TUTAVUNA KWA HIKI TUNACHOPANDA JUMUIYA YA MADOLA

TUTAVUNA KWA HIKI TUNACHOPANDA JUMUIYA YA MADOLA

148
0
KUSHIRIKI

TANZANIA ni moja ya nchi ambazo zitapeleka wanamichezo katika michuano ya Jumaiya ya Madola, itakayofanyika Aprili, mwakani Mji wa Gold Coast, Australia.

Katika michuano hiyo, Tanzania itawakilishwa na timu tano za michezo ya riadha, kuogelea, mpira wa meza, ngumi na paralimpiki, huku dalili za kufanya vizuri na kupata medali zikionyesha kutokuwapo, kutokana na maandalizi hafifu.

Matumaini kwa Tanzania kurejea na medali kama nchi za wenzetu  wanavyofanya vizuri katika michuano hiyo, tunaiona ni ndogo, kutokana na timu zitakazoshiriki kuonekana  kusuasua katika maandalizi yake.

Tumeanza kupata wasiwasi kwa wanamichezo wetu kuweza kufanya vema na baadaye kurejea na medali nchini kwa kuwa hawaonyeshi jitihada za kushindana na wenzao watakapokuwa Gold Coast.

Tunasema kwamba, kwa muda uliobaki kufikia michuano hiyo, tunauona ni mdogo kwa wanamichezo wetu kuweza kufanya maandalizi kwa kiwango cha kuchuana na mataifa mengine.

Mpaka sasa ni timu moja  ya meza ambayo imeanza kambi nchini China kupitia mpango wa diplomasia ya michezo, lakini nyingine hazifahamiki zitaanza lini kuweka kambi ya pamoja.

Kama tulivyosema, mwenendo tunaouona wa maandalizi kwa wanamichezo wetu unatutia shaka kwa kuwa hautupi matumaini ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Madola.

Tumemsikia Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi, amesema baadhi ya wachezaji wanaendelea na mazoezi kwenye klabu zao, lakini mazoezi ya pamoja yanategemea uwezo wa timu husika.

Lakini kufanya vizuri kwa mchezaji katika michuano ya Madola itategemeana na maandalizi, akijua wachezaji wengi wanaendelea na mazoezi kwenye klabu zao.

Tumeambiwa kwamba, mazoezi ya pamoja yanategemea uwezo wa timu, hata hivyo, kambi ambayo itagharamiwa na TOC msimu huu itategemeana na fedha kama zikipatikana.

BINGWA tunasema kwamba, Tanzania katika michuano ya Jumuiya ya Madola itavuna hiki ambacho kinapandwa sasa, kwani tunaona muda uliobaki kwa wanamichezo wetu kuweza kufanya maandalizi mazuri ni mdogo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU