HII HAPA‘FIRST ELEVEN’KALI EPL 2017

HII HAPA‘FIRST ELEVEN’KALI EPL 2017

651
0
KUSHIRIKI

LONDON, England

HATIMAYE leo ni Januari mosi, mwaka 2018, ikiwa ni baada ya kuzimaliza siku 365 za mwaka 2017.

Kwa mashabiki wa soka, Ligi Kuu England (EPL), ilikuwa burudani kubwa kwao kwa kipindi chote cha mwaka jana, huku uhondo ambao bado unaendelea ukiwa kwenye vita ya ubingwa ambapo ni Man City na Man United.

Lakini pia, kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20, mashabiki waliishuhudia Arsenal ikishindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hata hivyo, ulikuwa ni mwaka mzuri kwa baadhi ya wachezaji ambao waling’ara kwenye timu zao. Kwa kuzingatia ubora wao kwa kipindi chote cha mwaka 2017, hawa ni wachezaji wanaouda ‘first eleven’    kali ya EPL.

Kipa: De Gea (Man United)

Mhispania huyo ameuanza vizuri msimu huu.Kiwango alichokionesha katika mchezo dhidi ya Arsenal, ambao ulikuwa wa 15, kiliiokoa Man United isipoteze pointi tatu.

Kabla ya mchezo wa juzi, David de Gea mwenye umri wa miaka 27, alikuwa ameokoa mabao ya wazi 70.

Beki wa kushoto: Alonso (Chelsea)

Tangu alipong’ara katika mchezo wa pili dhidi ya Tottenham, Marcos Alonso amekuwa mchezaji muhimu kwenye safu ya ulinzi ya Chelsea.

Nyota huyo ameingia kikosi cha kwanza katika mechi zote za Ligi Kuu England na ameipachikia timu hiyo jumla ya mabao matano.

Beki wa kati: Otamendi (Man City)

Ubora wake umeifanya Man City kuwa na beki imara msimu huu na sifa yake kubwa inayomvutia kocha Pep Guardiola ni uwezo wa kukaa na mpira.

Kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Crystal Palace, tayari Otamendi alikuwa amepiga pasi 1,606 katika michezo ya Ligi Kuu England, ndiye mchezaji aliyekuwa anayeongoza katika kazi hiyo na alikuwa ameshafunga mabao manne. Chini ya beki huyo mwenye umri wa miaka 29, Man City walikuwa wameruhusu mabao 12 pekee.

Beki wa kati: Azpilicueta (Chelsea)

Kwa misimu miwili mfululizo, Cesar Azpilicueta amekuwa mchezaji muhimu kwa Chelsea. Kabla ya mchezo wa juzi dhidi ya Stoke, tayari alikuwa na bao moja, ‘asisti’sita, krosi 43, huku mipira yake mirefu 69 ikiwa imewafikia walengwa.

Beki wa kushoto: Walker (Man City)

Guardiola alilipa Pauni milioni 50 kumng’oa Tottenham na ni kutokana na uwezo wa beki huyo katika kuzuia na kushambulia.

Kwa mujibu wa Guardiola, Kyle Walker ndiye beki bora wa pembeni duniani.

Kiungo wa kati: Silva (Man City)

Sifa kubwa ya Mhispania huyo ni pasi zake ambazo asilimia 89 huwafikia walengwa. Mbali na hilo, David Silva amekuwa mzuri pia katika upachikaji mabao.

Kabla ya kuwavaa Palace jana, Silva alikuwa ameshafunga mara tano na kutoa ‘asisti’ nane.

Kiungo wa ulinzi: Fernandinho (Man City)

Huenda wengi hawajui kuwa ubora walionao Man City msimu huu unachangiwa kwa kiasi kikubwa na uimara wa safu yake ya kiungo.

Ingawa Fernandinho hazungumziwi sana kama De Bruyne au Sterling, pasi na uwezo wake wa kucheza mipira ya vichwa vimekuwa vikiibeba Man City.

Lakini pia, takwimu kabla ya mchezo wao na Palace zilionesha kuwa Mbrazili huyo mwenye umri wa miaka 32, ameshaifungia timu hiyo mabao mawili na kutoa asisti tatu.

Kiungo wa kati: De Bruyne (Man City)

Tangu alipojiunga na Man City, hakuna mchezaji wa Ligi Kuu England aliyewahi kumzidi ‘KDB’ kwa asisti na msimu huu ameshafanya hivyo mara sita, huku akipasia nyavu mara tisa. Hiyo ni kabla ya mchezo wa jana.

Mashabiki wa Ligi Kuu England watakiri kuwa pasi yake iliyomfikia Leroy Sane na kufunga bao la pili katika ushindi wa mabao 7-2 dhidi ya Stoke itabaki kwenye kumbukumbu zao kwa miaka mingi.

Winga kulia: Salah (Liverpool)

Mwanasoka huyo raia wa Misri amekuwa kwenye kiwango bora tangu alipotua Liverpool, ambapo katika mechi za Ligi Kuu pekee, ameshafunga mabao 17 na kutoa asisti tano.

Huku silaha kubwa ikiwa ni mguu wake wa kushoto, mashuti yake hulenga lango kwa asilimia 52.

Mshambuliaji wa kati: Kane (Tottenham)

Katika kila misimu kati ya mitatu iliyopita, Kane amefunga si chini ya mabao 20. Tangu kuanza kwa msimu huu, tayari ameshatupia 18.

Licha ya kuwa ndiyo kwanza ana umri wa miaka 24, tayari nyota huyo wa kimataifa wa England anawekwa meza moja na mastaa Lionel Messi (30) na Cristiano Ronaldo (32).

Winga kushoto: Sterling (Man City)

Kwa takwimu za kabla ya mchezo wao wa jana dhidi ya Palace, nyota huyo mwenye asili ya Jamaica alikuwa ameshafunga mabao 13 na kutoa asisti nne tangu kuanza kwa msimu huu. Kwa kufanya hivyo, ni Kane na Salah pekee waliokuwa wamemzidi.

Sterling amekuwa mchezaji muhimu Man City, hasa baada ya ujio wa Guardiola. Silaha yake kubwa katika kuwatesa mabeki wa timu pinzani ni kasi.

Watakaotokea benchi

Nick Pope (Burnley), Harry Maguire (Leicester City), James Tarkowski (Burnley), Antonio Valencia (Manchester United), Wilfred Ndidi (Leicester City), Leroy Sane (Manchester City), Philippe Coutinho (Liverpool), Sergio Aguero (Manchester City)

Kocha

Pep Guardiola (Man City)

Mfumo

4-3-3

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU