MO KUMLETA KIBOKO YA BWALYA SIMBA

MO KUMLETA KIBOKO YA BWALYA SIMBA

3772
0
KUSHIRIKI

SAADA SALIM NA EZIEKIL TENDWA

MARA baada ya kutangazwa rasmi kuwa mwekezaji mpya wa klabu ya Simba, tajiri Mohamed Dewji (Mo) amepiga ‘stop’ usajili wa mshambuliaji wa Nkana Rangers, Walter Bwalya na sasa anamtaka kiboko wa nyota huyo, Jesse Were wa Zesco United ambaye ameibuka kinara wa mabao wa Ligi Kuu Zambia iliyomalizika hivi karibuni.

Simba ilianza kumfukuzia Bwalya ambaye pia anasakwa kwa udi na uvumba na mahasimu wao Yanga kwa ajili ya kusajiliwa dirisha dogo lililofunguliwa Novemba 15, mwaka huu, lakini baada ya Mo kupewa timu, amezuia mchakato wa kumfukuzia nyota huyo na sasa mipango inaanza kunasa saini ya nyota wa Kenya, Were.

BINGWA limejulishwa kuwa bilionea huyo ameamua kumgeukia Were ambaye amemaliza msimu huu wa Ligi Kuu Zambia, akipachika jumla ya mabao 18, hivyo Simba wanaangalia namna ya kuanza kufanya mazungumzo na mchezaji huyo ambaye anadaiwa kuongeza mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo ya Zesco.

Chanzo cha ndani karibu na Mo kilisema: “Kwa sasa Simba inahitaji kuwa timu bora hapa nchini, baada ya mabadiliko haya tunatarajia kuona mabadiliko makubwa ndani ya kikosi hasa kuhakikisha wanafanya usajili mzuri kulingana na mahitaji ya mechi zinazotukabili ikiwamo Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.”

Mtoa habari huyo alisema kwa sasa bilionea huyo ameiambia Kamati ya Usajili kuachana na Bwalya na kuangalia uwezo wa Were ambaye ameonyesha kiwango kizuri Ligi ya Zambia.

“Nafasi ya Bwalya kuja kucheza Simba sidhani kama itakuwapo tena, kwa sasa mshambuliaji anayetakiwa ni Were, ambaye pia ndio aina ya mchezaji anayetakiwa na benchi la ufundi,” alisema mtoa habari huyo.

 

HAKUNA MAONI