ZANZIBAR HEROES MBELE KWA MBELE

ZANZIBAR HEROES MBELE KWA MBELE

373
0
KUSHIRIKI

TIMU ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, imefanikiwa kuwavua ubingwa mabingwa watetezi wa michuano ya Kombe la Chalenji (Cecafa Challenge Cup), Uganda, baada ya kuwachapa mabao 2-1 katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa jana jioni nchini Kenya.

Kwa kutinga fainali ya michuano hiyo, Zanzibar Heroes itavaana na wenyeji Kenya katika mchezo wa fainali kesho kwenye Uwanja wa Kenyatta uliopo Machakos, Kenya.

Kwa upande wao, Kenya walitinga fainali baada ya kuitoa Burundi kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza wa nusu fainali juzi.

Katika mchezo wa jana, hadi kipindi cha kwanza Zanzibar Heroes na Uganda walikuwa wamefungana bao 1-1 kabla ya vijana wa Tanzania Visiwani kupata bao la pili kwa mkwaju wa penalti iliyofungwa na Mohammed Issa ‘Mo Banka’.

BINGWA tunapenda kuwapongeza wachezaji na benchi la ufundi la Zanzibar Heroes kwa mafanikio yao hayo kwenye michuano hiyo, ukizingatia kuwa haikuwa kazi rahisi kufanya hivyo.

Kama kila mmoja wetu alivyoshuhudia, timu hiyo ilifanya kazi kubwa kwa kuzifunga timu zilizokuwa zikipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kama Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ na Rwanda, lakini pia ikiitoa jasho Libya.

Kwa kiasi fulani, mafanikio ya Zanzibar kwenye michuano hiyo hadi kufika fainali, yalitokana na juhudi, maarifa pamoja na uzalendo wa hali ya juu wa wachezaji wa timu hiyo.

Na sasa kikosi hicho kinapojiandaa kushuka dimbani kesho kuvaana na Kenya katika fainali, BINGWA tunawatakia kila la heri tukiamini vijana wetu hao wana kila sababu ya kushinda na kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Ifahamike kuwa mafanikio ya timu hiyo Chalenji si tu ya Wazanzibari, bali pia wapenzi wa soka wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla.

Hilo linathibitishwa na jinsi ambavyo mashabiki wa soka Tanzania Bara walivyokuwa wakiisapoti vilivyo timu hiyo tangu mwanzo, hata kabla ya kutolewa kwa Kilimanjaro Stars.

Hivyo basi, timu hiyo inapojiandaa kuvaana na Wakenya kesho, ni vema kila mpenzi wa soka Zanzibar na Tanzania Bara kwa ujumla, kuelekeza dua kwa vijana wetu hao ili waweze kufanya vema na kurejea na kombe hapa nchini. Hongereni Zanzibar Heroes na kila la heri kuelekea mchezo wa fainali kesho.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU