MABEKI WANAVYOIUMIZA KICHWA BARCA

MABEKI WANAVYOIUMIZA KICHWA BARCA

329
0
KUSHIRIKI

CATALAN, Hispania

SAFU ya ulinzi ya klabu ya Barcelona imeanza kupatwa na majanga. Wengine wameumia na waliobaki hatima yao haieleweki, kama watabaki au watasepa.

Nguvu kubwa ya Barca katika wiki za kwanza za msimu huu ni safu imara ya ulinzi, lakini mambo yameanza kubadilika na kocha wa klabu hiyo, Ernesto Valverde, anaona sasa umefika wakati mwafaka wa kusajili beki.

Katika dirisha la majira yaliyopita ya kiangazi, Barca ilikaribia kumsajili beki wa kati wa Real Sociedad, Inigo Martinez, lakini hawakufanikiwa, huku beki aliyetajwa sana miezi michache iliyopita, Yerry Mina, yeye anatarajiwa kutua Camp Nou mwakani akitokea Palmeiras.

Mwisho wa siku Barca walijikuta wakihamishia matumaini yao sasa kwa mabeki; Gerard Pique, Samuel Umtiti, Javier Mascherano na Thomas Vermaelen.

Kuanzia sasa watamkosa Umtiti hadi Februari, baada ya beki huyo kuungana na Mascherano kwenye orodha ya majeruhi (Mascherano anatarajiwa kurudi Desemba 17), hivyo kumwachia mtihani mkubwa Valverde.

Kwa kuzidisha changamoto, Mascherano anatajwa kuwa mbioni kuondoka Camp Nou, ambapo vyombo vya habari Hispania viliripoti kuwa tayari ameshasogezewa ofa mezani kutoka China na Marekani, hiyo ikiwa na maana kwamba katika dirisha lijalo la majira ya baridi anaweza kufungasha virago na kusepa.

Kilichobaki kwa benchi la ufundi la Barca ni kuombea Mascherano abaki hadi majira yajayo ya kiangazi ambapo nafasi yake pekee ya kucheza itategemea na Umtiti kama atapona haraka au la.

Maamuzi mengine ya mbadala yote anayo Valverde. Kuna kikosi B ambacho kina mabeki wa kati wanaofikiriwa kupandishwa kikosi cha kwanza hivyo ataamua kama wamekomaa ipasavyo kuitwa kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Rafael Jimenez ‘Fali’ na Jose Antonio Martinez, huenda wakaitwa lakini kama inavyojulikana hawatoruhusiwa tena kurudi kikosi B kama wakiichezea Barca kwenye La Liga kwani wote wana umri wa zaidi ya miaka 23.

Beki pekee wa timu ya vijana ambaye hajafikia vigezo vya kucheza michuano ya Ulaya au La Liga ni Rodrigo Tarin, ambaye hata hivyo naye ni majeruhi.

Valverde yupo njia panda. Kama Pique au Vermaelen wakiumia hivi sasa au wakiadhibiwa, basi kocha huyo atalazimika kuwatumia aidha Lucas Digne au Sergio Busquets, kwenye safu ya ulinzi wa kati, kitu ambacho hataombea kitokee.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU