sheria….mshtakiwa anahukumiwa kutumikia kifungo cha miaka miwili jela.”

Mama Lulu hakuamini kilichotokea

BAADA ya kutolewa hukumu hiyo, baadhi ya wananchi waliokuwa mahakamani hapo walipigwa na butwaa.

Baadhi ya ndugu zake Lulu walionekana wakimshikilia mama yake mzazi, Lucrencia Karugila  ambaye alikuwa hawezi kutembea baada ya kusikia mtoto wake amehukumiwa kwenda jela miaka miwili.

Ndugu hao walimchukua mama yake na kumwingiza kwenye gari ndogo na kuanza kumfariji kutokana na uamuzi wa mahakama hiyo.

Mama Kanumba aenda makaburini kwa mwanaye

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutolewa hukumu hiyo, mama mzazi wa msanii Kanumba, Flora Mtengoa, aliishukuru mahakama na kudai kuwa imetenda haki.

Alisema licha ya kesi hiyo kukaa muda mrefu mahakamani, lakini hukumu iliyotolewa imetenda haki kulingana na ukubwa wa shtaka lenyewe.

“Ninaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na jaji aliyetoa hukumu hii, kwa sababu ametenda haki kulingana na ukubwa wa shtaka lenyewe, kilichobaki niende kwenye kaburi la mwanangu na kulia,” alisema mama Kanumba.

Mastaa wamkacha Lulu

Wakiwa mahakamani hapo, hakuna msanii yeyote maarufu aliyeonekana kumsindikiza kwa ajili ya kusikiliza hukumu hiyo, hali ambayo iliwashangaza wengi.

Hii inaonyesha kuwa Lulu hakuwa na mahusiano mazuri na wenzake au walishajua nini kinatokea kutokana na mlolongo wa kesi ilivyokuwa ikienda.

Atolewa kwa kificho kupelekwa jela

Ilipofika saa nane mchana, gari la wazi ambalo lilikuwa na polisi zaidi ya sita waliovalia kiraia, huku wakiwa na silaha lilifika mahakamani hapo na kwenda moja kwa moja kwenye mlango wa nyuma.

Baada ya kufika, baadhi ya askari hao waliingia ndani ya jengo la mahakama na kwenda kumchukua msanii huyo, huku wakiwa wamemficha ili waandishi wasiweze kumuona wala kumpiga picha.

Hata hivyo, baadhi ya wapiga picha walishtuka na kuanza kulikimbia gari hilo ambalo walifanikiwa kulipiga picha, licha ya kukatazwa na polisi.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU