BELL 9: NATUNGA SHERIA NITARUDI KWA KISHINDO

BELL 9: NATUNGA SHERIA NITARUDI KWA KISHINDO

270
0
KUSHIRIKI

NA ESTHER GEORGE

WAHENGA walisema ukimwona kobe kainama ujue anatunga sheria.

Ndivyo ilivyo kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Abelnego Damian maarufu kama Bell 9, ambaye licha ya kuwa na kipaji cha kutunga nyimbo nzuri zenye ujumbe wa mapenzi katika jamii, lakini kwa siku za karibuni amekuwa hasikiki japo alikuwa akitamba vilivyo.

Japo nyimbo zake nyingi zimekuwa zikipendwa na mashabiki wengi kutokana na uimbaji wake wa hisia kali, lakini kwasasa amekuwa kimya wakati wadau wakimkubali mno.

Bell 9: amepitia mambo mengi katika safari yake ya muziki hadi kufika hapo licha ya kuonekana bado ana kazi ya kufanya kimuziki.

BINGWA: lilipata nafasi ya kufanya mahojiano naye ambapo amezungumza mengi kuanzia maisha yake binafsi hadi muziki wake.

BINGWA: Kitu gani kimekufanya kuwa kimya tangu ulipoanza shughuli za kufanya muziki kwenye sherehe za harusi?

Bell 9: Unajua tulianzisha kuhudumia muziki kwenye masherehe mbalimbali, lakini wateja wetu wakawa wanalalamika kuwa bei kubwa hivyo tukawa tunafanya ‘project’ (miradi) ya kuangalia jinsi gani tutashusha bei ndio maana nipo kimya kidogo.

Bell 9: Baadhi ya mashabiki zako wanaamini umeanza kupotea kiaina katika muziki kwa kutoachia nyimbo, je, unalizungumziaje?

Bell 9: Natambua sana ninachokifanya, najithamini na naamini nyimbo zangu ziliwapa mafundisho watu wa rika mbalimbali wazee kwa vijana, kwa     sababu zina mafundisho ya mapenzi ambayo yanagusa kila mtu, unajua nafanya mambo mengine kwanza na muziki pia.

BINGWA: Unalizungumziaje suala la kuvuma na kupotea kwenye muziki kwa baadhi ya wasanii hapa nchini?

Bell9: Mimi kwa upande wangu napambana na nina uhakika nitafika kule ninapopataka, kwani ndoto zangu kimuziki ni kufika levo za juu kabisa, hivyo suala la kuvuma na kupotea ndivyo muziki ulivyo kutokana na hali ya ushindani.

BINGWA: Unaweza kutuambia misingi gani umeiweka katika maisha yako?

Bell 9: Siri kubwa ya mimi ni kutokata tamaa kwani naamini hakuna mafanikio yanayokuja pasipo kuvuja jasho, bado ninaishi na ndoto zangu na napenda kufikisha ujumbe kupitia nyimbo zangu kwa jamii kwa kile kilichopo ndani yangu kupitia sanaa, na niliamua kutoa nyimbo za mapenzi ambazo  najua zinawakonga mioyo mashabiki zangu.

BINGWA: Vijana wengi vijana wengi hususan wasanii wamepotelea kwenye matumizi mabaya ya dawa za kulevya, wewe unalichukuliaje hili?

Bell 9: Suala hili linaumiza kweli kwani wengi bado vijana wadogo wanadanganyika na makundi yasiyofaa.

BINGWA: Unahisi ni kwanini wanakimbilia kuharibu maisha yao?

Bell 9: Ninachoweza kusema wanaingia huko kutokana na kupata vishawishi na kudhani maisha yatakuwa rahisi kumbe hawajui ndio wanajiteketeza.

BINGWA: Unawashauri nini vijana ambao wamejikita katika makundi yasiyofaa?

Bell 9: Ningependa kuwaambia kuwa maisha hayakimbiwi ni kupambana nayo, kwani ukijikita kwenye makundi mabaya unayaharibu maisha yako na kusababisha kuingia katika mambo ya uovu ambayo yatakufanya upoteze maisha kabisa.

BINGWA:    Unawashauri nini vijana chipukizi ambao bado hawajatoka kisanaa?

Bell 9: Ushauri wangu wajitume wasikate tamaa hata sisi tulianzia huko huko, hakuna mafanikio yanayokuja bila kupitia misukosuko.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU