ZANZIBAR HEROES WAJIPANGE KWA MWAKANI

ZANZIBAR HEROES WAJIPANGE KWA MWAKANI

333
0
KUSHIRIKI

TIMU ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, imeshindwa kuchukua ubingwa Kombe la Chalenji (Cecafa Challenge Cup), baada ya kufungwa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 3-2 na Kenya katika mchezo wa fainali uliochezwa jana Uwanja wa Kenyatta, Machakos, jijini Nairobi, Kenya.

Ubingwa wa michuano hiyo ulilazimika kuamuliwa kwa mikwaju baada ya timu hizo kutoka sare ya kufunga mabao 2-2 ndani ya dakika 120.

Zanzibar Heroes walitinga fainali baada ya kuifunga mabao 2-1 Uganda katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa wiki iliyopita.

Kenya walitinga hatua hiyo baada ya kuitoa Burundi kwa bao 1-0 katika mchezo wa nusu fainali.

Katika mchezo wa jana, Zanzibar Heroes walifungwa bao la mapema ikiwa ni dakika ya tano na baadaye wao kusawazisha, kabla ya Kenya kuongoza na pili na Wazanzibari kusawazisha tena.

BINGWA tunapenda kuwapongeza wachezaji na benchi la ufundi la Zanzibar Heroes kwa mafanikio yao ya kufika fainali, licha ya kufungwa na kushindwa kuchukua ubingwa.

 

Tunaamini kwamba haikuwa kazi rahisi kwa Zanzibar Heroes kutinga hatua hiyo, ndio maana tumekuwa wa kwanza kuwapongeza.

 

Kama kila mmoja wetu alivyoshuhudia timu hiyo ilifanya kazi kubwa kwa kuzifunga timu zilizokuwa zikipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kama Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ na Rwanda, lakini pia ikiitoa jasho Libya.

Kwa kiasi fulani, mafanikio ya Zanzibar kwenye michuano hiyo hadi kufika fainali yalitokana na juhudi, maarifa pamoja na uzalendo wa hali ya juu wa wachezaji wa timu hiyo.

BINGWA tunaamini kwamba Zanzibar Heroes wanaweza kufanya vizuri zaidi michuano ya mwakani, iwapo wachezaji wa timu hiyo wataendelea kutunza viwango vya soka.

Tunasema kwamba mafanikio ya timu hiyo si tu ya Wazanzibari, bali pia Watanzania wote bila kujali upande mmoja wa nchi ya Jamhuri ya Muungano.

Hongereni Zanzibar Heroes kwa kiwango mlichoonyesha katika michuano ya mwaka huu ya Chalenji ingawa ubingwa umebaki kwa wenyeji Kenya.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU