BARAKA THE PRINCE: NAJ ALINIPA WAZO LA KUANZISHA BANA MUSIC LAB

BARAKA THE PRINCE: NAJ ALINIPA WAZO LA KUANZISHA BANA MUSIC LAB

540
0
KUSHIRIKI

NA CHRISTOPHER MSEKENA

BARAKA The Prince yumo kwenye orodha ya mastaa wa Bongo Fleva, wanaoutendea haki muziki huo kwa kufanya kazi nzuri zinazokonga nyoyo za mashabiki wa ndani na nje ya nchi.

Leo kupitia safu hii ya Jiachie na Staa Wako, Baraka The Prince, anakwenda kujibu maswali yenu yote ambayo wasomaji mbalimbali walimuuliza kupitia namba hiyo hapo juu, karibu.

SWALI: Hamis Chiumbi kutoka Kariakoo, Dar anauliza sababu zilizofanya Baraka ajitoe kwenye lebo ya Rockstar 4000.

Baraka The Prince: Ishu ya Rockstar ilikuwa ni jinsi ya utoaji wangu wa kazi, tangu niingie pale nimetoa Nisamehe na Acha Niende ambazo ni nyimbo mbili tu ndani ya miaka miwili.

Na kama unavyojua unapoacha kutoa nyimbo wakati wasanii wenzako wanatoa nyimbo nyingi kila siku unapoteza mashabiki na hata hadhi yako pia inashuka, mimi niliingia Rockstar kufanya kazi, kujenga kipaji changu na kuongeza mashabiki kwa sababu ni menejimenti makini na wanafanya kazi kitaalamu, nikadhani watanisogeza mbele lakini vile nilivyotarajia ilikuwa tofauti ndiyo maana nikatoka.

SWALI: Razak wa Kimara anauliza ilikuwaje ukafanya kazi yako mpya, Sometimes na prodyuza Mr T Touch?

Baraka The Prince: Mr T Touch ni prodyuza wangu wa kwanza kufahamiana naye hapa Dar, nimefahamiana naye zaidi ya miaka 6 ila hatujawahi kufanya wimbo zaidi ya mimi kushiriki kwenye viitikio tu vya nyimbo za wasanii wengine, kwa hiyo Sometimes ni wimbo wangu wa kwanza kurekodi naye na tulifanya toka mwaka jana.

SWALI: Selemani Mwakabana anauliza sababu gani zimefanya siku hizi wewe na Naj hamjionyeshi sana katika mitandao ya jamii kama zamani?

Baraka The Prince: Tumeamua kuwa na maisha yetu binafsi, si kila kitu tunaweza kukianika Instagram, tunaitumia mitandao ya jamii sana kwa ajili ya kutukutanisha na mashabiki zetu, kwa hiyo huwezi kuona tena tunapostiana labla iwe ni ishu ya kazi.

SWALI: Kevi wa Arusha anauliza ulipata wapi wazo la kuanzisha lebo yako ya Bana Music Lab

Baraka The Prince: Kwanza mpenzi wangu Naj ndiye alileta hilo wazo la lebo na mwanzo Bana ilisimama kama Baraka & Najma, lakini tulipotaka kuifanya kibiashara tukaibadilisha ikawa Baraka Nation Lab ili iwe kampuni na isikae kimapenzi sana.

SWALI: Dianamo Paclizer, anauliza uliwahi kuandikiwa nyimbo na vipi hii mpya, Sometimes umeandikiwa?

Baraka The Prince:  Nimewahi kuandikiwa nyimbo zangu kadhaa ila huu mpya kila kitu nimefanya mwenyewe, kuandikiwa nyimbo si jambo la ajabu linafanyika duniani kote, unajua muziki wetu ulipofikia ni lazima tugawane majukumu, anayeimba aimbe, anayetunga atunge na anayeprodyuzi atengeneze muziki.

SWALI: Natasha Kambo wa Iringa, anauliza uhusiano na meneja wako wa zamani (Kid Boy) aliyekutoa kimuziki upo vipi na kwanini uliacha kufanya naye kazi?

Baraka The Prince: Mimi na Kid tupo poa, namheshimu sana sababu yeye ndiye msingi wangu aliyenifanya niwe hapa, nilitoka kwa sababu yalikuwa ni maamuzi ya Kid mwenyewe, aliniambia tusimame kufanya kazi.

Nakumbuka ilikuwa wakati wa kampeni, mpenzi wangu wa zamani aliniomba nimsindikize Dodoma na mimi nikajua wikiendi hatuna kazi, nikaamua kumsindikiza Dom, nafika Dodoma usiku Kid alinipigia simu akaniambia kuna shoo imepatikana Iringa.

Na mimi nikaona siwezi kurudi tena Morogoro ili niunge Iringa kwenye shoo sababu ilikuwa usiku sana, nikamwambia naweza kwenda ila nitachelewa sana.

Akachukia akaniandikia meseji hataki kufanya kazi na mimi, nikaona kama ni adhabu nikasubiri hasira zake zipungue, nikamwomba sana msamaha lakini meseji zangu akawa hajibu, hiyo ndiyo ilikuwa chanzo cha mimi kuacha kufanya kazi na Tetemesha.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU