TAHADHARI UGOMVI WA LIVER NA EVERTON USIINGILIE

TAHADHARI UGOMVI WA LIVER NA EVERTON USIINGILIE

265
0
KUSHIRIKI

MERSEYSIDE, Liverpool

WIKIENDI hii Ligi Kuu England itanogeshwa zaidi na mechi za wapinzani wa jadi, ambapo Liverpool inatarajiwa kuikaribisha Everton kwenye mtanange wa ‘Merseyside Derby’.

Timu hizo zitakutana kwa mara ya kwanza msimu huu huku Liver ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mabao 3-1 kwenye mchezo wa mwisho uliopigwa msimu uliopita.

Historia inaonesha kuwa Liver na Everton zikikutana huwa ni patashika nguo kuchanika. Mshindi kupatikana katika dakika za lala salama ni kitu cha kawaida.

Ukiona matokeo ya sare katika mechi hizo basi ujue ni lazima ‘damu imwagike’ kwanza. Aina za ushangiliaji ni za kusisimua halafu kadi nyekundu hutolewa kama njugu vile.

Hiyo ndiyo ‘Merseyside derby’. Mtandao wa Sky Sports umeziorodhesha mechi saba kali baina ya timu hizo tangu zilipoanza kukutana kwenye Ligi Kuu England.

Liverpool 3 Everton 2 – Aprili 1999

​Hii ilikuwa ni mechi ya kwanza ya mkongwe wa zamani wa Liverpool, Steven Gerrard na alikaribishwa na ushindi.

Everton ndio walioanza kuziona nyavu za Liver kupitia kwa Olivier Dacourt, lakini majogoo hao walibadili ubao wa matokeo na kunyakua ushindi.

Straika matata wa Liverpool wakati huo, Robbie Fowler, alisawazisha na kuongeza la pili huku akiyasindikiza mabao yake na aina ya kipekee ya kushangilia, kwa kutembea kama mbwa na kunusa chini kabla ya Patrik Berger kupachika la tatu. Francis Jeffers, ndiye aliyefunga bao la pili kwa upande wa Everton.

Almanusura Everton wasawazishe kama si juhudi za Gerrard kuokoa mpira uliokuwa unaelekea langoni katika shambulizi la dakika za mwisho.

Liverpool 0 Everton 1 – Septemba 1999

Haukuwa ushindi mnono ila kwa jinsi ambavyo Everton ilipambana na kuupata pale Anfield, mchezo huo umepata haki ya kuingia kwenye orodha ya mechi kali zaidi baina ya Liverpool na Everton.

Kilikuwa ni kichapo cha kisasi kwa ndugu zao hao. Ulikuwa ni mchezo mgumu na uliotawaliwa na rafu za hapa na pale ambapo wachezaji watatu walioneshwa kadi nyekundu kwenye mtanange huo.

Sander Westerveld na Gerrard kwa upande wa Liverpool waliwaacha wenzao uwanjani, huku Michael Owen akibahatika kuoneshwa kadi nyekundu. Kwa upande wa Everton, Jeffers naye yalimkuta.

Cha kufurahisha ni kwamba, kabla ya kadi nyekundu hizo, Everton ndio walikuwa wametoka kupata bao pekee kupitia kwa Kevin Campbell dakika ya nne tu ya mchezo.

Everton 2 Liverpool 3 – Aprili 2001

Kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka 10 kupita, Liverpool ilikuja kupata ushindi kwenye dimba la Goodison, licha ya kwamba walipunguzwa na kuwa 10 kufuatia beki Igor Biscan kulimwa kadi nyekundu.

Mchezo huo ulikuwa unaonekana kama ungeisha kwa sare kwani kila Liverpool walipofunga bao, Everton.

Liverpool walianza kuziona nyavu kupitia kwa Emile Heskey, Duncan Ferguson, akasawazisha. Markus Babbel akapiga la pili lakini David Unsworth akaifungia Everton la pili.

Hata hivyo, Garry McAllister, alipofunga bao kali la frikiki akiwa mbali mno Everton walisalimu amri na kukubali kichapo.

Liverpool 3 Everton 1 – Machi 2006

Ilikuwa ni siku mbaya sana kwa nahodha wa Liver, Gerrard, ambaye alijikuta akioneshwa kadi mbili za njano kwa kuwachezea vibaya wapinzani.

Kocha wa Liverpool wakati huo, Rafa Benitez, alishaelewa kuwa bila nahodha wao huyo, wachezaji wake wasingeweza kupambana. Lakini, aliwaomba na kuwasihi wacheze kwa kutumia akili na moyo wao wote kwani mashabiki wasingevutiwa kuona Everton wakishinda mchezo huo.

Liver walipambana na kupata mabao mawili ya haraka, ambapo beki wa Everton, Phil Neville, alijifunga na lingine kutupiwa kambani na Luis Garcia.

Tim Cahill aliwapa matumaini Everton kwa kufunga bao la kwanza lakini kadi nyekundu ya mchezaji mwenzake, Andy van der Mayde, ilivuruga kila kitu. Dakika za lala salama ndipo Harry Kewell alipoumaliza mchezo kwa kutupia la tatu kwa upande wa Liverpool.

Everton 3 Liverpool 0 – Septemba 2006

Miezi sita baadaye, Everton wakaja kulipiza kisasi bwana. Tena na rekodi zilivunjwa hapo hapo.

Ushindi huo mnono ulikuwa ni wa kwanza mkubwa kwa Everton ndani ya miaka 42 lakini pia ilikuwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kufunga mabao matatu kwenye mchezo wa ligi baina yao na Liverpool tangu mwaka 1966.

Cahill alifungua karamu ya mabao kabla ya Andrew Johnson kutupia mawili.

Bao la kwanza la Johnson lilitokana na uzembe wa beki, Jamie Carragher, ambaye alichezeshwa katika mtanange huo ikiwa ni siku chache sana tangu alipopona majeraha yake. La pili lilitokana na kipa Pepe Reina kushindwa kuzuia vyema shuti la Lee Carsley na kumtengea mpachika mabao huyo zawadi ya mpira na nyavu.

Everton 3 Liverpool 3 – Novemba 2013

​Katika mtanange huo wa miaka minne tu iliyopita, straika Romelu Lukaku alikaribia kuwa shujaa wa ‘derby’ yake ya kwanza kwa kufunga mabao mawili, lakini straika aliyetokea benchi siku hiyo, Daniel Sturridge, alimnyima nafasi hiyo kwa kuisawazishia bao Liverpool.

Hakika ulikuwa ni mchezo wenye burudani ya kutosha kutoka timu zote mbili. Mabao yalianza kufungwa haraka na mapema mno kupitia kwa Philippe Coutinho, Kevin Mirallas na Luis Suarez.

Mirallas alikuwa na bahati sana ya kukosa kuoneshwa kadi nyekundu kwa kumkanyaga vibaya Suarez. Hakuna mtu wa Liverpool siku ile ambaye ungemwambia Mirallas hakustahili kadi nyekundu na angekuelewa hadi leo.

Liverpool 4 Everton 0 – Januari 2014

Miezi kadhaa baadaye, timu hizo zilikutana tena na safari hii Everton ilikutana na moto mkali wa Suarez ambaye aliisaidia Liver kunyakua ushindi wa kwanza mkubwa tangu 1982.

Gerrard alitupia bao la kwanza kwa kichwa. Haikuishia hapo, Lukaku akaumia na Sturridge akatupia mabao mawili ndani ya dakika tatu.

Kama hiyo haitoshi, Suarez, akatupia bonge la bao na kuifanya Liverpool ikaribie kutwaa taji la Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza baada ya miaka 24.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU