AZAM FC KUMNG’OA TSHISHIMBI YANGA

AZAM FC KUMNG’OA TSHISHIMBI YANGA

4134
0
KUSHIRIKI
  • Yabainika Jangwani hawana jeuri ya kumzuia
  • Dili linaweza kumalizika ndani ya siku saba zijazo

HUSSEIN OMAR NA SAADA SALIM

AMA hakika pesa (fedha) ni sabuni ya roho kwani pamoja na kufahamu jinsi anavyopendwa na watu wa Yanga, kiungo Pappy Kabamba Tshishimbi yupo njiani kutua Azam ili kufuata ‘malisho’ bora zaidi.

Tayari klabu ya Azam imethibitisha kumtaka kiungo huyo kipenzi cha wana-Yanga na kwamba kwa kuwa dirisha dogo la usajili linafunguliwa kesho, lolote linaweza kutokea ndani ya wiki moja au mbili hivi.

Ikumbukwe kuwa Tshishimbi alitua Yanga mwanzoni mwa msimu huu ambapo alianza kujipatia umaarufu kutokana na kandanda safi alioionyesha wakati wa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, Agosti 23, mwaka huu.

Katika mchezo huo, Tshishimbi alicheza vizuri mno na kuwafunika mastaa kibao wa timu hizo kongwe hapa nchini, akiwamo ‘mtaalamu’ Emmanuel Okwi kiasi cha kuwateka watu wa Yanga ambao pamoja na kupoteza mchezo huo kwa mikwaju ya penalti, walitoka Uwanja wa Taifa wakiwa meno nje kutokana na kuvutiwa na kandanda ya mchezaji wao huyo.

Lakini ikiwa ni siku chache baada ya kung’ara tena katika mechi dhidi ya Simba ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, tayari kuna uwezekano kiungo huyo aliyetua nchini akitokea Mbabane Swallow ya Swaziland, akatimkia Azam.

Taarifa zilizoifikia BINGWA wikiendi iliyopita, zinasema kwamba kutokana na kuyumba kwa hali ya uchumi ya Yanga, Azam wanatumia nafasi hiyo kunasa huduma ya kiungo huyo ambaye ameonyesha dhahiri yupo tayari kutua katika kikosi cha ‘Wanalambalamba’ hao.

“Yanga wapo katika hali mbaya, kuna uwezekano mkubwa kumkosa Tshishimbi na kujiunga na Azam ambao wameonyesha kuhitaji huduma yake,” alisema mtoa habari wetu wa uhakika.

Mtoa habari huyo alisema kwa kuwa Azam wanaendelea kuimarisha kikosi chao, wapo tayari kutumia udhaifu huo wa Yanga kumng’oa kiungo huyo ndani ya siku saba zijazo.

BINGWA lilimtafuta Mwenyekiti wa Azam, Nassor Idrissa ‘Father’, kuzungumzia juu ya habari hiyo ambapo alikiri kuwa Tshishimbi ni mchezaji mzuri hivyo hakuna timu ambayo itamkataa.

Alisema katika safu ya viungo kwa Yanga, mchezaji huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ameimarisha na kujituma kwake kumeifanya timu hiyo kuonekana vizuri zaidi katika eneo analocheza.

“Ni mzuri, sitaweza kusema lolote zaidi ya hilo…,” alisema.

Pamoja na Idrissa kushindwa kuweka wazi kama wanaweza kumsajili Tshishimbi, lakini BINGWA lina taarifa kuwa uwezekano huo upo.

Lakini pia, gazeti hili linafahamu kuwa kabla ya kutua Yanga, Tshishimbi alitamani kuichezea Azam baada ya kuiona wakati timu yake ya Mbabane Swallows ilipomenyana na ‘Wanalambalamba’ hao katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka jana.

Kiungo huyo alivutiwa na Azam kutokana na uwekezaji wake katika soka, akiamini timu hiyo inaweza kumsaidia katika kutimiza ndoto yake ya kucheza soka la kulipwa katika timu kubwa Afrika na hatimaye Ulaya.

Katika jarida moja la soka lililotoka hivi karibuni hapa nchini, Tshishimbi alikaririwa akisema: “Nilishafanya mazungumzo na Orapa (klabu ya soka ya nchini Botswana) na tayari walishanitumia fedha ya tiketi ya kwenda Botswana, lakini kocha wangu alinifuata na kuniambia Yanga wananitaka. Sikuwa naifahamu. Nilimuuliza inatoka wapi, akanijibu Tanzania.

“Aliniambia pia kocha wao (George Lwandamina), alikuwa anakuja Swaziland mara kwa mara kunifuatilia. Binafsi nilisema kama ningerudi Tanzania, basi ningecheza Azam, lakini nilipopewa vizuri historia ya Yanga, sikufikiria mara mbili. Nilishacheza Mbabane kwa misimu miwili, hivyo nilihitaji changamoto mpya.”

Ni kutokana na kauli hiyo ya Tshishimbi na hali ilivyo ndani ya Yanga, hata mtoto mdogo hawezi kukataa juu ya mpango wa kiungo huyo kutua Azam.

Japo bado ana mkataba na Yanga, lakini kitendo cha kutolipwa mishahara ya miezi mitatu, kinamfanya kuwa huru kuamua lolote juu ya majaliwa yake kisoka kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), ukizingatia alitua hapa nchini kusaka fedha na si kutalii.

Mfano mzuri ni kwa sakata la Okwi ambaye aliondoka Yanga akiwa na mkataba na kurejea Simba baada ya kutolipwa mishahara ya miezi mitatu.

Hata Yanga walipomshtaki Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), klabu hiyo iligonga mwamba kwa kutumia kanuni hiyo na mwisho wa siku, Mganda huyo kuendelea na ‘hamsini zake’.

Bingwa ilipomtafuta Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa jana kuzungumzia suala hilo, simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokewa.

Lakini ni siku tatu zilizopita, kiongozi huyo alikiri klabu yao kukabiliwa na ukata na kuwaahidi wachezaji kumalizana nao kabla ya kwenda likizo.

Mkwasa alitoa ahadi hiyo alipotembelea mazoezi ya timu yake kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ili kuwaweka sawa wachezaji baada ya tetesi za vijana wao hao kupanga kugoma.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU