KWA HILI LA NGOMA, ANGALAU YANGA WAMEONYESHA UKOMAVU

KWA HILI LA NGOMA, ANGALAU YANGA WAMEONYESHA UKOMAVU

1768
0
KUSHIRIKI

NA EZEKIEL TENDWA

TIMU zetu hizi kongwe za Simba na Yanga, zimekuwa zikiabudu wachezaji wa kimataifa ambao kwa namna moja ama nyingine, wanajiona kama wafalme kutokana na kupendwa na mashabiki.

Hakuna asiyekumbuka namna Emmanuel Okwi, alivyokuwa akiwachezesha Simba ngoma ya Kiganda, kipindi cha nyuma kiasi kwamba kuweza kuwapeleka Kaskazini, wakakubali, akawarudisha Kusini, wakamfuata tu na hata pale alipowarudisha Magharibi na Mashariki waliendelea kumtii.

Okwi ni kama alikulia Simba na akawa anawajua tabia zao ndiyo maana alifanya kila aliloliona yeye linafaa, lakini asiulizwe kitu japo kwa sasa angalau anaonekana kama amekuwa vile.

Kitu kilichokuwa kikimtofautisha Okwi na wachezaji wengine wa kimataifa ni tabia aliyokuwa nayo ya kutokomea kwao Uganda, pale alipokuwa akipewa mapumziko na baya zaidi alikuwa akizima simu zake zote kitu kilichokuwa kikizua taharuki kwa mashabiki.

Alikuwa akikaa kwao muda anaoutaka yeye na hata pale aliporudi kituo chake cha kazi, viongozi na mashabiki walikuwa wakimpokea kama mfalme, licha ya utovu huo wa nidhamu aliouonyesha ambao kwa hali ya kawaida ilitakiwa aadhibiwe.

Katika ulimwengu wa sasa wa soka, majina ya Cristiano Ronaldo wa Real Madrid pamoja na Lionel Messi wa Barcelona, ndiyo yanayovuma sana, lakini huwezi kuwaona wakileta masihara kwenye kazi yao, kwani wanajua wataadhibiwa na timu zao ikiwamo kukatwa mishahara, utamaduni ambao kwetu ni kama haupo.

Barani Ulaya mchezaji hata ana kiwango gani, hata kama analipwa mshahara kiasi gani lakini akionyesha utovu wa nidhamu, anaadhibiwa tofauti na huku kwetu mchezaji mwenye uwezo mkubwa anaweza akacheza na akili za viongozi na mashabiki atakavyo bila kufanywa lolote.

Angalau Yanga wameanza kuonyesha kile wenyewe wanachodai timu ni kubwa kuliko jina la mchezaji na hii ni kutokana na kumwekea ngumu mshambuliaji wao, Donald Ngoma, kwamba ajitetee kwanini asiadhibiwe kutokana na matendo yake mabaya.

Ngoma aliondoka nchini bila kupata baraka zote za uongozi na benchi la ufundi yeye mwenyewe akidai alikwenda kwao kutibiwa na sasa huenda akajutia maamuzi yake, kwani amewekwa kitimoto apeleke maelezo ya kina.

Kwa hali ambayo tuliizoea, ni kwamba kutokana na uwezo wa Ngoma aliouonyesha tangu atue hapa nchini, angeanza kubembelezwa japo ndiye mwenye makosa, lakini hiki wanachokifanya cha kumbana, kitaleta heshima kwa wachezaji wote waliopo na watakaosajiliwa baadaye.

Ni kweli kwamba Ngoma ni mchezaji mzuri, lakini uzuri wake usimfanye kuiona Yanga ipo kiganjani mwake kwani walikuwepo waliokuwa na uwezo zaidi yake, wakawa wanaheshimu uongozi na mashabiki wake.

Nina imani kwamba uongozi wa Yanga, utafika hatua umsamehe lakini hilo litakuwa funzo kwa wengine kwamba yeyote atakayefanya kosa, ataadhibiwa na atakayefanya vizuri atapata heshima yake kama ilivyokuwa kwa akina Edibily Lunyamila.

Hapa kwanza lazima nimsifu sana tena katibu mkuu wa klabu hiyo, Charles Mkwasa, kwani ni moja ya viongozi wanaosimamia nidhamu akijua kwamba, kama atawaacha wachezaji kila mmoja kuwa na maamuzi yake, basi Yanga itakuwa genge la wahuni.

Kama kweli hizi timu zetu zinataka zipige hatua, zinatakiwa zizingatie suala zima la nidhamu kuanzia kwa wachezaji mpaka kwa uongozi, vinginevyo itakuwa bora liende, lakini sasa nawaona Yanga wameanza kukunjua makucha.

Nina uhakika hata wachezaji wenzake watakuwa wamefurahia hatua hiyo ya uongozi kumkomalia Ngoma kujieleza kwanini aliwaacha katika kipindi kigumu cha mapambano na yeye kutimkia kwao bila taarifa.

Kama uongozi ungemruhusu tu kwenda kufanya mazoezi na wenzake bila kumuweka kitimoto, ingeleta picha mbaya kwa wengine, lakini hiki walichokifanya cha kumkalia kooni ajieleze kinagaubaga, kwanini aliondoka bila taarifa za kina, itarudisha nidhamu kwa wachezaji wote kwamba, Yanga ni kubwa na kila aliyepo hapo ni wa kupita tu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU