MC PILIPILI: MVUNJA MBAVU ANAYEZIDI KUPAISHWA KIMATAIFA

MC PILIPILI: MVUNJA MBAVU ANAYEZIDI KUPAISHWA KIMATAIFA

429
0
KUSHIRIKI

*Churchill, Trevo Noah nao wampigia saluti

NA JESSCA NANGAWE


UNAPOTAJA jina la Emmanuel Mathias maarufu kama Mc Pilipili, hapo unamzungumzia mchekeshaji mahiri wa hapa nchini anayefanya vizuri mno akitikisa hadi nje ya mipaka ya Tanzania.

Umahiri Mc Pilipili katika sanaa yake umemfanya kupata mialiko mbalimbali ndani na nje ya nchi, ambayo imemsaidia kuzidi kujitangaza zaidi huku akijiwekea mikakati mipya ya kuanza mwaka mpya akijikita kimataifa zaidi.

Moja ya mialiko mikubwa aliyokutana nayo kwa mwaka huu, ni ziara yake ya nchini Marekani pamoja na leo kutumbuiza katika kipindi cha Churchill kinachofanyika Nairobi, nchini Kenya akiwa Mtanzania pekee aliyepata mwaliko huo.

BINGWA lilipata nafasi ya kufanya mahojiano na mchekeshaji huyo ikiwa ni muda mchache kabla ya kupaa kuelekea Nairobi, ambapo amezungumzia machache kuhusiana na safari yake hiyo pamoja na mipango yake katika kukuza zaidi kipaji chake hicho kwa siku zijazo.

ALIVYOPATA NAFASI

Mc Pilipili anasema umaarufu wake katika uigizaji wa stand up Comedy ulitokana na ubunifu pamoja na jitihada zake katika kuhakikisha anatimiza ndoto zake katika kufikia malengo yake.

Anasema alipata mwaliko huo kutoka kwa Daniel Ndambuki maarufu kama ‘Churchill’, mmoja wa waanzilishi wakubwa nchini Kenya ambaye moja kwa moja akimtaka kuhudhuria kutokana na kipaji chake katika vipindi mbalimbali anavyofanya.

“Tangu nimeanza standup Comedy Wakenya wananifuatilia sana na hata nchi mbalimbali wamekuwa wakinipigia simu na kunipongeza kwa kazi nzuri ninayoifanya, nashukuru sana Churchill ameona uwezo wangu na kunichagua kuweza kushiriki kwenye tamasha kubwa kama hili,”     anasema Mc Pilipili.

Anaongeza: “Nimefurahi kuona nakubalika na watu wakubwa kama hawa, nitakutana na wasanii wakubwa kama Basketmouth na wengine, ukweli najiona ni mtu mwenye bahati kubwa sana.”

Kuhusu kulipwa, Mc Pilipili anasema baada ya kuitwa alitajiwa kiasi cha fedha atakacholipwa, lakini hakuridhika nacho na kuwatajia kiasi anachotaka yeye ambapo waliridhia kitu kilichozidi kumpa kujiamini zaidi kupitia kazi zake.

Anasema baada ya kushiriki shoo hiyo ambayo ilishirikisha mastaa wakubwa Afrika, ameweza kupata uzoefu zaidi na kuona bado ana safari ndefu ya kuhakikisha sanaa yake inazidi kuokuwa kitaifa na kimataifa.

“Nimekutana na mastaa kama kina Churchill, Basketmouth, Eric Mond na wengine wamenifunza mambo mengi na kunishauri nahitaji kujituma sana na kuwa mbunifu ili niweze kufanikiwa zaidi kimataifa.

“Churchill kanipa moyo sana, kasema anakubali sana kile ninachokifanya lakini kanipa angalizo la kutakiwa nisibweteke na mafanikio ninayoyapata kwa sasa kwa kuwa     bado ni kijana mdogo na nina safari ndefu ya mafanikio,” anasema.

TUZO ZA NIGERIA

Mc Pilipili amekuwa msanii pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kuchaguliwa kushiriki kwenye tuzo hizo zilizofanyika nchini Nigeria, Desemba 13 na kusisitiza kuteuliwa kwake kuwania tuzo hizo, ni ishara kuwa kazi yake inaonekana na kukubalika.

“Kwangu bila kuangalia kama nitashinda tuzo, kuchaguliwa tu kuwania ni ishara kuwa ninafanya kazi nzuri na zinaonekana na kukubalika,” anasema Mc Pilipili.

Alisema kuwa anawaomba Watanzania na wananchi wa Afrika Mashariki kumpigia kura kwa wingi kuweza kushinda tuzo hiyo na kuitangaza Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki, kuna wasanii wengi wa vichekesho, lakini MC Pilipili amekuwa na bahati ya kuwa msanii pekee kuwania tuzo hizo.

Tuzo hiyo inawaniwa na wasanii wengine kumi na moja kutoka katika nchi za Nigeria na Ghana, ambapo mshindi wake atatangazwa na kukabidhiwa tuzo kwenye hafla itakayofanyika mapema mwakani.

MIKAKATI YAKE YA 2018

Pilipili anasema moja ya mikakati yake katika mwaka unaokuja ni kujitangaza kimataifa zaidi na kuhakikisha anaitangaza vyema nchi yake.

“Nimeshaanza kuwa wa kimataifa kwa sababu napata mialiko mingi sana ya nje ya nchi, nimeitwa Marekani na kulipwa pesa (fedha) ninayoitaka mimi, nimealikwa Kenya kwa fedha ninayoitaka mimi, hapa tayari ninaitwa wa kimataifa, ninachotaka mwaka unaoanza nizidishe kufanya kazi zaidi za kimataifa,” anasema Mc Pilipili.

ANAVYOMKUBALI ASLAY

Wasanii wa muziki wa Bongo wanafanya vizuri lakini namkubali sana Dogo Aslay, ni mtoto mdogo lakini amefanya mambo makubwa sana katika umri wake mdogo.

“Pamoja na kundi la Yamoto Band kufa lakini tumeona Aslay alivyorudisha heshima na kuufanya muziki wa Bongo uzidi kupaa, anaimba vitu real sana, anajua kucheza na watu maskini, matajiri na hata wenye matatizo ya mapenzi,” anasema.

Katika kuonyesha mahaba yake kwa Aslay, Mc Pilipili ameamua kuufanyia wimbo wa ‘Natamba’ ‘comedy’ ya peke yake kutokana na ujumbe uliomo ndani ya wimbo huo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU