‘MISS WORLD’ IMEMALIZIKA, TANZANIA TUJIPANGE SASA

‘MISS WORLD’ IMEMALIZIKA, TANZANIA TUJIPANGE SASA

359
0
KUSHIRIKI

NA CHRISTOPHER MSEKENA

KILELE cha shindano la urembo la dunia (Miss World) lilifanyika Novemba 18 mwaka huu huko Sanya nchini China na kuwakutanisha warembo 120 kutoka  kila pembe ya dunia na hatimaye mrembo kutoka India, Manushi Chhillar, akishinda taji hilo kubwa duniani.

Shindano hilo lililokuwa na msisimko wa aina yake, limeendelea kujizolea umaarufu kufuatia mikakati yake iliyolenga kulibakiza kwenye ubora ule ule toka lilipoanzishwa mwaka 1951.

Kupitia shindano la mwaka huu la urembo la dunia (Miss World) kuna mambo kadhaa ya kujifunza ili ndoto yetu ya kutwaa taji hilo kubwa la urembo siku moja itimie.

Inafahamika kuwa mwaka huu shindano la Miss Tanzania halijafanyika kwa hoja ambazo Waziri mwenye dhamana na sanaa, Dk. Harrison Mwakyembe, alizitoa kwa waandaaji wa shindano hilo akiwataka wajipange na kuboresha shindano kwa kutoa zawadi kwa wakati kama wanavyoahidi.

Waziri Mwakyembe, alitoa uamuzi huo kufuatia Miss Tanzania mwaka 2016/17, Diana Edward, kutopewa zawadi zake, yaani fedha na gari aliloahidiwa ndani ya muda uliopangwa jambo lililoitia doa tasnia ya urembo nchini.

Hivyo basi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alikuwa sahihi kabisa kutaka uboreshwaji wa shindano hilo linalotegemewa kutuletea taji la Miss World siku za usoni.

Oktoba 19 mwaka huu, kamati ya shindano la Miss Tanzania ikaamua kufanya maamuzi ya kumteua mrembo, Julitha Kabete, abebe bendera kwenda nchini China kutuwakilisha kwenye shindano hilo.

Kamati ilimteua mrembo huyo baada ya kujiridhisha kuwa, Julitha ni mzoefu wa mashindano ya urembo ya ndani, uelewa wa vivutio vya utalii na rasilimali nyingine zilizopo nchini hali kadhalika ana nidhamu ya kutosha iliyomfanya afanye vizuri kwenye shindano la Miss Tanzania mwaka 2016 kuanzia ngazi ya kitongoji, mkoa, kanda hadi fainali na kupata fursa ya kushiriki mashindano ya urembo ya Afrika (Miss Africa) mwaka huo huo.

Hivyo basi Julitha alikuwa amekamilika kuiwakilisha Tanzania kwenye shindano la Miss World. Na hakika alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuitangaza nchi yetu pale ambapo aliingia Top 20 ya warembo wenye tija kwa jamii kupitia mpango wake wa kutoa elimu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Hayo ni mafanikio makubwa kwetu ukilinganisha muda tuliojiandaa mpaka kufikia hatua hiyo. Shindano la Miss World limemalizika na mrembo wa Tanzania (Julitha Kabete) kuweza kufikia hatua hiyo kubwa kwake.

Sasa mpaka hapo unaweza kuona ni namna gani maandalizi yanavyoweza kuwa na mchango mkubwa katika ushindi.

Mrembo wa Kihindi, Chhillar, amekidhi vigezo na kuweza kutwaa taji la Miss World kutokana na maandalizi ambayo ameyafanya kuanzia nchini kwao India yaliyompa nafasi ya kushinda.

Mashindano ya urembo nchini India hayana ubabaishaji, yanafanyika kila mara na kuwa na msisimko mkubwa hivyo mrembo anayepatikana kwenye mashindano yao anakuwa na viwango vya kushindana popote pale duniani na akashinda.

Lakini hapa kwetu, hali bado si shwari, shindano la Miss Tanzania linahitaji kufanyiwa marekebisho yale aliyoyasema Waziri ili tuwe na uwezo wa kushindana na wenzetu.

Navuta picha ya Julitha Kabete, mrembo aliyetuwakilisha kwenye shindano la Miss World 2017, endapo angepata maandalizi ya kutosha hapa nyumbani pamoja na uzoefu wake wa mashindano ya kimataifa.

Haina shaka angefanya vizuri zaidi, Tanzania isingeishia kwenye ‘Top 20’ ya Beauty with a Purpose’, tungesogea ngazi nyingine za juu. Muda bado upo, shindano la mwaka huu limemalizika, huu ni muda mzuri wa kamati ya Miss Tanzania kujipanga na kutuletea shindano bora zaidi kwa ajili ya mwakani.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU