KWA HILI LA MSONDO NGOMA, WCB MMENIANGUSHA

KWA HILI LA MSONDO NGOMA, WCB MMENIANGUSHA

1439
0
KUSHIRIKI

NA CHRISTOPHER MSEKENA

SUALA la Hakimiliki ni jambo kubwa linalozingatiwa duniani kote. Umakini ni muhimu sana hasa pale unapotaka kunakili kitu ambacho tayari kimewahi kufanywa kabla yako.

Ndani ya sanaa kunakili kazi ya msanii wa zamani ni jambo la kawaida, limeshafanywa na wasanii wengi tu lakini hufanywa kwa utaratibu ambao pande zote zitaridhiana.

Ni kosa kisheria kutumia au kunakili kazi ya mtu bila ridhaa yake, ndiyo maana mtu anayeiba kinyemela akibainika hupigwa faini kubwa ili iwe fundisho kwa wengine wanaopenda kunakili na kubandika kazi za watu.

Lakini nimeshangaa niliposikia malalamiko ya baba wa muziki nchini, bendi kongwe ya Dansi, Msondo Ngoma, kuhusu lebo namba moja Bongo, WCB ikiitaka kulipwa fidia baada ya wasanii hao kunakili moja ya kazi yao ya sanaa bila ruhusa.

Bendi hiyo kongwe kupitia wanasheria wao (Maxim Advocates), wiki iliyopita iliiandikia barua lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) inayomilikiwa na Diamond Platnumz, ikitaka ilipwe shilingi milioni 300 huku ikionyesha dhamira ya kuishtaki isipofanya hivyo ndani ya siku saba kwa kosa la kunakili kionjo cha ala ya upepo (Saxophone), kilichowahi kutumiwa na bendi hiyo katika wimbo wao unaoitwa Ajali.

Agosti 25, mwaka huu, Diamond Platnumz akishirikiana na wasanii wake wa lebo ya WCB ambao ni Rayvanny, Rich Mavoko, Queen Darleen, Maromboso na Lavalava, walitoa wimbo unaoitwa Zilipendwa ambao ndani yake katika dakika 4:55 hadi dakika 5 sekunde ya 10, kilichezwa kionjo cha Saxophone ambacho kinafanana na kionjo kilichotengenezwa na kuchezwa na Msondo Ngoma katika dakika ya 6:38 mpaka dakika ya 6:52 ya wimbo wao wa Ajali.

Wakili wa Msondo Ngoma, Mwesigwa Muhingo kupitia barua hiyo, aliitaka lebo ya WCB kuilipa bendi ya Msondo Ngoma kiasi hicho cha fedha kwa haraka iwezekanavyo huku nakala ya barua ikipelekwa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Chama cha Hakimiliki (COSOTA).

Meneja wa bendi ya Msondo Ngoma, Said Kibiriti, alinambia hili suala si la kuliongelea kwenye vyombo vya habari, kwani limekaa kisheria zaidi huku upande wa WCB wakiwa kimya mpaka sasa.

Malalamiko hayo ya Msondo Ngoma yamefanya nijiulize maswali kadhaa kama ina maana uongozi wa WCB chini ya mameneja Sallam Sk, Babu Tale, Fella, Diamond Platnumz hawajui suala ya Hakimiliki?

Bila shaka wanafahamu, ila sijui nini kilitokea mpaka wakaachia wimbo wa Zilipendwa ukiwa na kionjo cha Saxophone ambacho kiliupa umaarufu wimbo wa Ajali wa Msondo Ngoma bila ridhaa ya wakongwe hao.

WCB wanajua hilo ni kosa, ndiyo maana nakumbuka mwaka jana walipotaka kuurudia wimbo wa Maria Salome ulioimbwa na Saida Karoli, walimtafuta meneja wa zamani wa Saida, wakaongea naye biashara na kukubaliana kisha wimbo ukatoka.

Lakini pia kipindi ambacho WCB wanatoa wimbo wao wa Zilipendwa, kesi ya Mwana Fa na AY dhidi ya kampuni moja ya mawasiliano ilikuwa inarindima Mahakama Kuu ya Tanzania, ishu ikiwa ni hiyo hiyo ya Hakimiliki.

Sasa iweje msanii mkubwa kama Diamond Platnumz ashindwe kuelewa kuwa kunakili kionjo kidogo tu kutoka kwenye kazi ya msanii mwingine ni kosa, inatia aibu. Hiyo inaleta picha kuwa huwenda WCB hawathamini kazi ya kutukuka iliyowahi kufanywa na wakongwe wa Msondo Ngoma.

Naamini sakata hili litamalizika kwa pande zote mbili kuridhiana, kwa kuwa ni wazi WCB wamefanya kosa huku Msondo Ngoma nao wakiitaka haki yao.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU