NJOMBE MJI, STAND UNITED ZIPAMBANE KUBAKI LIGI KUU

NJOMBE MJI, STAND UNITED ZIPAMBANE KUBAKI LIGI KUU

233
0
KUSHIRIKI

NA MAREGES NYAMAKA

UHONDO wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara unatarajia kuendelea leo Azam watakapowakaribisha Stand United kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Ligi hiyo itaendelea kwa mzunguko wa 12, baada ya kusimama kwa takribani mwezi mmoja kupisha michuano ya Kombe la Chalenji lililofanyika nchini Kenya.

Katika michuano hiyo ya Chalenji timu za Taifa za Tanzania, Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes zilikwenda kushiriki  na wenyeji Kenya kuchukua ubingwa.

Azam ambao wanashika nafasi ya pili katika msimamo kutokana na pointi 23 sawa na Simba wanaoongoza kwa mabao ya kufunga, leo watawania kukaa kileleni watakapocheza na wapinzani wao Stand United.

Lakini kazi kubwa itakuwa kwa Njombe Mji ambao walianza vibaya ligi hiyo kwa kufungwa michezo mitatu mfululizo na klabu hiyo kufikia uamuzi wa kumtimua aliyekuwa kocha mkuu, Hassan Banyai.

Njombe Mji watacheza na Singida United keshokutwa kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe, mchezo ambao ni muhimu kwa kushinda ili kuweza kujiweka katika mazingira bora ya kutoshuka daraja.

Matokeo mabaya kwa Njombe Mji katika mchezo huo yatakuwa yamezidi  kuwaweka pabaya ambayo wanashika nafasi ya pili kutoka mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo.

Ili Njombe Mji waweze kujihakikishia kubaki katika msimu ujao wa ligi hiyo, wanatakiwa kuonyesha ushindani mkali wa soka baada ya kufanya usajili kipindi cha dirisha dogo.

Vinginevyo tunaweza kushuhudia Njombe Mji ikishiriki msimu mmoja wa ligi ambayo ilipanda kwa mara ya kwanza, baada ya kufanya vizuri Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara msimu uliopita.

Kutokana na hali ilivyo, kocha Mrage Kabange, ana kibarua kizito kuhakikisha Njombe Mji inabakia ligi kuu na ikizingatia ushindani wa soka unaonyesha ni mkubwa.

Pengine usajili wa wachezaji wapya uliofanywa na klabu hiyo unaweza kuwa na tija, lakini hata hivyo wachezaji wanatakiwa kuvuja jasho ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kuifanya timu hiyo kuondoka mkiani.

Hili linawezekana pia iwapo kama viongozi wa klabu ya Njombe Mji atakuwa wameondoa changamoto zilizosababisha timu kupepesuka katika michezo mitatu mfululizo na kupoteza pointi tisa.

Nafasi ya Njombe Mji kufanya vizuri kwenye ligi hiyo bado naiona bado ipo kwa kuwa mechi zilizobaki ni nyingi, hivyo viongozi wa klabu hiyo, wakiwa karibu na benchi la ufundi wachezaji wanaweza kuondoka nafasi wanayoshika kwa sasa.

Ukiondoa Njombe Mji wanaoonekana kusuasua kwenye ligi hiyo, timu kama Stand United ambayo leo jioni itacheza na Azam isiposhinda itakuwa imeendelea kujichimbia kaburi la kushuka daraja, licha ya kwamba ligi bado mbichi.

Kiwango cha Stand United kimekuwa si kizuri msimu huu, kwani hadi sasa wameshinda mchezo mmoja, wakitoka sare nne na kupoteza michezo sita.

Ni wazi kwamba Stand United wasipobadilika  kwa maana ya kupambana na kupata matokeo mazuri wanaweza kuwa timu ya kwanza kushuka daraja msimu huu, kwani hawajaonyesha kucheza kwa ushindani.

Viongozi wa Stand United wanatakiwa kujitwisha msalaba kuhakikisha wachezaji wanapata mahitaji yote ambayo yatawapa morali wa kucheza  soka ya ushindani, lakini tofauti na hivyo ushindi kwao utaendelea kusuasua na kuzidi kujiweka katika mazingira ya kushuka daraja.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU