KITAELEWEKA TU NI AUBAMEYANG, MANE AU SALAH MCHEZAJI BORA AFRIKA 2017?

KITAELEWEKA TU NI AUBAMEYANG, MANE AU SALAH MCHEZAJI BORA AFRIKA 2017?

760
0
KUSHIRIKI

CAIRO, Misri

ZIMEBAKI wiki kadhaa kabla ya macho na masikio ya mashabiki wa soka kuelekezwa kwenye hafla ya utoaji tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa ya wadhamini wa tuzo hiyo ambao ni Shirika la Habari la Uingereza (BBC), mshindi anatarajiwa kutangazwa Desemba 11.

Mwaka jana, ilitua kwa winga wa Leicester City na timu ya Taifa ya Algeria, Riyard Mahrez, lakini katika orodha ya mwaka huu ameshindwa kuingia ‘top five’ ambayo ilitangazwa Novemba 11.

Ni majina ya Pierre-Emerick Aubameyang, Sadio Mane, Naby Keita, Victor Moses na Mohamed Salah pekee yaliyobaki.

Je, kati ya mastaa hao wa klabu za Borussia Dortmund, Liverpool, RB Leipzig na Chelsea, nani atakayeibuka kidedea?

Aubameyang (Gabon, Dortmund)

Alipochukua kiatu cha mfungaji bora kwa msimu wa 2016-17 wa Bundesliga na kutwaa kiatu cha mfungaji bora, Aubameyang aliweka rekodi ya kuwa Mwafrika wa kwanza kufikisha idadi hiyo ya mabao.

Lakini pia, alikuwa mchezaji wa nne kufunga zaidi ya mabao 30 katika historia ya ligi hiyo, hivyo akaingia moja kwa moja kwenye kikosi bora cha Bundesliga, ikiwa ni mara yake ya pili.

Aubameyang aliingia hata kwenye kinyang’anyiro cha Mchezaji Bora wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa). Pia, alitajwa kwenye tuzo ya Ballon d’Or.

Naby Keita (Guinea, Leipzig)

Keita aliuanza msimu uliopita akiwa hajulikani lakini aliumaliza akiwa staa, akitajwa hata kwenye kikosi bora cha Bundesliga. Klabu yake ya RB Leipzig ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya pili, akiwa amefunga mabao nane na kutoa asisti saba.

Pia, alikuwa amekokota mpira mara nyingi kuliko staa wa Bayern Munich, Arjen Robben.

Mafanikio hayo yaliwavuta Liverpool ambao wamekubali kutoa pauni milioni 48 na atatua Anfield hapo mwakani.

Sadio Mane (Senegal, Liver)

Aliingia kwenye kinyang’anyiro cha kuiwania Ballon d’Or na alikuwa mmoja kati ya waliounda kikosi bora cha Chama cha Wachezaji wa Kulipwa England (PFA).

Ameiwezesha Senegal kutinga fainali za Kombe la Dunia za mwakani nchini Urusi, ikiwa ni mara yao ya kwanza tangu mwaka 2002. Tangu kuanza kwa mwaka huu, ameifungia Senegal mabao manne katika mechi tisa. Katika fainali za Afcon za mwaka jana, aliipeleka timu hiyo robo fainali.

Msimu uliopita, aliipa Liver mabao 13, akiwa ndiye mfungaji bora wa kikosi hicho, licha ya kwamba alikosa takribani miezi miwili kutokana na majeraha ya goti.

Ikiwa ataibeba tuzo ya mwaka huu, basi itakuwa ni mara yake ya tatu.

Victor Moses (Nigeria, Chelsea)

Alikuwa kwenye kiwango kizuri msimu uliopita kwani alikuwa sehemu muhimu ya safari ya ubingwa wa Chelsea. Mbali na kuipa ubingwa wa Ligi Kuu, Moses aliiwezesha Chelsea kushika nafasi ya pili katika Kombe la FA.

Tangu kuanza kwa mwaka huu, Moses amecheza mechi tatu pekee za kimataifa, lakini alifunga katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Cameroon, ambao uliipa Nigeria nafasi ya kwenda Kombe la Dunia.

Ikiwa ataichukua, basi Moses atakuwa Mnigeria wa kwanza tangu Jay-Jay Okocha alipoibeba mwaka 2004.

Mohamed Salah (Misri, Liver)

Wamisri wanamkumbuka kwa bao lake dhidi ya Congo ambalo ndilo lililowapa tiketi ya kwenda Urusi mwakani.

Misri hawajashiriki Kombe la Dunia tangu mwaka 1990 lakini Salah aliwapa nafasi hiyo kwa mara nyingine.

Katika mechi za kufuzu, Salah aliwapa Mafarao hao mabao matano katika mechi saba.

Baada ya kumalizika kwa fainali za Afcon za mwaka huu, aliingia kwenye kikosi bora cha michuano hiyo, akifunga mabao manne kati ya matano waliyokuwa nayo Misri.

Lakini pia, amekuwa mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha Liver tangu alipojiunga nayo Juni mwaka huu akitokea Roma. Miezi miwili baada ya kutua Anfield, yaani Agosti, alipewa tuzo ya mchezaji bora klabuni hapo, ambayo pia aliitetea Septemba.

Huku akiwa na mabao 11 kwenye ligi, tayari mchezaji huyo ameshafunga mabao matano katika mechi sita za michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Katika msimu wake wa mwisho Roma kabla ya kuelekea England, Mwarabu huyo alikuwa amefunga mabao 15 na kutoa asisti 11, ambapo aliiwezesha Roma kumaliza ligi ikiwa nafasi ya pili, ikiachwa kwa pointi nne pekee na mabingwa Juventus.

Hii ni mara ya kwanza kwa Salah kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuiwania tuzo ya Mchezaji Bora Afrika na kama atafanikiwa kuibeba, atakuwa Mmisri wa kwanza tangu ilipotua mikononi mwa Mohamed Aboutrika mwaka 2008.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU