MO DEWJI: SIMBA KUTORUDIA MAKOSA YA 1993

MO DEWJI: SIMBA KUTORUDIA MAKOSA YA 1993

1707
0
KUSHIRIKI

NA EZEKIEL TENDWA

AMA kweli Mohamed Dewji ‘Mo’ anaipenda mno Simba, kwani wakati baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo wakiwa wameshasahau kilichoitokea timu yao mwaka 1993, mfanyabiashara huyo bado anakumbuka na sasa ameweka wazi kuwa hawatarudia makosa waliyoyafanya mwaka huo.

Iko hivi! Mwaka huo Simba ilifanikiwa kutinga fainali michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika wakati huo likijulikana kama Kombe la Caf, lakini wakafungwa kizembe na Stella Abidjan ya Ivory Coast tena kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), Dar es Salaam.

Katika mchezo wa kwanza, Simba wakiwa ugenini walipambana vilivyo na kufanikiwa kupata suluhu,  lakini wakajikuta wakifungwa mabao 2-0 kwenye uwanja wao wa nyumbani na kuwafanya mashabiki wao kurudi nyumbani vichwa chini.

Simba ndiyo timu pekee nchini kujitutumua na kufika hatua hiyo ambapo wakati kila mmoja akiamini watamaliza mchezo mapema nyumbani baada ya kupata suluhu ugenini, ghafla wakafungwa mabao hayo 2-0 kitu ambacho kinautesa moyo wa Mo Dewji, mpaka leo.

Tayari Mo ameshatangaza kutoa donge nono la usajili baada ya mwishoni mwa wiki hii wanachama wa Simba kwa kauli moja kukubali kumpa timu awekeze hisa za 49%, huku mfanyabiashara huyo hasira zake zikiwa ni kuona timu yao ikitwaa makombe makubwa Afrika.

Kigogo mmoja wa Simba ambaye ni rafiki wa karibu wa ‘Mo’, ameliambia BINGWA kuwa bilionea huyo amekumbushia jinsi anavyoumia roho akiukumbuka mchezo huo dhidi ya Stella na sasa anataka kufanya kitu ambacho kitawafurahisha mashabiki wao.

“Ule mchezo Simba walioshindwa kutwaa ubingwa dhidi ya Stella Abidjan, bado jamaa (Mo Dewji), anaukumbuka na anasema anakereka sana jinsi mashabiki walivyomiminika uwanjani wakaondoka wakiwa wanyonge.

“Lakini pia kama unakumbuka Simba wanayo misimu kama mitano hivi tunashindwa kushiriki michuano ya kimataifa, kitu ambacho Mo anaona ni kama kushushwa hadhi kwa jina la klabu yetu ndiyo maana ukaona anatoa ahadi za kufanya usajili wa nguvu.

“Kilichopo tuzidi kuomba Mungu atupe uhai maana kama hayo aliyoyaweka kwenye mipango yake yatakwenda vizuri, bila shaka tutakuwa tukipambana na timu kubwa kama TP Mazembe, Al Ahly na nyingine kuliko sasa ambapo eti timu kama Lipuli inaweza kutusumbua,” alisema kigogo huyo.

mwisho

 

 

 

Yanga yaonywa kisa mbaya wa Okwi

NA MWANDISHI  WETU

UONGOZI wa klabu ya Prisons ya Mbeya, umeionya Yanga juu ya mpango wao wa kutaka kumsajili kinyemela mshambuliaji wa timu hiyo, Mohamed Rashid na kuwataka mabingwa hao kufuata utaratibu.

Yanga inadaiwa kumwania Rashid mwenye mabao sita hivi sasa katika ligi kuu kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi chake katika mechi za ligi ya kimataifa hapo mwakani.

Akizungumza na BINGWA jana, Katibu Mkuu wa Prisons, Avintishi Abdallah, alisema yeye kama mtendaji mkuu wa klabu hiyo mpaka kufikia jana walikuwa hawana taarifa yoyote juu ya straika kutaka kusajiliwa na Yanga zaidi ya kusoma katika vyombo vya habari.

“Mimi nasikia tu kupitia vyombo vya habari kuwa Rashid anatakiwa na Yanga, lakini hakuna mazungumzo yoyote mpaka sasa hivi kati yetu na     wenzetu wa upande wa pili kitu ambacho ni hatari sana kwa maendeleo ya soka letu,” alisema     Rashid.

Katibu huyo alikwenda mbali na kusema kumekuwapo na ujanja ujanja mwingi kuhusiana na Rashid kuhusishwa kutaka kusajiliwa na Yanga na kusisitiza kamwe hawatamwachia kirahisi nyota huyo kuondoka.

“Ukiongea na mchezaji anakwambia sijafanya mazungumzo na Yanga, lakini hapo hapo tunaonyeshwa picha yupo na viongozi wa Yanga sasa hii inatupa mashaka kwanini haya mambo yafanyike kwa siri kuna nini hapa,” alihoji Abdallah.

Alisema tayari uongozi wa Prisons umemtumia tiketi straika huyo na kumtaka aende Mbeya leo haraka kujiunga na wenzake kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya Ligi Kuu Bara.

“Jana tumemtumia tiketi aje haraka Mbeya kujiunga na wenzake hayo mengine kama yapo yataendelea kufanyika yeye akiwa huku, lakini mimi ninavyojua Rashid hawezi kuondoka kirahisi na kwenda kujiunga na Yanga,” alisisitiza.

Dirisha dogo la usajili linatarajiwa kufungwa Desemba 15, mwaka huu huku mambo yakionekana kuwa magumu kwa Wanajangwani hao katika harakati zao za kusajili wachezaji wengine kutokana na kuyumba kiuchumi.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU