HEKO Z’BAR HEROES KUFIKA FAINALI ILA WAOMBENI RADHI WATANZANIA

HEKO Z’BAR HEROES KUFIKA FAINALI ILA WAOMBENI RADHI WATANZANIA

1871
0
KUSHIRIKI

NA CLARA ALPHONCE

NI furaha isiyo kifani kwa Zanzibar Heroes kutinga fainali katika michuano ya Kombe la Chalenji, baada ya kuwavua ubingwa Uganda kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa Uwanja wa Moi, Kisumu jana.

Ushindi wa Zanzibar Heroes umewatoa kimasomaso Watanzania wote, bila kujali upande mmoja wa nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya timu ya Bara, Kilimanjaro Stars kutolewa mapema kwenye michuano hiyo.

Tanzania ni nchi pekee katika michuano ya Chalenji ambayo iliwakilishwa na timu mbili, ambazo ni Zanzibar Heroes na Kilimanjaro Stars.

Kilimanjaro Stars mwaka huu haikuweza kufanya vizuri, baada ya kuambulia pointi moja tu katika michezo minne waliyocheza kwenye michuano hiyo.

Zanzibar Heroes sasa watakutana na wenyeji Kenya, waliofanikiwa kuwatoa Burundi kwa ushindi wao wa bao 1-0 katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa juzi.

Timu hizo mbili za Kilimanjaro Heroes na Kilimanjaro Stars zilipangwa Kundi A pamoja na Uganda, Rwanda, Libya na Kenya, ambao watakutana na Zanzibar Heroes katika mchezo wa fainali.

Ndugu hao walikutana katika mchezo wa pili wa michuano hiyo, na Zanzibar Heroes walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1.

Ukweli ni kwamba, si mara ya kwanza kwa Zanzibar Heroes kupata ushindi dhidi ya Tanzania Bara wanapokutana kwenye michuano tofauti tofauti.

Lakini ushindi wa safari hii ulipelekea vijana hao wa Visiwa vya Karafuu kuzidiwa na furaha na mwisho wachezaji hao kutoa matusi mazito dhidi ya watu wa Bara.

Katika busara ya kiubinadamu, kitendo hicho hakikuwa cha kiungwana kufanywa na wanasoka hao, kwa sababu michezo ni furaha na ushindani unabaki uwanjani, mkitoka hapo wote ni kitu kimoja.

Kwa upande wa Zanzibar, wao wameifanya jamii ya soka ianze kuamini kwamba soka ni uadui na kufikia kutoa maneno machafu ambayo yaliwadhalilisha ndugu zao wa Bara.

Upande ambao ulishukiwa na maneno makali ulihitaji kuona waliofanya kitendo hicho, ambao ni wachezaji wa Zanzibar Heroes, wakichukuliwa hatua kali na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).

Hata hivyo, Mwenyekiti wa ZFA, Ravia Idarous, alichukua hatua inayoonekana kuwa ni nyepesi kwa kuwataka nyota hao waombe msamaha, akigusia pia kwamba jambo hilo lilisababishwa na furaha kubwa waliyonayo.

Zanzibar Heroes na Kilimajaro Stars ni timu za Watanzania. Ni watoto wa baba mmoja. Kitendo kile kilikuwa si cha uanamichezo. Kina nguvu kubwa ya kututenganisha na kutengeneza uadui ambao hauna tija yoyote.

Ingefaa kusikia wenye mamlaka ya kusimamia mchezo wa soka Zanzibar wakichukua hatua zenye kutoa fundisho na kuonyesha kukerwa na kitendo kile.

Sisi ni ndugu na ndiyo maana ikifika wakati wa timu ya Taifa (Taifa Stars) tunaungana pamoja, wachezaji wa Bara na wa Zanzibar wanakuwa katika kikosi kimoja na kuwakilisha nchi moja ambayo ni Tanzania.

Tabia hiyo inajenga picha mbaya, hasa kwa vijana wadogo ambao wanakua katika soka kuona kuwa Bara na Zanzibar kwenye soka ni maadui wakubwa.

Viongozi wa Zanzibar na wachezaji wa Zanzibar Heroes hawana pa kujifichia kutokana na walichokifanya, hivyo wanatakiwa kutumia busara na kuwaomba radhi Watanzania wote wa Bara na Visiwani.

Busara hupisha shari, ni bora kujishusha ili kulinda heshima kuliko kujifanya jeuri halafu ukadhalilika na kudharaulika.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU