SHOMARI KAPOMBE: NAONDOKA SIMBA

SHOMARI KAPOMBE: NAONDOKA SIMBA

2886
0
KUSHIRIKI

CLARA ALPHONCE NA WINFRIDA MTOI

BAADA ya kukosekana dimbani kwa muda mrefu kutokana na majeraha, beki wa timu ya Simba, Shomari Kapombe ameweka wazi kuwa yupo tayari kuondoka kwenye kikosi hicho iwapo mkataba wake utavunjwa.

Kauli hiyo imekuja baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa klabu hiyo, Zacharia Hanspoppe, kumlalamikia beki huyo katika vyombo vya habari kuwa hataki kucheza kwa makusudi.

Kapombe alisema amesikitishwa sana na kitendo cha kiongozi huyo kutoa kauli hiyo kwenye vyombo vya habari wakati anafahamu kuhusu afya yake baada ya juzi kuzungumza naye na kumweleza kila kitu juu ya maendeleo yake.

“Mimi siwezi kuacha kucheza mpira kama ningekuwa nimepona, bado naumwa, hata dokta kaniambia naweza kurudi uwanjani rasmi mzunguko wa pili, kwasababu yeye ndiye anajua naumwa nini, kwa sasa kuna program maalumu ambayo naendelea nayo. Hanspoppe hajawahi kucheza mpira, anachojua yeye ni kulalamika tu.

“Wao kama wanataka kuvunja mkataba, wavunje tu, mimi siwezi kulazimishwa kucheza nikiwa naumwa, eti kwa kuogopa mkataba wangu utavunjwa! Wavunje,” alisema Kapombe.

Alichosema dokta wa Simba

Dokta wa Simba, Yassin Gembe, alilithibitishia BINGWA kuwa, Kapombe bado hayupo fiti kwa asilimia 100, kwani kuna matibabu mengine anaendelea nayo, ikiwamo program maalumu ya mazoezi na huenda akarejea uwanjani mzunguko wa pili.

Mashabiki wamshukia Hanspoppe

Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida, mashabiki wa Simba waliokuwa wanafuatilia mada hiyo jana walimtupia lawama Mwenyekiti huyo kwa kauli zake kupitia mitandao ya kijamii ambapo wengi walimpinga.

Kauli ya Hanspoppe juu ya Kapombe

Alisema kuwa walimsajili Kapombe ili acheze mpira, hivyo kama ameshindwa kucheza inabidi wakae waangalie ni jinsi jinsi ya kufanya kuhusu hilo na yeye ndiye anatakiwa kuchagua kucheza au kuondoka.

“Vipimo vinaonyesha kapona ila yeye anaogopa kucheza kwa kuhofia ataumia, hatuwezi kuendelea kumlipa mtu mshahara wakati hafanyi kazi inayotakiwa, majeruhi gani asiyepona muda mrefu, kwasababu vipimo havidanganyi.

“Hivyo msimamo wa kubaki Simba anao mwenyewe anatakiwa atuambie anataka kucheza au hataki, kama ni majeruhi bado atupishe ile ni kazi ambayo anatakiwa kutumia mwili wake kama huwezi utapewa mshahara wa kazi gani?” Alihoji Hanspoppe.

Kapombe alirejea tena Simba msimu huu akitokea timu ya Azam FC, kwa mkataba wa miaka miwili ambao hajaitumikia mechi hata moja ya Ligi Kuu Tanzania Bara tangu alipoumia katika mechi ya timu ya Taifa, Taifa Star dhidi ya Rwanda ya kuwania kufuzu fainali za CHAN kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU