SHILOLE: NDOA YANGU ITAKUWA YA KIFAHARI, YA KUMPENDEZA MUNGU

SHILOLE: NDOA YANGU ITAKUWA YA KIFAHARI, YA KUMPENDEZA MUNGU

392
0
KUSHIRIKI

NA KYALAA SEHEYE

KILA kijana anatamani umri ukifika awe na mwenza wake wanayesikilizana na kupendana kwa dhati bila kujali kama ni staa au wa kawaida, tajiri ama mwenye maisha ya kawaida.

Zuwena Mohamed ‘Shilole’, ni mmoja wa mastaa anayeamini mchumba wake wa sasa, Asharf Uchebe ‘Uchebe’, ndiye hasa mume aliyeandikiwa na Mungu pamoja na kupita kwa wanaume kadhaa kimahusiano kwa kuwa wanaendana na kusikilizana kwa kila hali kama alivyojinadi msanii huyo.

Shilole ambaye ni mama wa watoto wawili, licha ya awali kuwa na mahusiano na staa mwenzake wa Bongo Fleva, Nuhu Mziwanda, pia alishawahi kuolewa na wanaume wawili tofauti ambao wote kila mmoja alimzalisha.

Juu ya hilo, Shilole anadai kuwa ndoa zile hazikuwa na radhi za Mungu wala mapenzi ya kweli, bali zilikuwa ndoa ilimradi zilizotokana na shinikizo la wazazi.

Akizungumza na BINGWA mwishoni mwa wiki iliyopita, Shilole anasema kuwa anaamini Uchebe ndiye hasa mwanaume wa maisha yake na ndiye aliyechaguliwa na Mungu kwa kuwa tangu awe naye, anaona kabisa kila kitu kinanyooka.

“Mahusiano ambayo yana radhi za Mwenyezi Mungu utayaona hata mwelekeo wa kimaendeleo hata kama mnakwama, mnashauriana mfanye nini ili kufikia malengo. Nilianza uhusiano na Uchebe nikiwa mwanamuziki na mama lishe ila sasa hivi nimefanikiwa kufungua biashara nyingine ambayo tunaiendesha kwa kufuata misingi na maadili ya Muumba wetu, kwa kuwa mume wangu ni mcha Mungu mno,” anasema Shilole.

Aidha, aliongeza kuwa tangu Uchebe aingie katika maisha yake, ameona tofauti kubwa na hapo mwanzo amekuwa Shilole mwingine kabisa ambaye anajitambua na kujua nini anatakiwa afanye kwa wakati huu ilimradi afanikiwe kihalali na si kwa njia za kumuudhi Mungu, huku akisisitiza kuwa ndoa yake iko karibu na itakuwa ya kifahari mno na kumpendeza Mungu.

“Ndoa yangu ni Desemba 20, nitahakikisha inakuwa ya kifahari na  inampendeza Mungu kwa kuwa maisha ya kukaa chini ya kivuli cha Muumba ni mazuri na yana maendeleo kwa kuwa yeye ameyapa radhi zake, nimeona tofauti kubwa na taratibu nitafanya biashara zinazompendeza Mungu, ninaamini nitakuwa maarufu zaidi ya umaarufu nilionao,” anasema  Shilole.

Anasema kuwa awali alipoteza mwelekeo baada ya kupata wanaume waliokuwa wanakuja kwake kwa maslahi na si mapenzi, kwani walikuwa wakimtegemea yeye kwa kila kitu hata mawazo ya kimaendeleo walishindwa kumpa na mwisho wa siku kufanya vitu vya ajabu na wao kumpa sapoti kubwa kitu ambacho kwa Uchebe hakipo kabisa.

“Kabla ya Uchebe wanaume waliokuja kwangu walikuja kimaslahi, hawakuwa na mapenzi ya kweli, walikuwa wakitaka kulelewa kwa manufaa yao, ila  yeye yuko tofauti mno, ni mwanaume anayejali na kujua majukumu yake hata kama unaanzisha kitu kwa pesa zako, atataka mshirikiane ili mpate faida na yeye anatumia nguvu zake kuhakikisha kinakua.

“Pia, amenipa misingi bora ya kumwamini Mungu tofauti na zamani na toka nimeingia kwenye imani na Muumba wangu, kila kitu kwangu kinanyooka hii ni faraja kwangu na ninaamini kote nilikuwa napoteza muda na kujifunza maisha aliyeumbwa kwa ajili yangu ni Uchebe pekee,” anasema Shilole.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU