HONGERA TFF KWA KUPATA UDHAMINI HUU, LAKINI…

HONGERA TFF KWA KUPATA UDHAMINI HUU, LAKINI…

283
0
KUSHIRIKI

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limepata udhamini wa vifaa vya michezo wenye thamani ya takribani Sh bilioni 1.9 kutoka kwa Kampuni ya Macron ya nchini Italia, kwa ajili ya timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Tumeelezwa kwamba mkataba huo utakuwa wa kiasi cha Euro 300, 000 (sawa na shilingi milioni 791,749,000) kama fedha taslimu kwa muda wa miaka yote miwili.

Rais wa TFF, Wallace Karia, alitangaza udhamini walioupata jana katika mkutano wa wahariri wa habari za michezo ambaye alisema, kiasi kingine cha euro 400,000 (sawa na shilingi bilioni 1,055,670,000) kitakuwa maalumu kwa vifaa vya timu zote za Taifa ikiwamo za wanawake na vijana.

Katika mkutano huo alizungumzia jinsi alivyotumia miezi yake minne ya mwanzo kutekeleza sera zake kwa asilimia 75 tangu alipochaguliwa Agosti 12, mwaka huu mjini Dodoma.

Kwa upande wetu sisi BINGWA, tuna kila sababu ya kuupongeza uongozi wa Karia kwa mafanikio aliyopata katika siku 120 ambazo amekuwa madarakani, hasa hilo la timu za taifa kupata udhamini huo.

Tunafahamu kwamba kuendesha timu za taifa ni mzigo mkubwa kama hapakuwa na wadhamini ambao wataweza kupunguza baadhi ya changamoto.

BINGWA tunaona ni hatua nzuri ambayo Karia na wenzake wamefikia, lakini tunahitaji kuona udhamini kama huo unapatikana na klabu zinashiriki Ligi Daraja la Kwanza, Daraja la Pili, tukiamini kwamba ndilo chimbuko la wachezaji wengi.

Tunasema kuwepo kwa udhamini kwa timu za taifa pekee na kuacha klabu za daraja mbalimbali hakutasaidia kuboresha ligi zetu ambazo ndizo zinamwezesha kocha wa taifa kuangalia wachezaji.

Tumeshuhudia baadhi ya klabu zinashindwa kushiriki ligi kutokana na kukosa udhamini na sasa TFF wanatakiwa kuangalia kwa kina jinsi ya kuisaidia ili baadaye tuwe na mafanikio katika soka.

Ni imani yetu kwamba TFF wataendelea kusaka wadhamini zaidi  kwa klabu zinazoshiriki ligi mbalimbali ili iwe katika kiwango cha juu cha ushindani wa soka.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU