UBORA WA SANAA ZAO UMEWABEBA KISIASA

UBORA WA SANAA ZAO UMEWABEBA KISIASA

365
0
KUSHIRIKI

NA WINFRIDA MTOI

UBORA wa kazi siku zote ndio kinachomfanya mtu akubalike sehemu yoyote, iwe ofisini, nyumbani au katika jamii inayomzunguka.

Ni wazi kuwa unapofanya jambo zuri katika jamii, inakufanya ujikusanyie mashabiki wengi, huku wakifuatilia hatua kwa hatua kwa kile unachokifanya na unapokwenda tofauti na matarajio yao lazima watakukimbia

Kazi ya sanaa hasa muziki na filamu ni moja ya sehemu yenye mashabiki wengi ukilinganisha na nyingine duniani ndio sababu wasanii wake kuwa wakitumika katika shughuli mbalimbali za kijamii na kitaifa.

Hata wanasiasa wengi hutumia wasanii maarufu katika kujipigia debe kwa wananchi hasa kipindi cha uchaguzi ambapo burudani huwa ndio kivutio kikubwa kwenye maeneo wanayopita kusaka kura.

Licha ya kutumika katika kampeni, miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mwamko mkubwa kwa wasanii kujiingiza kwenye ulingo wa siasa, nadhani ni baada ya kuona wenzao waliojaribu kufanikiwa.

Wengi wamefanikiwa katika ulingo huo wa siasa kwa kupata nafasi ya kushika nyazifa mbalimbali ndani ya vyama vyao, lakini hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na ubora wa kazi zao za sanaa walizofanya.

Ubora wa kile wanachokifanya umewafanya wajikusanyie mashabiki lukuki wanaowaamini kwa kila jambo, hivyo kuwapa nafasi ya kuwawakilisha katika maeneo tofauti.

BINGWA linakuletea baadhi ya wasanii waliotusua baada ya kuchaguliwa kuwa wabunge na wananchi wao.

Desmond Elliot

Ni mwigizaji nyota wa Nigeria aliyezaliwa mwaka 1974 na aliweza kujijengea jina kubwa kutokana na umahiri wake wa kuigiza katika filamu mbalimbali za Nigeria na Ghana.

Mwaka 2014, msanii huyo ambaye pia ni mwongozaji wa filamu, alijitosa kwenye siasa kupitia Chama cha APC, ambapo mwaka 2015 alifanikiwa kushinda ubunge kwenye Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo, akiwakilisha Jimbo la Surulere lililoko Lagos.

Bobi Wine

Msanii huyu wa muziki wa Uganda aliyeanza kuimba mwaka 2000, ni maarufu kwa nyimbo za reggae na raga. Jina lake halisi ni  Robert  Ssentamu Kyagulanyi, alifanikiwa kushinda  ubunge wa Kyadondo Mashariki  kama mgombea huru katika uchaguzi mdogo uliofanyika mwaka huu kwa kupata kura 25,659 kati ya kura 33,310 zilizopigwa.

Hata kwenye vurugu zilizotokea hivi karibuni katika Bunge la Uganda, alionekana mstari wa mbele kumpinga Spika wa Bunge hilo kutaka kuwatoa wabunge wa upinzani nje.

Jaguar

Si jina geni hata hapa nchini kwani aliwahi kufika kwa ajili ya kufanya kazi zake za muziki. Jaguar ambaye jina lake halisi ni Charles Njagua ni miongoni mwa wasanii waliopata ‘shavu’ kwenye ulingo wa siasa.

Jaguar ni mwanamuziki wa Kenya aliyeshinda kiti cha ubunge katika Jimbo la Starehe nchini humo katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka huu kupitia Chama cha Jubilee ambao hata hivyo ulirudiwa mwezi uliopita kwa nafasi ya urais pekee.

Profesa Jay

Mwanamuziki mkongwe wa hip hop Tanzania, Joseph Haule ‘Profesa Jay’, alishinda ubunge wa Jimbo la Mikumi, Morogoro, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2015.

Mr. Sugu

Jina lake halisi ni Joseph Mbilinyi ‘Mr Sugu’ ni mmoja wa wasanii wa mwanzo katika Bongo Fleva, walianza kuimba aina ya muziki wa hip hop. Mara ya kwanza alishinda ubunge wa Mbeya Mjini mwaka 2010 kupitia Chadema na mwaka 2015 alifanikiwa kutetea kiti chake.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU