ASLAY KUZISAMBARATISHA TEAM KIBA, TEAM DIAMOND LEO?

ASLAY KUZISAMBARATISHA TEAM KIBA, TEAM DIAMOND LEO?

687
0
KUSHIRIKI

NA JESSCA NANGAWE

HITIMISHO la msimu wa Tigo Fiesta unatarajia kuhitimishwa leo kwenye viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam, huku mashabiki mbalimbali wakisubiri kwa hamu kuhudhuria tukio hilo la kihistoria kwenye kiwanda cha burudani.

Pamoja na kutokuwapo kwa msanii wa kimataifa kama ilivyozoeleka, lakini mashabiki wa burudani wameonekana kuridhishwa na wasanii wa hapa nyumbani ambao soko la ushindani limezidi kujidhihirisha kadiri muda unavyokwenda na kuwafanya wazidi kufanya vizuri.

Licha ya wasanii kama Rostam, Maua Sama, Nandy na wengine kufanya vizuri katika msimu huu wa Tigo Fiesta, lakini macho ya mashabiki wengi yanamtazama zaidi kijana mdogo, Aslay ambaye ameonekana kuja kwa kasi zaidi kupitia nyimbo zake, hasa baada ya shoo zake za mikoani kufanya vizuri.

Uwapo wa Aslay katika tamasha la leo, huenda ukawasahaulisha mashabiki wa Ali Kiba na Diamond uwezo wa nyota hao ambao wote wametoa nyimbo mpya hivi karibuni ambazo zimefanya vizuri na badala yake, wakaelekeza zaidi masikio yao kwa kijana huyo ambaye kwa sasa ni kipenzi cha mashabiki wengi wa muziki hapa nchini.

Ali Kiba kwa sasa anatamba na wimbo wake wa Seduce Me, huku Diamond akiwa na kibao matata cha Hallelujah, zote zikiwa zimepokewa vizuri mno na mashabiki.

Akitamba na nyimbo zake mpya za Pusha, Natamba, Mario, Danga, Rudi, Kidawa na nyinginezo, Aslay anatajwa kuwa msanii aliyeongoza kwa kupewa ushirikiano wa hali ya juu na mashabiki wakati wote wa tamasha la Tigo Fiesta ambapo mashabiki walikuwa wakiimba naye na kucheza nyimbo zake kwa hisia kali.

Kukosekana kwa Diamond katika tamasha la leo, huku Ali Kiba akiwapo, kunaweza kufungua mlango kwa Aslay kupata sapoti zaidi kwani hakutakuwapo ushabiki wa Team Kiba na Team Diamond kama ilivyojitokeza katika matamasha yaliyopita.

Akizungumzia tamasha hilo lenye kaulimbiu ya ‘Tumekusoma’ ambalo litahusisha zaidi ya wasanii 18, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa Tigo, William Mpinga, alisema kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 16 ya tamasha hilo, Tigo Fiesta ilikuwa imewashirikisha wasanii wa Kitanzania pekee.

 

“Kilele cha msimu wa Tigo Fiesta 2017 kitawahusisha wasanii wa Kitanzania pekee. Tigo imejikita kuleta mageuzi makubwa kwa kuinua vipaji vya wasanii wa Kitanzania kama njia mojawapo ya kukuza sanaa na ajira kwa vijana nchini. Tumewakutanisha wasanii wetu maarufu na mashabiki wao katika mikoa yote 16 tuliyotembelea na kuwajengea uwezo wa kutumbuiza laivu mbele ya halaiki kubwa ya watu,” alisema Mpinga.

 

Alisema wameamua kutumia wasanii wa ndani kwani wameona wana uwezo wa kukata kiu ya muziki ya Watanzania bila hata kuwa na msanii kutoka nje ya nchi.

Mpinga alisema katika matamasha ya mikoani, wasanii hao wamethibitisha kuwa wanaweza kuwaburudisha mashabiki wao kwani walifanya mambo makubwa, huku pia mwitikio wa mashabiki ukiwa ni mkubwa kwa kuwa wengi walijitokeza kushuhudia burudani kutoka kwa wasanii wao.

 

“Kununua tiketi ni rahisi. Fuata utaratibu wa kawaida wa kutuma pesa na tuma Sh 9,000 kwenda namba ya Tigopesa 0678 888 888. Hapo hapo utapokea ujumbe mfupi wa SMS unaothibitisha manunuzi yako ya tiketi. Hifadhi huo ujumbe mfupi. Baadaye utapokea maelekezo ya jinsi na wapi pa kwenda kuchukua tiketi yako. Bei halisi ya tiketi getini ni Sh 10,000,” alisema Mpinga.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandilizi ya Tigo Fiesta 2017, Sebastian Maganga, aliwataka wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi Leaders Club akiwaahidi kupata burudani ya hali ya juu, huku pia akiwahakikishia ulinzi wa kutosha, hasa wakati wa kutoka.

 

“Tamasha la Tigo Fiesta litaanza mapema tu, milango itafunguliwa saa sita mchana na kutakuwa na matukio mbalimbali yanayolingana na muda huo na itakapofika saa moja jioni, moto utawashwa rasmi kwa wasanii kuanza kulishambulia jukwaa kama nyuki hadi saa saba usiku,” alisema Maganga.

Maganga aliwataja wasanii watakaotoa burudani kesho katika tamasha hilo kuwa ni Ali Kiba, Aslay, Ben Pol, Barnaba, Chege, Darasa, Dogo Janja, Jux, Fid-Q, Rostam (Roma na Stamina), Rich Mavoko na Nandy.

 

Wengine ni Mr Blue, Vanessa Mdee, Maua Sama, Zaiid, Lulu Diva, Mimi Mars, Rosa Ree, Chin Beez, Nyandu Tozi, Nedy Music, Ommy Dimpoz, Bright, Weusi (Joh Makini, G-Nako na Nikki wa Pili) na wengineo.

 

Alisema tamasha hilo kwa mwaka huu limezunguka katika mikoa ya Arusha, Kahama, Musoma, Mwanza, Tabora, Dodoma, Iringa, Songea, Njombe, Sumbawanga, Kigoma, Morogoro, Tanga, Mbeya, Moshi na Mtwara.

 

Wakizungumzia maandalizi yao, wasanii watakaopanda jukwaani kesho wameahidi kutowaangusha wakazi wa Dar es Salaam na vitongoji vyake watakaofika Leaders kesho.

Ben Pol akizungumza kwa niaba ya wenzake, alisema wamejipanga vilivyo kufanya mambo makubwa kesho, kila mmoja wao akiwa amepanga kufanya ‘surprise’ ya aina yake itakayoifanya siku hiyo kuwa ya kukumbukwa.

“Wapenzi wa burudani waje kwa wingi Leaders kushuhudia tukihitimisha msimu huu wa Tigo Fiesta kwa weledi wa aina yake, kila mmoja wetu amejiandaa vya kutosha kufanya shoo ‘bab kubwa’, karibuni sana,” alisema.

Naye Vanessa Mdee, alisema: “Wakazi wa Dar es Salaam watarajie shoo kabambe zaidi ya ilivyokuwa mikoani, kwa upande wetu wasanii tumejipanga kufanya shoo kali, hatutawaangusha hata kidogo.”

Kwa upande wake, Aslay alisema amejipanga vilivyo kuhakikisha anafanya shoo ya nguvu jijini Dar es Salaam kesho kama ilivyo kawaida yake.

“Jumamosi (leo) pale Leaders Club, Dar es Salaam ndio kilele cha Tigo Fiesta, nimejipanga kufanya mambo makubwa hivyo wapenzi wa muziki na burudani wajitokeze kwa wingi siku hiyo sitawaangusha hata kidogo,” anasema.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU