MASTAA WATOA NENO KIFUNGO CHA LULU

MASTAA WATOA NENO KIFUNGO CHA LULU

700
0
KUSHIRIKI

NA CHRISTOPHER MSEKENA

UMAARUFU unaweza kufananishwa na mvua za masika pale zinapoweza kuleta neema kwa kustawisha mazao shambani au kuleta mafuriko yatakayoleta maafa katika jamii.

Huo ni mfano ulio dhahiri kwenye maisha ya mwigizaji, Elizabeth Michael ‘Lulu’, mrembo aliyezaliwa Aprili 19 mwaka 1995, jijini Dar es Salaam na wazazi wake, Michael na Lucresia Kimemeta.

NDANI YA SANAA

Haina ubishi kuwa kipaji cha uigizaji kimezaliwa ndani ya Lulu. Mrembo huyo alianza kuonyesha uwezo wake akiwa na miaka mitano tu baada ya msanii Dk. Cheni kuvumbua kipaji chake kwa kumwingiza kwenye kundi la Kaole Sanaa Group.

Ndani ya kundi hilo, Lulu alijipatia umaarufu kupitia michezo mingi ya runinga aliyoigiza kama Zizimo, Baragumu, Gharika, Taswira na Demokrasia, kipindi hicho akiwa bado mwanafunzi wa Shule ya Msingi Remnant Academy na baadaye Sekondari ya Perfect Vision kisha St Mary ya jijini Dar es Salaam.

AKUA KISANAA

Baadaye aliingia kwa kishindo kwenye soko la filamu baada ya kushirikishwa filamu ya kwanza iliyoitwa Misukosuko.

Umaarufu alioupata uliendelea kumfungulia milango katika tasnia ya filamu, ambapo aliweza kuwa mwongozaji wa filamu na kuzalisha kazi zake mwenyewe.

Mwaka 2013 alizindua filamu yake ya kwanza inayoitwa Foolish Age, filamu iyo ilimpa mafanikio lukuki ikiwamo kuingia kwenye tuzo za ZIFF 2014.

Hakuishia hapo, mwaka 2015 Lulu aliachia filamu nyingine inayoitwa Mapenzi ya Mungu. Filamu hii ilimpa umaarufu kwenye anga la kimataifa na akaweza kushinda tuzo za Africa Magic Viewers Choice Awards 2016 zilizotolewa huko Lagos, Nigeria katika kipengele cha Filamu Bora Afrika Mashariki.

APATA MISUKOSUKO

Ustaa haukuwahi kumwacha Lulu salama licha ya kumpa mafanikio kwenye tasnia ya filamu, umaarufu umempitisha kwenye misukosuko kadhaa ambayo leo hii imemfanya awe mfungwa.

SKENDO YA SEKI

Mwaka 2015 mwigizaji huyo aliikwaa skendo ya kutoka kimapenzi na mfanyabiashara wa madini anayeitwa Lusekelo Mwandenga (Seki), licha ya yeye mwenyewe (Lulu) kutotaka kuzungumza kitu chochote kuhusu kifo cha jamaa huyo, japo kuwa mashabiki zake walimshambulia kwa maneno yaliyompa kero kiasi cha kujiondoa kabisa kwenye mtandao wa Instagram.

KUUA BILA KUKUSUDIA

Hakuna aliyewahi kufahamu kama Lulu na Steven Kanumba walikuwa wapenzi, labda ndugu na jamaa wachache wa     karibu. Lakini kilipotokea kifo cha gwiji hilo la filamu, mapenzi yao yakawa bayana.

Itakumbukwa kuwa Aprili 7, mwaka 2012, taarifa za huzuni zilisambaa kwamba msanii Steven Kanumba amefariki ghafla akiwa nyumbani kwake, Sinza, Vatican, Dar es Salaam.

Taarifa hizo ziliambatana na uvumi kwamba kuna msichana mdogo (Lulu) anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kuwa ndiye aliyekuwa na Kanumba chumbani wakati anapoteza maisha.

Kwa mara ya kwanza Lulu akapandishwa kizimbani Aprili 11, 2012 mbele ya  Hakimu Mfawidhi wa wakati huo wa Mahakama ya  Hakimu Mkazi Kisutu, Augustina Mbando, ambapo alisomewa mashitaka ya mauaji.

Lakini Januari 29, 2013 aliachiwa kwa dhamana baada ya kesi yake kubadilishwa hati ya mashitaka kutoka kwenye kesi ya mauaji kwenda mauaji ya bila kukusudia, ambapo badiliko hilo lilimpa nafasi ya kupata dhamana.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa tena Oktoba 19 na kuahirishwa Oktoba 26 mwaka huu baada ya Jaji Sam Rumanyika kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, yaani upande wa Jamhuri na upande wa utetezi sambamba na maoni ya Wazee wa Baraza, kisha kupangiwa tarehe ya hukumu ambayo ilikuwa ni jana na ilitolewa kwa Lulu baada ya kukutwa na hatia ya kumuua Steven Kanumba.

MASTAA WAMPA NENO LULU

Diamond Platnumz

“Mwenyezi Mungu ameamua kukupa mtihani huu wewe kwa sababu anaamini wewe ni shujaa na imara, pia anaamini wewe ndiyo msichana pekee unayeweza kuuhimili mtihani huu hivyo usisononeke, Make him proud.”

 Wema Sepetu

“Dah speechless, pole my baby, this too shall pass.”

 Dk Cheni

“Linapokukuta jambo wapo watakaokuonea huruma na wapo watakaokuwa na furaha, ila niwakumbushe jambo hakuna ajuaye kesho yake kubwa kila mapito mwambie Mungu asante.”

Gabo

Wacha niridhike na sauti ya kunyamaza huku mtima wangu ukiwa na majonzi na maswali tele, hivi Kanumba angekuwa hai asingeshtakiwa kwa kuishi kinyumba na mtoto chini ya miaka 18?,”

Irene Uwoya

“Daah! Mungu akupe ujasiri mama, tupo nyuma yako.”

Rose Ndauka

“Hakika kilichotokea Aprili 7, 2012 kili-affect sana na kinaendelea kuaffect tasnia ya filamu Tanzania na kilichotokea leo kimetuachia somo kubwa sana kama vijana. Pole sana Lulu  Mungu yupo nawe, tunakuombea.”

Kajala

“Sala iwe chakula chako cha kila siku. Usimuache Mungu wako. Tuko pamoja katika kuomba. Usinung’unike mshukuru kwa kile kilichitoke.”

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU