SIMBA, KWASI KUNA MTU KAIBIWA

SIMBA, KWASI KUNA MTU KAIBIWA

2628
0
KUSHIRIKI
  • Bingwa lashuhudia mkataba wake na Lipuli, labaini madudu matupu
  • Mkuu wa Mkoa Iringa atishia kuwafunga waliocheza rafu

NA WAANDISHI WETU


 

MAPYA yameibuka juu ya sakata la usajili wa Asante Kwasi ambapo kwa hali ilivyo, kati ya mchezaji huyo, Simba na klabu ya Lipuli, kuna mmoja atakuwa ameliwa.

Baada ya sakata hilo kushika kasi tangu zilipoonekana picha za Mghana huyo akisaini mkataba wa Simba, Bingwa liliufungia kazi mkataba wake na Lipuli ambapo jana lilifanikiwa kuuona.

Kwa mujibu wa mkataba huo, hakuna kipengele kinachoonyesha Kwasi alikuwa huru kuzungumza na timu yoyote inayomtaka badala yake klabu iliyohitaji huduma ya beki huyo, ilipaswa kuwasiliana kwanza na Lipuli wanaommiliki.

Lakini pia, mkataba huo unaonyesha kuwa Kwasi amebakiza miezi saba ndani ya Lipuli, hivyo hakuna klabu yoyote iliyokuwa na haki ya kufanya naye mazungumzo bila kuwasiliana na klabu yake hiyo.

Hivyo kwa kuwa sheria na kanuni za usajili zinaelekeza klabu inaweza kufanya mazungumzo na mchezaji moja kwa moja pale tu atakapokuwa amebakiza miezi sita au chini ya hapo katika mkataba na klabu yake, Simba kama kweli wamemsaini Kwasi, watakuwa wamekosea.

Kwa maana hiyo, kwa mujibu wa mkataba baina ya Lipuli na Kwasi kama ulivyoshuhudiwa na Bingwa jana, Simba walipaswa kuzungumza na klabu yake hiyo kwanza badala ya kuwasiliana na mchezaji husika, hivyo iwapo sheria zitafuata mkondo wake, Wekundu wa Msimbazi hao watakuwa matatani.

Lakini pia, iwapo Lipuli itaweka ngumu na kukataa kumalizana na Simba ‘nje ya mahakama’, Kwasi anaweza kujikuta matatani ndani ya klabu yake kwa shutuma za utoro kazini.

Hata hivyo, Bingwa limebaini kuwa kuna mkataba unaomwonyesha Kwasi kama mchezaji wa Gordogordo ya Nigeria na kwamba klabu hiyo ilimtoa kwa mkopo kwenda Lipuli baada ya awali kufanya hivyo kwa Mbao FC.

Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Lipuli, Ramadhan Mahano, alisema: “Sisi tunavyofahamu Kwasi ni mchezaji wetu, amebakiza miezi saba katika mkataba wake, aliondoka klabuni kwenda kwao kwa ajili ya msiba wa baba yake, tukampa nauli ya kwenda na kurudi, tumeshangaa kusikia yupo Dar es Salaam, tena amesajiliwa na Simba.

“Simba wameonyesha si waungwana kwa kuzungumza na mchezaji bila ridhaa yetu, tumeamua kuwaacha tutakutana nao kwenye Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi ya Wachezaji kipindi cha pingamizi na ikitokea wakija, wajiandae kutupa fedha zaidi ya walizompa Kwasi.

“Tofauti na hapo, mchezaji huyo hataweza kucheza kwa sababu sisi tuliwaomba watupe Jamal Mnyate na Juma Luizio kupitia Hans Poppe (Zacharia- Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Simba), wakatuambia tubadilishane na Kwasi, tukakataa, suala hilo likaishia hapo.

“Ndio maana Mnyate alipokuja kwetu kwa mkopo wa miezi sita, tulikubali masharti yao ya mchezaji huyo kutocheza mechi yoyote tutakayocheza na Simba pamoja na kumpa mshahara walioutaka Simba.”

Alisema walishangaa Simba kuzungumza na Kwasi bila kuwashirikisha wao jambo walilolikataa awali.

Alipoulizwa juu ya klabu ya Gordogordo kuwapa Kwasi kwa mkopo, alisema: “Wakati tunamsajili tulikuwa tunajua ni mchezaji huru, baadaye tukabaini ana mkataba wa mwaka mmoja na hiyo klabu…tukaamua kwenda kuzungumza nao wakakubali kutuachia kwa mkataba waliomsajili wao lakini wakatutaka tumpe dau la usajili pamoja na mshahara aliokubaliana nao (Gordogord).

“Tulikubaliana iwapo kuna timu itakayomhitaji (Kwasi), tuwasiliane nao kwanza…Tunashangaa Simba wamepata wapi haki ya kumsajili mchezaji bila hizi timu mbili kuhusishwa, hasa sisi tunaommiliki kihalali kwa sasa.”

Mmoja wa vigogo wa moja ya kamati za TFF, alikiri Kwasi kubakiza miezi saba katika mkataba wake na Lipuli hivyo kama Simba wamemsainisha, wamefanya makosa na kamati yao ikikaa na kulisimamia suala hilo, mchezaji huyo anaweza kusimamishwa huku Wekundu wa Msimbazi wakipigwa faini kama ilivyokuwa kwa Yanga dhidi ya Ramadhan Kessy.

“Suala la Kwasi na Simba bado lina utata, ila kama Simba wamemsainisha  mchezaji huyo itawafikisha pabaya pande zote mbili, mchezaji na klabu kwa sababu bado ana mkataba wa miezi saba na Lipuli.

“Endapo kanuni zitafuatwa Simba itapigwa faini na mchezaji atasimamishwa, mfano wa kesi hii ni kama ile ya mchezaji Hassan Kessy na Yanga ambao walilazimika kulipa milioni 50,” alisema.

Alisema njia salama ya kumaliza suala hilo, labda Simba wakae na Lipuli wazungumze japo wanasubiri kwa sababu hadi sasa hawana uhakika kama Simba wamemsainisha mkataba Kwasi kwa kuwa kuna majina yao yaliyogoma kuingia kwenye mtandao wa usajili (TMS).

Kwa upande wake, mmoja wa maofisa wa TFF, alisema kuna uwezekano wa Kwasi kuichezea Simba kwani Hanspope ndiye aliyempeleka Lipuli baada ya viongozi wake kumkataa alipopendekeza asajiliwe Msimbazi.

“Kinachoonekana, Lipuli walimrithi Kwasi kutoka Mbao FC alikokuwa akicheza kwa mkopo, hivyo nao kisheria hawatambuliki zaidi ya klabu yake mama, yaani Gordogordo ya Nigeria…sitashangaa iwapo ataidhinishwa kuichezea Simba,” alisema.

Katika hatua nyingine, imedaiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza ambaye ni mlenzi wa Lipuli, ametishia kuwatupa lupango viongozi wa timu hiyo iwapo atabaini kujihusisha na sakata la usajili wa Kwasi kwenda Simba.

Imeelezwa kuwa leo uongozi wa Lipuli unakutana na kiongozi huyo ili kujadili suala hilo na kulipatia ufumbuzi.

Juu ya sakata hilo, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema litapatiwa ufumbuzi katika kikao cha Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji kitakachofanyika Desemba 30, mwaka huu.

“Kikao cha Kamati kinatarajia kufanyika tarehe 30 mwezi huu kujadili kesi zote zinazohusu wachezaji, ikiwamo hiyo ya Asante Kwasi,” alisema Lucas.

Habari hii imeandaliwa na ZAINAB IDDY, WINFRIDA MTOI na SALMA MPELI.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU