UMEWAONA WALIONG’ARA LA LIGA WAKAFELI EPL?

UMEWAONA WALIONG’ARA LA LIGA WAKAFELI EPL?

509
0
KUSHIRIKI

LONDON, England


DILI nyingi zimewahi kufanyika kwa wachezaji wa La Liga kutua Ligi Kuu England (EPL). Kwa misimu miwili iliyopita, jumla ya mastaa 21 wameondoka Hispania na kujiunga na timu za England.

Huku wengi wakionekana kufanikiwa, wapo ambao walijikuta wakishindwa kung’ara kutokana na ugumu wa mikikimikiki ya EPL.

Lucas Perez

Arsene Wenger alivutiwa na mabao yake 17 akiwa na Derpotivo ya La Liga. Hata hivyo, licha ya kuigharimu Arsenal pauni milioni 17, nyota huyo wa kimataifa wa Hispania alichemsha kwani katika mechi 11 alizocheza, alifunga bao moja pekee.

Roberto Soldado

Ni staa mwingine aliyetokea La Liga akiwa kwenye kiwango kizuri lakini akajikuta anafeli England. Soldado alihamia Tottenham akiwa mmoja kati ya mastraika bora duniani kwani alikuwa ameifungia Sevilla mabao 59 katika mechi 101.

Soldado ni miongioni mwa wachezaji walionunuliwa na Spurs kuziba pengo la Gareth Bale. Wengine ni Nacer Chadli, Erik Lamela, Paulinho, Etienne Capoue na Christian Eriksen.

Soldado aliwagharimu pauni milioni 27 lakini alifunga mabao 16 pekee katika michezo 76 aliyocheza. Baadaye alirejea La Liga kujiunga na Villarreal.

Nolito

Ni msimu mmoja pekee uliotosha kwa Pep Guardiola kusema Nolito hafai kucheza Etihad. Akiwa na Celta Vigo, mchezaji huyo alikuwa moto wa kuotea mbali, akifunga mabao 39 katika mechi 100.

Man City wakatoa pauni milioni 13.8  kumsajili lakini alijikuta akiwa mchezaji wa akiba katika mechi nyingi kati ya 30 alizocheza akiwa na timu hiyo.

Robinho

Mbrazil huyo hakufurahia maisha ya England kwa kipindi chote cha miezi 18 alichokaa nchini humo. Kabla ya hapo, alikuwa staa kwenye kikosi cha Real Madrid, ambapo aliipa mataji mawili ya La Liga, akicheza mechi 32.

Pia, alikuwa mmoja kati ya mastaa wa kikosi cha timu ya Taifa ya Brazil, akicheza zaidi ya mechi 100. Hata hivyo, akiwa Etihad, alicheza mechi 41 pekee na kufunga mabao 14.

Hiyo ilionesha ni jinsi gani Man City ‘walibugi’ kutoa pauni milioni 32.5, kiasi cha fedha ambacho kilimfanya Robinho kuwa mchezaji ghali katika historia ya soka la England.

Angel Di Maria

Kwa kipindi hicho, mwaka 2014, Muargentina huyo alikuwa mchezaji ghali zaidi kununuliwa na klabu za England kwani Man United walitoa pauni milioni 59.7 kumnasa.

Man United walimnunua kutokana na makali yake alipokuwa na Real Madrid, ambapo alikuwa sehemu muhimu ya kikosi hicho kilichotwaa taji lake la 10 la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Licha ya kuwa hakuwa mfungaji mara kwa mara, mchango wa winga huyo ulikuwa chachu ya mafanikio hayo ya Madrid.

Di Maria alikianza vizuri kibarua chake Old Trafford, akifunga mabao mawili na kutoa ‘asisti’ mbili na kisha kutajwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Septemba kwenye kikosi hicho cha Mashetani Wekundu.

Kilichofuata baada ya hapo ni majeraha ya mara kwa mara na kujikuta akiipoteza namba yake ‘first eleven’. Haikuchukua mwaka mmoja kabla ya wachambuzi wa soka England kumtaja kuwa usajili mbovu wa Man United na ndipo alipopigwa bei PSG ambako pia kwa sasa hapati namba.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU