NOMA KWELI: WACHEZAJI HAWA WANACHUKIWA NA MASHABIKI WAO

NOMA KWELI: WACHEZAJI HAWA WANACHUKIWA NA MASHABIKI WAO

980
0
KUSHIRIKI

LONDON, England


MASHABIKI wa soka hawatabiriki hata kidogo hasa wa England ambao wanafahamika kwa ‘uwendawazimu’ wao kwa mchezo huo.

Si tu wamekuwa na utamaduni wa kuzichukia timu pinzani, bali hata wachezaji, makocha na hata viongozi wao.

Mara nyingi hiyo imekuwa ikitokea pale wanapohisi mmoja kati ya hao hatekelezi majukumu yake ipasavyo.

Hebu cheki wanasoka wa Ligi Kuu England (EPL), waliojikuta wakiwa maadui wakubwa wa mashabiki wa timu zao.

Dejan Lovren (Liverpool)

Ni miongoni mwa wachezaji watatu wa Southampton waliosajili na Liverpool mwaka 2014. Liver walitoa Pauni milioni 20 na kumfanya kuwa beki ghali zaidi katika historia ya timu hiyo.

Kinachowafanya mashabiki wa Anfield wamchukie ni makosa yake ya mara kwa mara. Wengi waliumizwa na uzembe wake ulioipa Spurs mabao mawili katika mchezo uliochezwa Oktoba mwaka huu kwenye Uwanja wa Wembley.

 

Baadaye iliripotiwa kuwa mashabiki wametuma ujumbe wa vitisho kwa familia yake ingawa uongozi wa Liver nao uliwajibu kwa hasira ukiwaambia wamwache.

Takwimu zinaonesha kuwa ndiye mchezaji anayechukiwa zaidi na mashabiki wa timu yake katika mikikimikiki ya Ligi Kuu England.

Moussa Sissoko (Tottenham Hotspur)

Wakati wa usajili wa majira ya kiangazi ya mwaka jana, kulikuwa na vita kali kati ya Everton na Tottenham zilizokuwa zikimwania staa huyo aliyekuwa anatokea Newcastle.

Akiwa na timu hiyo, Sissoko alikuwa  beki tegemeo kikosini na hata Spurs walipomchukua, mashabiki wa timu hiyo hawakushangaa kuiona timu yao ikitoa Pauni milioni 30 kumsajili.

Lakini si walivyotarajia kwani nyota huyo ameshindwa kufua dafu mbele ya viungo Christian Eriksen, Eric Dier, Dele Alli na Moussa Dembele.

Nyota huyo sasa ni adui wa mashabiki wa Spurs ambao wanaamini kuwa hastahili kuwa klabuni hapo na hata kocha Mauricio Pochettino ameshamwambia kuwa anataka kuonesha kuwa anastahili kuwa kikosini.

Andros Townsend (Crystal Palace)

Winga huyo wa timu ya Taifa ya England alijiunga na Palace mwaka jana akitokea Newcastle United.

Tangu alipojiunga na timu hiyo, Towsend amekuwa adui wa mashabiki wake hasa kutokana na kiwango chake kupanda na kushuka.

Mijadala mingi ya mashabiki wa Palace imekuwa ikimpiga vita nyota huyo. Wengi wanaamini kuwa Townsend ni mchezaji mbinafsi anavyokuwa na mpira.

Kuonesha walivyomchoka klabuni hapo, mashabiki wengi walishangilia zilipoibuka taarifa kuwa nyota huyo ataondoka ifikapo Januari.

Kinachomponza zaidi ni takwimu zake za msimu uliopita ambapo alifunga mabao matatu pekee katika mechi 36.

Francis Coquelin (Arsenal)

Wakati anarejea Arsenal mwaka 2014 akitokea Charton Athletic alikokuwa kwa mkopo, mashabiki wa Gunners walifurahi wakiamini wamepata suluhisho la ubovu wa safu yao ya kiungo.

Akang’ara baada ya kupata nafasi kutokana na wimbi la majeruhi lililokuwa limeikumba Arsenal. Mashabiki wa Gunners wakakoshwa na kiwango chake katika mchezo dhidi ya Man City ambapo aliwawezesha kushangilia ushindi wa mabao 2-0.

Mfaransa huyo akaanza kuwakera mashabiki wa timu hiyo kutokana na ubovu wa pasi zake. Akawa anapotea kirahisi katika mechi kubwa za Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu.

Coquelin aliwavuruga zaidi mashabiki wake kwa kiwango kibovu alichokionesha katika mchezo dhidi ya Chelsea uliochezwa Februari mwaka huu katika Uwanja wa Stamford Bridge.

Si tu alicheza vibaya, pia alikuwa chanzo cha Eden Hazard kufunga bao pekee katika mchezo huo.

Hivi sasa nyota huyo amekuwa akitumika zaidi katika michezo ya Ligi ya Europa, ambako kocha Arsene Wenger amekuwa akitumia kikosi chepesi.

Katika mchezo wa mwezi uliopita dhidi ya Red Star Belgrade, ambapo timu hizo hazikufungana, mashabiki waliofika kwenye Uwanja wa Emirates walimzomea Coquelin.

Gary Cahill (Chelsea)

Huyo ni beki wa kati wa Chelsea. Cahil ana umri wa miaka 31 na nyota huyo aliyetua Stamford Bridge ndiye nahodha wa kikosi hicho kwa sasa.

Hata hivyo, hivi sasa mambo si mazuri kwa upande wake ni miongoni mwa wachezaji wasiokubali mbele ya mashabiki wa Blues.

Katika siku za hivi karibuni, mlinzi huyo amekuwa akifanya makosa mengi yanayowafanya mashabiki wasimwamini kila wanapomuona uwanjani.

Wengi wanatamani kuona nyota huyo akivuliwa unahodha na hata kuondoka kwenye ‘ukuta’ wao.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU