MASHABIKI MAN CITY MMEMSIKIA ROONEY?

MASHABIKI MAN CITY MMEMSIKIA ROONEY?

1074
0
KUSHIRIKI

MERSEYSIDE, England


KAMA mashabiki wa Manchester City wameshaanza kuandaa sherehe za ubingwa, basi fowadi wa Everton, Wayne Rooney, amewaambia watafute kazi nyingine ya kufanya.

Kwa mujibu wa mpachikaji mabao huyo wa zamani wa Manchester United, kocha Pep Guardiola na vijana wake wa Man City wana safari ndefu kuufikia ubingwa.

Si ubingwa tu, Rooney anaamini bado ni mapema mno kuitaja Man City kuwa moja kati ya timu bora katika historia ya Ligi Kuu England.

Nyota huyo anajua wazi kuwa Man City wameshinda mechi 16 mfululizo, ukiwamo wa kichapo kizito cha mabao 4-1 walichoipa Tottenham wikiendi iliyopita.

Rooney ndiye aliyeifungia Everton katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Man City, mchezo pekee ambao vijana hao wa Guardiola walishindwa kuzoa pointi tatu.

“Sina uhakika kama wameshafanikiwa. Wanatakiwa waende hivyo hivyo,” alisema Rooney akizungumza  na kituo cha televisheni cha talkSPORT.

“Kwa miaka mingi zimekuwa zikitokea timu kubwa hapa Ligi Kuu England. Ili Man City nayo iwemo inatakiwa kushinda mataji mengi kwa miaka mingi.

“Sidhani kama watachukua ubingwa bila kufungwa. Wamefanya vizuri lakini Ligi Kuu ni ngumu, hasa kipindi hiki kuelekea Sikukuu ya Krismasi.

“Najua walivyo na kikosi kipana, kikosi cha wachezaji bora. Lakini kuna timu kubwa nyingi.

“Miaka miwili iliyopita, kulikuwa na timu mbili ambazo zilionekana zingeshinda kila mechi, lakini sasa kuna tano au sita ambazo zinaweza kufanya hivyo,” alisema Rooney.

Aidha, nyota huyo alipoulizwa ni timu gani anayoiona bora kuwahi kutokea Ligi Kuu England, aliitaja Man United aliyowahi kuichezea.

Kwa upande wao, wachambuzi wa soka wanaamini Man City imeonekana kuwa ya moto zaidi kutokana na ubora walionao Kevin De Bruyne, Leroy Sane, Raheem Sterling na David Silva, lakini Rooney ameonesha kumkubali zaidi kiungo Fernandinho.

Fernandinho raia wa Brazili, alijiunga na Man City mwaka 2013 akitokea Shakhtar Donetsk na klabu hiyo ya Ukraine haikuwa tayari kumwachia hadi ilipopewa  kitita cha Pauni milioni 34.

“Fernandinho ndiye anayewafanya wachezaji wengine wacheze. Bila yeye, Silva na De Bruyne wataanza kuhofia watakapopoteza mpira. Fernandinho anawabeba zaidi,” alisema.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU