MBAO YASAKA MILIONI 100/- KUJENGA KIKOSI

MBAO YASAKA MILIONI 100/- KUJENGA KIKOSI

351
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY

BAADA ya kushindwa kuonyesha makali waliyoyatarajia kwenye msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uongozi wa Mbao FC hivi sasa unahaha kusaka kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuboresha timu yao kuelekea mzunguko wa lala salama.

Hadi hivi sasa Ligi Kuu ikiwa imesimama, Mbao imecheza michezo 11 ambapo wamepata droo tano, kushinda mara mbili pamoja na kupoteza mechi nne hivyo kujikusanyia pointi 11.

Taarifa ambazo BINGWA limezipata kutoka ndani ya Mbao zinasema kuwa licha ya kuomba timu mbalimbali kuwapa wachezaji kwa mkopo, lakini wanasaka kiasi cha Sh  milioni 100 kitakachowasaidia katika uendeshaji wa timu kwenye mzunguko wa pili.

“Ukiondoa suala la usajili ambalo tunataraji kupata wachezaji wengi kutoka timu za Ligi Kuu watakaokuja kwetu kwa mkopo, lakini kuna suala la gharama za uendeshaji wa timu kuanzia mishahara, kambi, posho na hata usafiri ambalo lipo chini yetu.

“Kwa haraka haraka ili tuweze angalau kucheza kwa ushindani mzunguko wa lala salama, lazima tuwe na fedha kiasi kisichopungua Sh    milioni 100 ambazo pia haziwezi kukidhi mahitaji lakini tukipata zitatusogeza,”     alisema mtoa habari huyo.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa, kutokana na mahitaji ya fedha waliyonayo wameamua kuanza mchakato wa kutafuta wadhamini na wafadhili kutoka katika makampuni mbalimbali ambao wataweza kuwasaidia.

BINGWA lilimtafuta Mratibu wa Mbao FC, Masalinda Njashi, ili kutaka kujua juu ya jambo hilo ambapo alikiri kuwepo kwa hali mbaya kiuchumi, lakini si kwenye timu yao pekee  na hiyo inatokana na ugumu wa maisha ulivyo.

“Suala la uchumi kuyumba halipo Mbao peke yake bali kwa timu nyingi zinazoshiriki ligi msimu huu, lakini kila mmoja anahangaika na kuangalia jinsi ya kuisaidia timu isiweze kuyumba, hivyo hata sisi tangu ligi inaanza tulishaanza mchakato wa kutafuta wadhamini na bado tunaendelea nalo.

“Siwezi kuzungumza moja kwa moja juu ya kusaka hicho kiasi cha fedha, lakini suala la kuwatafuta wadhamini lipo, tunahitaji kiasi kikubwa cha fedha ili timu yetu iweze kucheza soka la ushindani,” alisema.

Hadi sasa Mbao tayari imefanikiwa kuinasa saini ya mlinda mlango wa Azam FC, Boniphace Metacha,  aliyekwenda kwa mkopo lakini pia ikiwa kwenye mazungumzo na Yanga juu ya kuwachukua kwa mkopo wanandinga wake, Maka Edward na Yusuph Mhilu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU