STRAIKA RAYON AWAPA HABARI NJEMA SIMBA

STRAIKA RAYON AWAPA HABARI NJEMA SIMBA

2346
0
KUSHIRIKI

*Atangaza: Nakuja Tanzania, mashabiki Simba jiandaeni kushangilia mabao

SAADA SALIM NA SALMA MPELI

STRAIKA wa Rayon Sport, Mrundi Naimana Shassir, ameweka wazi yupo tayari kujiunga na klabu ya Simba endapo mazungumzo yatakwenda vizuri baina yake na viongozi wa klabu hiyo ya Wekundu wa Msimbazi kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo linalofunguliwa kesho.

Shassir ni miongoni mwa majina yaliyopendekezwa na benchi la ufundi huku akihusishwa kocha msaidizi wa Simba, Irambona Masoud Djuma ambaye amewahi kumfundisha mchezaji huyo.

Shassir amecheza mechi tatu katika michezo ya Ligi Kuu Rwanda na kufunga mabao mawili mwenye uwezo wa kucheza namba 10 na kutokea pembeni.

Akizungumza na BINGWA jana kwa simu, Shassir, alisema amefanya mawasiliano na mmoja wa viongozi wa Simba kwa kumuhoji juu ya mkataba wake wa Rayon Sport ambaye timu anayotumikia sasa.

Alisema mkataba wake umebaki wa miezi sita ambapo yupo tayari kutoka na kujiunga na Simba endapo viongozi wa klabu hiyo itampa kile anachokihitaji, ikiwamo suala la fedha.

“Natafuta fedha ndio maana nimetoka Burundi kuja Rwanda, endapo Simba wakija rasmi kuzungumza, sina shaka, nakuja Tanzania kucheza na kufikia malengo yanayotarajiwa mashabiki wa timu hiyo,” alisema Shassir.

Mshambuliaji huyo alisema kwa sasa suala la dau ni mapema kulitaja kwani bado hawajaanza mazungumzo zaidi ya kufanya mawasiliano ya awali.

“Matarajio yangu ni kujiunga na Simba nikiwa mchezaji huru, lakini kama mawasiliano yatakwenda vizuri na kuafikiana, nina imani nitachezea timu hiyo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Kocha msaidizi wa Simba, Djuma, amekiri kumfahamu mchezaji huyo, lakini hana taarifa za kuwa anakuja kujiunga na timu hiyo.

Alisema kuwa yeye mwenyewe anazisikia hizo habari akiulizwa na kwamba iwapo taarifa hizi ni za kweli, basi viongozi ndiyo wanaozifahamu.

“Umepata wapi hizo habari na nani kakwambia? Mimi sifahamu kama huyo mchezaji anakuja, ila namjua, anacheza Rayon. Kama ni kweli, basi viongozi wa Simba watakuwa ndiyo wanafahamu zaidi,” alisema Djuma.

Kocha huyo aliyeanza kuinoa Simba mwanzoni mwa mwezi Oktoba, aliwahi kuinoa Rayon Sport ambayo aliipa taji la Ligi Kuu nchini humo msimu uliopita kabla ya kuamua kuachana nao msimu huu na kujiunga na Wekundu wa Msimbazi.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU