SIMBA, YANGA MSIPUUZE KOMBE LA MAPINDUZI

SIMBA, YANGA MSIPUUZE KOMBE LA MAPINDUZI

517
0
KUSHIRIKI

NA JESSCA NANGAWE

PAZIA la michuano ya Kombe la Mapinduzi lilifunguliwa rasmi jana visiwani Zanzibar, ambapo timu nane kutoka Tanzania Bara zitashiriki kuwania kombe hilo.

Michuano hiyo inaandaliwa maalumu kwa lengo la kudumisha sherehe za Mapinduzi ambazo hufanyika kila mwaka inapofikia Januari 12.

Timu za Zanzibar zinazoshiriki kombe hilo ni JKU, Jamhuri, Mlandege, Taifa Jang’ombe na Zimamoto ambapo zote zinashiriki Ligi Kuu ya Zanzibar

Kwa upande wa Tanzania Bara timu zitakazoshiriki mashindano hayo ni Singida United iliyopanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu huu, Simba, Yanga na Azam FC ambao ni mabingwa watetezi.

Timu ya URA kutoka nchini Uganda ambao walibeba taji la kombe hilo mwaka 2015, wamepata mwaliko kwa mara nyingine baada ya kuvuliwa ubingwa na Azam mwaka jana.

Singida United pia wanashiriki kwa mara ya kwanza baada ya kurejea Ligi Kuu Bara, lakini wanajaza nafasi ya Mtibwa Sugar ambayo haipo kwa mwaka huu.

Klabu za Simba na Yanga zinaweza kunufaika na mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwa kuwa ni sehemu ya mazoezi na maandalizi ya vikosi vyao ambavyo vitashiriki michuano ya  kimataifa mwakani.

Yanga ambao ni mabingwa watetezi Ligi Kuu Bara, wanajiandaa kushiriki Ligi ya Mabingwa barani Afrika wakati Simba watawakilisha kwenye Kombe la Shirikisho Afrika mwakani baada ya kunyakua taji ya ubingwa Kombe la FA.

Michuano ya Kombe la Mapinduzi ambayo imepangwa kuanzia hatua ya makundi, itazipa timu za Simba na Yanga fursa ya kucheza michezo mingi ya kuwapima wachezaji wao kabla ya kuanza maandalizi yao ya mechi za kimataifa.

Vigogo hao wa soka kwa upande wa Tanzania Bara wanaweza kuboresha na kuimarisha vikosi vyao kwa kutumia fursa ya kushiriki Kombe la Mapinduzi, hasa kwa kuzingatia kuna wachezaji wapya waliosajiliwa katika dirisha dogo lililofungwa hivi karibuni.

Naamini kabisa wachezaji chipukizi kama Yohana Nkomola na wengine, huu ndio wakati wao wa kuwaonyesha wadau wa soka kuwa hawakusajiliwa kwa makosa kwenye timu hizo.

Endapo watapata nafasi ya kucheza, hii itakuwa nafasi ya pekee kwao kuhakikisha wanafanya vema ili kujijengea jina na kuaminika zaidi kwa  benchi la ufundi.

Makocha pia wanatakiwa kuitumia fursa hii kuwapa nafasi wachezaji wao hasa wale waliokuwa hawapati nafasi ili waonyeshe uwezo.

Kupitia mashindano haya Simba na Yanga zinaweza kuibua wachezaji ambao wataleta mabadiliko makubwa katika vikosi hivyo na kupata nafasi ya kucheza mechi za Ligi Kuu pamoja na zile za kimataifa.

Mbali na vigogo hao, klabu ya Singida United inayoshiriki Kombe la Mapinduzi kwa mara ya kwanza pia inaweza kunufaika na fursa hiyo na kujipanga zaidi.

Licha ya usajili mzuri waliofanya Singida United, pia mafanikio watakayoyapata yatawasaidia kuongeza makali kwenye mechi za Ligi Kuu msimu huu katika kuhakikisha wanafanya vizuri.

Ugeni wao kwenye michuano ya Mapinduzi usiwe ni kisingizio cha wao kufanya vibaya, bali iwe ni fursa kwao kutamani kufika mbali kwa kuiga mambo yenye manufaa kutoka kwa wapinzani.

Kikosi cha URA chenye historia ya kufanya vizuri kwenye Kombe la Mapinduzi, pia kina mikakati ya kuchukua ubingwa lakini kwa ushindani uliopo wengi wanaamini kombe hilo litabaki nyumbani.

Maandalizi yaliyofanywa na timu hizo ni kiashiria kwamba kombe hilo halitatoka nje ya Tanzania bali litabaki hapa nyumbani na kunogesha sherehe za Mapinduzi pamoja na kujenga heshima kwa timu zetu.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU