GEORGE WEAH KUTOKA UFUNDI SIMU, KUNYAKUA BALLON D’OR HADI KUWANIA...

GEORGE WEAH KUTOKA UFUNDI SIMU, KUNYAKUA BALLON D’OR HADI KUWANIA URAIS

503
0
KUSHIRIKI

MONROVIA, Liberia

WENGI watakuwa wakimfahamu nyota wa zamani, George Weah, kutokana na umahiri wake aliouonesha wakati akisakata kandanda.

Hata hivyo, si wote watakuwa wakifahamu historia yake ya nyuma kabla ya kufikia kuwa mwanasoka bora wa dunia na hatimaye kujitosa katika masuala ya siasa na hadi akagombea urais.

Kutokana na hali hiyo, BINGWA kwa msaada wa mitandao limejaribu kuangalia njia ambazo nyota huyo alipitia mpaka sasa.

*Maisha ya utotoni

 

Weah alizaliwa Oktoba mosi, 1966 katika Jiji la Monrovia. Weah anatoka  katika kabila la Kru ambalo linatoka upande wa Kusini-Mashariki mwa Liberia kwenye Kaunti ya Grand Kru, ambayo ni moja ya maeneo masikini sana nchini humo.

Wazazi wake walikuwa ni William T. Weah, Sr na Anna Quayeweah.

Alilelewa zaidi na bibi yake upande wa baba, Emma Klonjlaleh Brown. Alihudhuria shule ya msingi katika shule ya Muslim Congress na sekondari katika Shule ya Wells Hairston High School.

 

*Safari yake katika soka

Kabla ya kujiunga na soka la kulipwa, Weah alikuwa akifanya kazi katika Shirika la Mawasiliano la Liberia kama fundi simu.

Weah alianza safari yake ya soka katika timu ya Liberia ya Incincible Eleven na Tonnerre Yaounde ya Cameroon. Baada ya hapo mwaka 1988 alikwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya ambapo alijiunga na timu ya Monaco ambayo ilikuwa ikifundishwa na Arsene Wenger.

Akiwa na timu hiyo aliiwezesha  kushinda Kombe la Ufaransa mwaka 1991  kisha baadaye alijiunga na Paris Saint Germain mwaka 1992-95.

 

Aliiongoza timu hii kuchukua Kombe la Ligi ya Ufaransa mwaka 1994. Akiwa hapo aliweza kuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya (UEFA) mwaka 1994–95.

Mwaka 1995-2000 alikuwa akiichezea timu ya AC Milan ambayo ilishinda ligi ya Italia mwaka 1996 na 1999. Mwaka 2000 aliondoka AC Milan na kujiunga na Chelsea, baada ya muda mfupi alijiunga na Manchester City na baadaye Marseille mwaka 2001.

 

Alimaliza soka la kulipwa akiwa na timu ya Al Jazira ya Falme ya Nchi za Kiarabu. Kwa ujumla alicheza soka la kulipwa kwa miaka 14.

Weah aliichezea pia timu ya taifa ya Liberia na aliiwakilisha nchi yake katika Kombe la Mataifa ya Afrika mara mbili.

Weah amekuwa akitoa misaada kusaidia wananchi wa Liberia. Mwaka 2004 alipewa Tuzo ya Ujasiri ya Arthur Ashe kwa juhudi zake za kusaidia kujenga nchi yake.

Tuzo alizozinyakua

 

Mwaka 1995, Weah alipewa tuzo na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kuwa Mwanasoka Bora Duniani. Yeye ni mwanasoka pekee toka Afrika aliyewahi kupewa tuzo hiyo. Mwaka huo huo alichaguliwa pia kuwa Mwanasoka Bora Ulaya na Mwanasoka Bora Afrika. Mwaka 1989, 1994 na 1995 alichaguliwa kuwa Mwanasoka Bora wa Mwaka Afrika na mwaka 1996 alichaguliwa kuwa Mwanasoka Bora wa Karne wa Afrika.

Mwaka 2004, Pele alimchagua kwenye orodha ya Fifa ya wachezaji bora ambao wako hai.

 

Safari yake kisiasa

Baada ya kumalizika vita ya pili ya wenyewe nchini Liberia, Weah alitangaza dhamira yake ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ambapo aliunda chama cha siasa alichokipa jina la Congress for Democratic Change.

 

Hata hivyo, Weah kutokana na kuwa mtu mwenye jina nchini Liberia wapinzani walimwekea vikwazo kikiwamo cha ukosefu wa elimu ya kutosha ili kuendesha nchi ikilinganishwa na aliyekuwa mpinzani wake, Ellen Johmso Surleaf, aliyekuwa na elimu ya Chuo Kikuu cha Harvard na huku wachambuzi wengine wakikifananisha kitendo cha kukosa uzoefu mkubwa ni sawa na kumuacha mtoto ndani ya msitu.

 

Wakati mpinzani wake, Sirleaf, aliwahi kuwa Waziri wa Fedha miaka 1970 wakati wa utawala wa Tolbert na pia alikuwa amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika benki za Citibank, Benki ya Dunia na Umoja wa Mataifa.

 

Nia ya Weah kugombea urais ilizidi kutiliwa zengwe jingine kuwa aliwahi kuomba uraia wa Ufaransa enzi zake za soka wakati akiwa na timu ya Paris St. Germain, ingawa halikutiliwa maanani, lakini mizengwe hiyo yote hatimaye akaruhusiwa kugombea.

 

Katika duru ya kwanza iliyofanyika Oktoba 11 mwaka huo, Weah aliweza kupata asilimia 28.3 ambayo ilimruhusu kuingia duru ya pili ya kushindana na Rais Sirleaf.

 

Hata hivyo, katika duru hiyo iliyofanyika Novemba akapata asilimia  40.6 dhidi ya 59.4 aliyopata  Sirleaf.

Pamoja na kushindwa katika uchaguzi huo, Weah aliendelea kujikita kwenye sera za siasa za  Liberia ambapo mwaka 2009 baada ya kurejea kutoka nchini Marekani, alizifanya kampeini kwa mafanikio makubwa akiwa na chama chake cha Congress for Democratic Change ambapo aligombea useneta katika Jimbo la  Montserrado  na akashinda.

Ushindi huo uliwafanya wachambuzi wengi kubashiri kama hiyo ilikuwa njia nyingine ya nyota huyo kujipanga kwa ajili ya kugombea tena nafasi hiyo ya urais katika uchaguzi wa 2011.

 

 

Katika uchaguzi wa maseneta wa Desemba 2014,  Weah alimshinda Robert Sirleaf, ambaye ni mtoto wa Rais Sirleaf na hivyo mwanamichezo wa kwanza kimataifa nchini humo kuliwakilisha jimbo katika baraza hilo.

 

Alipata kura  99,226  sawa na asilimia  78.0 kutoka vituo 141 wakati mpinzani wake Sirleaf, aliambulia kura 13,692  sawa na asilimia 11.

Aprili 2016, Weah alitangaza kugombea tena urais kwa mara ya pili na mwaka huu akatimiza azma yake ambapo alikuwa akikabiliana na Makamu wa Rais, Joseph Boakai.

Weah amemuoa Clar Weah, mwenye asili ya Visiwa vya Karibiani. Wana watoto watatu; George Weah Jr, Tita na Timothy. Baada ya majaribio na timu ya Chelsea mwaka 2013, alijiunga na timu ya Paris Saint-Germain mwaka 2015. Timothy anaichezea pia timu ya taifa ya Marekani ya chini ya umri wa miaka 18. Binamu yake Weah, Christopher Weah aliwahi pia kucheza soka la kulipwa kwenye timu ya Arsenal.

 

Weah aliwahi kubadili dini toka Ukristo kwenda Uislamu na baadaye akarudi tena kwenye Ukristo. Hivi sasa ni muumini wa Ukristo wa Uprotestanti.

Elimu

 

Kielimu, Weah ana Shahada ya Kwanza ya Uendeshaji Michezo toka Chuo Kikuu cha Parkwood, London, Uingereza. Hata hivyo, baadhi ya watu wanatilia shaka shahada hii kwa kuwa chuo hiki kinajulikana kwa kutoa shahada bila kusoma hapo, baadaye alipata shahada ya Usimamizi wa Biashara toka Chuo Kikuu cha DeVry, Miami nchini Marekani. Mwaka 1999 alipata shahada ya Udaktari ya Heshima toka Chuo Kikuu cha A.M.E Zion nchini Liberia.

na mwaka 2017.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU