SIMBA BADO HAWAJAAMUA KUWA MABINGWA

SIMBA BADO HAWAJAAMUA KUWA MABINGWA

1906
0
KUSHIRIKI

NA AYOUB HINJO

JUMAPILI iliyopita timu ya Simba ilishindwa kutamba mbele ya Lipuli baada ya    kutoka sare ya 1-1, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa katika Dimba la Uhuru, uliopo jijini Dar es Salaam.

Hakika ulikuwa mchezo wa kuvutia kutokana na ufundi ulioonyeshwa na timu zote mbili, lakini Simba walishindwa kupata pointi zote tatu, baada ya kushindwa kutumia nafasi nyingi walizozitengeneza.

Takwimu pekee baada ya mchezo kumalizika zilitosha kutuonyesha kuwa Simba walistahili kushinda, lakini kushindwa kwao kutumia nafasi za wazi walizozitengeneza lilikuwa kosa kubwa kwao.

Mashuti yaliyolenga lango yalikuwa 12, mashuti yaliyopita nje ya lango yalikuwa saba na umiliki wa mpira ulikuwa asilimia 61. Hizo ni takwimu muhimu kwa upande wa Simba, kwa ufupi unaweza kusema mchezo huo ulikuwa mikononi mwao.

Inaaminika timu kubwa huchukua pointi kwa timu ndogo au zilizoizidi uwezo ili kujiweka sawa au kujihakikishia nafasi ya ubingwa itakapofika mwisho wa msimu.

Aina ya kikosi walichonacho Simba sasa kimeshindwa kuwa na muunganiko mzuri, licha ya kuwa na wachezaji wazuri kila idara.

Muunganiko wa timu umeshindwa kufanya kazi kwa wakati husika kiasi cha kutegemea matokeo kutokana na uwezo binafsi wa mchezaji.

Kikosi chao kina John Bocco, Haruna Niyonzima, Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude, Laudit Mavugo, Erasto Nyoni, Mohammed Hussein na wengine wengi bila kumsahau Emmanuel Okwi ambaye hakujumuika na timu hiyo katika michezo miwili iliyopita.

Kwa namna moja au nyingine kikosi cha Simba kinaonekana si bora kutokana na kocha wao, Joseph Omog, anavyoipanga timu hiyo au jinsi anavyotumia mbinu zake.

Kuwa na kikosi imara na bora basi kocha anatakiwa kufanya kazi ya ziada ili timu yake ifike katika kiwango anachokitarajia.

Thamani ya kikosi cha Simba ni bilioni 1.3 kama ilivyoelezwa na Haji Manara, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo.

Lakini thamani yao inashindwa kuonekana kwenye michezo ambayo unaamini Simba wataondoka na pointi tatu, baada ya mchezo kumalizika.

Kocha anachangia kwa kiasi kikubwa timu yake kuonekana bora au ya kawaida. Kikosi cha Simba kinaonekana cha kawaida tu licha ya kutumia pesa nyingi kwenye usajili wa wachezaji wengi nyota.

Binafsi naamini hakuna utofauti mkubwa kati ya Simba iliyotwaa ubingwa mwaka 2012 na hii ya sasa, lakini utofauti mkubwa upo kwa makocha ambao wapo kwenye vikosi vyao.

Mwaka 2012 kocha alikuwa Milovan Cirkovic ambaye aliisuka timu hiyo na kuwa tishio hapa nchini na katika michuano ya kimataifa ambayo Simba ilishiriki. Hata aina ya wachezaji waliokuwepo kipindi kile hawatofautiani sana na hawa waliopo sasa.

Hiki kikosi cha sasa kimekosa utimamu wa mwendelezo wa ubora wao kutoka kwenye mchezo mmoja kuelekea mwingine. Endapo Omog akiamua Simba kuwa mabingwa basi watakuwa mabingwa sababu kila kitu kipo mikononi mwake.

Itazame Manchester City ilivyo na inavyoshinda michezo yake. Inakuonyesha kabisa hawa wanahitaji ubingwa,  maana wamekuwa wakihakikisha wanachukua pointi tatu kwanza dhidi ya timu ndogo au za daraja la kati kabla hawajakutana na vigogo.

Uhakika wa kushinda ubingwa unaanzia katika kupata matokeo dhidi ya timu za kawaida kabla hujakutana na vigogo. Kila mmoja hakushangaa kuona Simba imetoa sare dhidi ya Azam na Yanga ni kutokana na ukubwa wa timu hizo, hilo halikumshangaza mtu, lakini kutoa sare na Lipuli ni utani uliovuka mipaka.

Jumamosi iliyopita  Yanga alitoa sare ya 1-1 na Prisons, ilitegemewa Simba angeshinda dhidi ya Lipuli ili kuweka pengo la pointi nyingi dhidi ya timu anazofukuzana nazo kwenye ubingwa, japo utetezi wao ni kwamba mpira una matokeo matatu (kushinda, sare na kufungwa).

Kwa timu zinazojielewa hiyo ilikuwa nafasi ya kumuacha mpinzani. Bado nitaendelea kuwatumia Manchester City kama mfano sababu wamekuwa wakionyesha hilo kwa uwazi, baada ya wapinzani wao Manchester United kuteleza kwenye michezo yao.

Wameutumia mwanya huo kujitanua kileleni na kuweka pengo la pointi nyingi baina ya timu hizo. Naamini Simba bado haijaamua kuwa bingwa, ikiamua kuwa bingwa watakuwa mabingwa, hilo halina shida kama wataamua kuamka.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU