HII NI NAFASI YA MWISHO KWA MAVUGO SIMBA

HII NI NAFASI YA MWISHO KWA MAVUGO SIMBA

1291
0
KUSHIRIKI

NA EZEKIEL TENDWA

SARAKASI za usajili wa dirisha dogo la Ligi Kuu Tanzania Bara zimemalizika, lakini kati ya wachezaji ambao walikuwa kwenye presha kubwa ni mshambuliaji wa Simba, Mrundi Laudit Mavugo aliyekuwa akitajwa kutemwa.

Ukweli ni kwamba, Mavugo aliponea kwenye tundu la sindano baada ya kuwepo kwa  taarifa kwamba Simba  waliiruhusu klabu ya AFC Leopards ya Kenya ili wafanye mazungumzo naye na kama ingependeza wangemsajili.

Lakini kilichoshindikana kutuma AFC Leopards ni baada ya Mrundi huyo kushikilia msimamo wake kwamba yeye ni mali ya Simba.

Nilipitia mtandao maarufu wa michezo nchini Kenya wa Futaa.com, nikaona habari iliyomhusu Mavugo ikiwanukuu viongozi wa AFC Leopard wakisema, wangemalizana na Mrundi huyo muda wowote baada ya kukubaliwa na Simba.

Simba walionekana kama hawakuwa na mpango wa kuendelea kumtumia Mavugo Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano mingine.

Ni wazi kwamba Mavugo ni kama amechokwa pale Simba na kinachomfanya kuendelea kuwapo ni kutokana na mkataba wake, lakini vinginevyo leo hii tungesikia Mrundi huyo amesajiliwa na timu nyingine.

Kinachowafanya Simba kutomhitaji tena Mavugo ni kutokana na ukweli kwamba, kile kiwango alichokuwa akikionyesha nchini Burundi katika Klabu ya Vital’O, akifunga mabao mengi kama alivyokuwa akitaka, hajakionyesha kwa Wekundu wa Msimbazi hao.

Amepewa nafasi mara kwa mara lakini haonyeshi utofauti wowote na wachezaji wazawa na badala yake amekuwa sasa akisugua benchi kitu ambacho kiliwafanya Simba kufikiria kumtoa kwa mkopo kama si kumuuza jumla kabla ya dili hilo kufeli dakika za mwisho na kuwa ahueni kwake.

Binafsi naona hii ni nafasi ya mwisho kwa Mavugo kuonyesha ubora wake, vinginevyo msimu utakapomalizika anaweza akajikuta amesukumizwa nje kama ilivyokuwa kwa wenzake waliomtangulia akiwamo Mrundi mwenzake, Amis Tambwe, ambaye baadaye alijiunga Yanga.

Mavugo anatakiwa kujua kwamba Simba si wavumilivu na wanaweza wakachukua maamuzi ya kushangaza, kwani kama waliweza kumuacha Tambwe dakika za lala salama dirisha dogo, tena akiwa na kiwango kizuri kabla ya kudakwa na Yanga, je, yeye atapataje kupona na kiwango chake hicho cha sasa.

Bahati nzuri iliyopo ni kwamba Simba ina michezo mingi ambayo kama Mavugo akikaa sawa, anaweza kurudisha imani ya viongozi na mashabiki ambao baadhi yao wameshaonyesha kumchoka.

Simba ipo Ligi Kuu Tanzania Bara, itakwenda kushiriki michuano ya Mapinduzi Zanzibar na pia itaiwakilisha nchi michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Hiyo ni nafasi tosha kwa Mavugo kuonyesha uwezo wake na kuwafunga midomo wale wote waliokuwa wakimsema mabaya, vinginevyo hatakuwa  na     la kujitetea msimu utakapomalizika ikizingatiwa kuwa wenyewe wanataka kuifanya klabu yao kuwa ya kisasa zaidi.

Ninaamini kwamba Mavugo ni mmoja wa washambuliaji wazuri ila upepo haujamwendea  vizuri wakati huu,  lakini wasiwasi wangu ni kwamba kama upepo huo utazidi kumwendea kombo wenye timu yao hawatamvumilia kwani kama waliweza kumfukuza Joseph Omog baada ya kufungwa na Green Warriors, yeye ni nani asitimuliwe? Ajitafakari upya.

Mavugo anatakiwa kukaza kuanzia mchezo wao wa ligi utakaochezwa wikiendi hii dhidi ya Ndanda FC na baadaye akauwashe moto michuano ya Kombe la Mapinduzi, atakuwa ameanza kurejesha heshima yake     kwani Simba na Yanga kukukubali ni dakika moja na kukuchukia ni dakika moja, hivyo ndivyo hizi timu zilivyo.

Nadhani  uwapo wa kocha Mrundi mwenzake Masoud Djuma,  anaweza kumtumia na anapotakiwa kushikilia na kuanza kuonyesha cheche zake vinginevyo safari itakuwa inamhusu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU