WADAU OKOENI JAHAZI FAINALI MISS TANZANIA 2017

WADAU OKOENI JAHAZI FAINALI MISS TANZANIA 2017

419
0
KUSHIRIKI

NA ESTHER GEORGE


FAINALI za Miss Tanzania 2017 zilipangwa kufanyika Novemba mwaka huu, lakini hadi sasa hazijafanyika kutokana na ukata unayoikabili kampuni ya Lino International Agency ambao ni waandaaji wa mashindano hayo.

Hali hiyo imefanya mashindano hayo kushindwa kufanyika kwa wakati na muda sahihi uliopangwa hivyo kuwaweka njiapanda wadau wakibaki katika hali ya sintofahamu.

Japo shindano hilo ni muhimu katika jamii, hasa wasichana wenye ndoto za kufika mbali kupitia fani hiyo, lakini inaonekana wazi hakuna dalili za fainali zake kufanyika mwaka huu.

Hilo linatokana na ukweli kuwa hadi sasa waandaaji hawajatambulisha siku ya kuanza kambi ya taifa, lakini pia baadhi ya vitongoji na kanda zikiwa hazijasaka warembo wao.

Ni vema ikafahamika kuwa mashindano ya urembo yanastahili kupewa kipaumbele kama ilivyo kwa soka, muziki na shughuli nyinginezo za kimichezo na burudani.

Ushahidi unaonyesha kuwa wapo wasichana ambao wamefanikiwa kubadilisha maisha yao kupitia mashindano hayo kwa sasa wakiwa ni watu maarufu na wenye maisha ya juu tofauti na walivyokuwa awali.

Baadhi ya warembo hao kwa hapa nchini, wapo Wema Sepetu ambaye ni Miss Tanzania 2006, kwa sasa akiwa ni supastaa anayetamba katika soko la filamu na mjasiriamali maarufu.

Lakini pia, yupo Jokate Mwegelo, Miss Tanzania namba mbili 2006, ambaye kwa sasa anatamba katika filamu na muziki, lakini pia akiwa ni mjasiriamali na mwanaharakati.

Mwingine ni Richa Adhia, Miss Tanzania 2007 ambaye kwa sasa ni mjasiriamali maarufu hapa nchini akijihusisha na biashara na huduma za urembo wa ngozi na nyinginezo.

Katika orodha hiyo, huwezi kumweka kando Nancy Sumari, ambaye alikuwa ni Miss Tanzania 2005 ambaye alifanikiwa kutwaa taji la Miss World Africa, yaani Mrembo wa Dunia wa Afrika mwaka huo.

Kwa sasa Nancy anafanya vizuri mno katika ujasiriamali kiasi cha kutwaa tuzo lukuki.

Kimsingi, wapo wasichana wengi mno ambao wapo mbali kimaisha baada ya kujinadi kupitia mashindano ya Miss Tanzania.

Lakini ukiachana na mafanikio ya mtu mmoja mmoja, mashindano ya Miss Tanzania, yamesaidia kutoa ajira kwa wengi, kuanzia wanaofanya huduma za usafiri, hoteli, utalii, mavazi, vipodozi, ulinzi, mapambo na wengineo wengi.

Pia, kupitia mashindano hayo, Tanzania imeweza kujitangaza kimataifa kupitia ushiriki wa mrembo wake kwenye mashindano ya dunia, yaani Miss World.

Katika mashindano hayo, miaka yote mwakilishi hutambulika kwa jina la nchi yake hali inayosaidia kuitangaza nchi husika pamoja na vivutio vyake vyote vya kiutalii.

Lakini pamoja na yote hayo, mwaka huu inaonekana wazi fainali za Miss Tanzania huenda zikaota mbawa kwani hata katika ngazi ya vitongoji, wilaya, mikoa na kanda, kuna mengine hayakufanyika kutokana na kukosa wadhamini japokuwa warembo wengi walijitokeza na kutamani kushiriki.

Kwa maeneo yalikofanyika mashindano hayo, hadi sasa warembo waliokata tiketi ya kushiriki fainali za Miss Tanzania hawafahamu hatima yao.

Ifahamike kuwa kutofanyika kwa mashindano haya, ni sawa na kukatiza ndoto za wasichana wengi wa Kitanzania na si kumkomoa Hashim Lundenga na kamati yake chini ya Lino International Agency.

Hivyo, ni vema wadau kujitokeza kuona ni vipi wanaweza kuokoa jahazi ili shindano hilo lifanyike mwaka huu au mapema mwezi ujao.

Kwa kuwa Serikali ina mkono mrefu na kwamba haishindwi na jambo lolote, basi iangalie ni vipi inaweza kuokoa jahazi kwa kushawishi kampuni, mashiriki na taasisi mbalimbali kudhamini mashindano hayo.

Kwa kufanya hivyo, Serikali itakuwa imewasaidia wasichana wa Tanzania wenye ndoto ya kufanya vema kupitia mashindano hayo kufanikisha ndoto zao kwa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.

Mungu ibariki Miss Tanzania

Mungu ibariki Tanzania

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU