KARIA TUMEKUSIKIA LAKINI…

KARIA TUMEKUSIKIA LAKINI…

262
0
KUSHIRIKI

NA CLARA ALPHONCE

JUMATANO wiki hii, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, alifanya mkutano na wahariri wa michezo wa vyombo mbali mbali vya habari nchini.

Mkutano huo ulikuwa wa kwanza tangu uongozi wake ulipoingia madarakani Agosti 12, mwaka huu, baada ya uchaguzi uliofanyika mjini Dodoma.

Katika mkutano huo, Karia alieleza mambo mazuri yaliyofanyika kwa kipindi cha miezi minne na mikakati mingine kwa miaka ijayo.

Moja ya mambo ya mafanikio yake katika kipindi kifupi ambacho yuko madarakani ni kupata udhamini wa jezi kwa timu za Taifa kutoka Kampuni ya Marcon ya Italia.

Pamoja na kupata udhamini huo, lakini  alizungumzia suala la mashindano ya ndondo ambayo yamekuwa yakiandaa kiholela hapa nchini bila kufuata kanuni.

Karia anaonekana hakueleweka alipozungumza kuhusu mashindano  kuwa yasiandaliwe bila kupata kibali kutoka kwa wanachama wa shirikisho ambao ni vyama vya mikoa na vyama vya wilaya.

Kauli ya Karia inaonekana imepokewa tofauti kutokana na wadau kutomwelewa alichokimaanisha katika mkutano wake na wahariri wa michezo.

Nilivyomwelewa Karia  ni kwamba,  watu watakaondaa mashindano ya ndondo ni lazima wapate kibali  kutoka vyama vya mikoa na wilaya  na kama yatakuwa ya kitaifa kibali cha kuandaa mashindano hayo kitoke TFF.

Lengo la kufanya hivyo ni kutaka kila kitu kiende kwa mpangilio mzuri, ambao utaweza kuboresha mashindano yenyewe ya ndondo na si mtu anaibuka na kuandaa mashindano yake huku mitaani bila FA kufahamu, huu unakuwa si utaratibu unafaaa katika kuendesha mpira.

Kauli hiyo ni nzuri na inatakiwa kuungwa mkono na wadau wa soka hapa nchini. Lakini tu kama itasimamiwa kwa umakini na kutoa haki kwa kila mmoja.

Ni kweli kuna watu wamekuwa wakiandaa mashindano ya ndondo bila kufuata taratibu na tatizo likitokea wanaokuwa wa kwanza kuwajibika ni TFF na viongozi wa wilaya na mikoa.

Sioni kama kuna tatizo kwa Karia kutaka utaratibu mpya wa kuandaa mashindano ya ndondo, kwani hata sheria za nchi haziruhusu kufanya mkusanyiko wa aina yoyote bila kibali kutoka kwa ngazi husika.

Tusichukulie urahisi katika soka, kwani linapofikia jambo limeharibika wa kwanza kuwajibika wanakuwa ni viongozi wa soka.

Kufuata utaratibu ni jambo jema na ni suala ambalo linafanyika katika kila sehemu hapa nchini, labda huku kwenye mpira watu wanaweza kuliona suala geni kwa kuwa lilikuwa halitiliwi mkazo tu.

Wasanii hasa wa muziki jambo hilo kwao si geni, wanajua hawawezi kuandaa tamasha lolote bila kupata kibali kwa wamiliki wa muziki ambao ni Baraza la Sanaa Tanzania (Basata).

Leo  hii TFF wakitaka kuandaa mashindano ya kimataifa lazima wapate kibali kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kuwa  kanuni zinasema hivyo.

Mashindano ya ndondo siku zote huwa tuna amini kuwa yanaibua vipaji na baadaye wanakuja kuwa wachezaji wakubwa katika timu kubwa hapa nchini, kama ni hivyo kwanini yasifuate taratibu na kuwa na kanuni ambazo zitafanya yazidi kuwa bora.

Angalizo ni kwenye kuandaa kanuni za mashindano hayo ni vema wakawashirikisha wadau ambao ni waandaaji wakubwa wa mashindano hayo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU