LIGI BORA ITATOA TIMU BORA YA TWIGA STARS

LIGI BORA ITATOA TIMU BORA YA TWIGA STARS

205
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY

PAZIA la msimu mpya wa Ligi ya Wanawake ngazi ya taifa lilifunguliwa rasmi jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, katika viwanja vya General Tyre, mkoani Arusha.

Ligi ya Wanawake msimu huu inashirikisha jumla ya timu 12 zilizogawanywa katika makundi mawili, ambapo Kundi A linalohusisha timu za Mlandizi Queens, JKT Queens, Mburahati, Fair Play FC, Simba Queens na Evargreen Queens wakati Kundi B likiwa na timu ya Marshi FC, Kigoma Sisters, Panama FC, Baobab Queens, Majengo Queens na Alliance Queens.

Huu ni msimu wa pili Ligi ya Wanawake kitaifa kufanyika, ambapo msimu uliopita bingwa alikuwa Mlandizi Queens ya Pwani iliyoweka historia ya kutopoteza mchezo hata mmoja kwenye hatua ya sita bora ikipata pointi 15 wakati JKT Queens ilimaliza nafasi ya pili ikiwa na pointi 12 na Kigoma Sisters ikishika nafasi ya tatu baada ya kujikusanyia pointi saba.

Mwenyekiti wa Chama cha Soka ya Wanawake (TWFA), Amina Karuma, alisema msimu uliopita walikutana na changamoto nyingi ambazo mwaka huu kupitia kamati yake ya mashindano wameweza kuhakikisha zinapungua.

“Msimu uliopita ikiwa ndio mara ya kwanza, tuliweza kukutana na changamoto nyingi katika kuendesha ligi hiyo na ndiyo maana msimu huu tukaamua kuanza kuweka mikakati mapema,” alisema.

Amina alisema mafanikio yaliyoonekana msimu uliopita ni kutokana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kusaidia TWFA kwa hali na mali ikiwemo kuwapa mwongozo wa nini cha kufanya kuanzia hatua ya mwanzo wa mashindano hayo hadi fainali.

“Kwa msimu huu changamoto kubwa ni suala la udhamini kwani ili ligi iwe bora zinahitajikla fedha za kuendesha mashindano, hivyo wito wetu kwa wadau wajitokeze kutusapoti kwani tunapokea wadhamini wa kutusaidia kwenye jambo lolote litakalochangia kulifanya soka la wanawake kukua Tanzania na siku moja liweze kututoa kimasomaso katika mashindano ya kimataifa,” alisema Mwenyekiti wa TWFA akisisitiza ligi hiyo ndiyo itakayotoa timu bora ya Twiga Stars (timu ya taifa ya wanawake).

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau, alisema soka la wanawake ni moja ya mambo yaliyokuwepo kwenye sera za Rais wa TFF, Wallace Karia, hivyo lazima watendaji waliopo nyuma yake walitekeleze kulingana na jinsi ilani inavyotaka.

“Rasmi ligi ya wanawake taifa ilianza msimu uliopita hivyo safari hii ni ya pili, kupitia changamoto zilizotokea kipindi cha nyuma, TFF kwa kushirikiana na TWFA tumeweza kutatua baadhi ya mambo lakini bado nyingine tunazifanyia kazi huku suala kubwa likiwa ni kupata wadhamini zaidi ya mmoja kama ilivyokuwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara,” alisema.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU