MACHO YOTE URUSI 2018

MACHO YOTE URUSI 2018

333
0
KUSHIRIKI

NA DOMINIC ISIJI

KARIBU mwaka 2018 ambao umesheheni matukio mengi ya kimichezo. Ni mwaka ambao kama taifa tunatarajia kuvuna medali kibao katika mashindano ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika Aprili 4 hadi 15, jijini Gold Coast, nchini Australia.

Lakini kikubwa ambacho wadau wengi wa michezo hususan soka wanasubiri mwaka huu wa 2018, ni Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Urusi. Mashindano haya yanarudi tena barani Ulaya tangu yafanyike mwaka 2006 nchini Ujerumani ambapo Italia walitwaa ubingwa baada ya kuifunga Ufaransa 5-3 kwa penalti.

Fainali hiyo ya 2006 ilikuwa ya kusisimua na hadi dakika 90 zinamalizika, timu zote zilikuwa zimekabana koo kwa kufungana bao 1-1. Unamkumbuka Zinedine Zidane aka Zizzou? Yeye ndiye aliyeipa Ufaransa bao dakika ya saba kwa mkwaju wa penalti kabla ya Marco Materazzi kusawazisha dakika ya 19 akitumia vyema mpira wa kona uliochongwa na mkongwe Andrea Pirlo.

Katika dakika 30 za nyongeza ambazo hazikuzaa bao lolote, kulishuhudiwa tukio la aina yake pale Zidane aliyeonekana kujawa na hasira alimshambulia kwa kichwa Materazzi aliyeanguka chini. Mwamuzi wa mchezo huo, Horacio Elizondo, raia wa Argentina, alimuonyesha Zidane kadi nyekundu na siku chache baadaye, mchezaji huyo ambaye sasa ni kocha mkuu wa Real Madrid ya Hispania aliamua kutundika daluga.

2018 kuanzia Juni 14 hadi Julai 15 ni zamu ya Urusi. Je, ni tukio gani jipya tutakalolishuhudia? Je, taifa gani litatwaa ubingwa fainali itakapofanyika Uwanja wa Luzhniki uliopo jijini Moscow? Kati ya timu 32 zilizofuzu kucheza Kombe la Dunia mwaka huu, timu 20 ikiwamo bingwa mtetezi Ujerumani, zilishiriki michuano hiyo ilipofanyika nchini Brazili miaka minne iliyopita.

Iceland na Panama ndizo timu pekee zinazoshiriki fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza ambapo mwaka huu nchini Urusi, jumla ya mechi 64 zitachezwa kwenye viwanja 12 tofauti vilivyojengwa katika majiji 11.

Bara la Afrika litawakilishwa na mataifa matano ambayo ni Misri, Tunisia, Senegal, Nigeria na Morocco. Hakuna timu kutoka Afrika ama ishawahi kutwaa kombe hilo au kutinga hatua ya nusu fainali. Umbali ambao wawakilishi wetu wameshafika ni robo fainali.

Kati ya timu tano zilizobeba matumaini ya Afrika mwaka huu, ni Senegal ambao walifika robo fainali michuano hiyo ilipoandaliwa kwa pamoja na Japan na Korea Kusini mwaka 2002. Misri ambao walizima ndoto za majirani Uganda, hawajawahi kuvuka zaidi ya hatua ya makundi na hii mara tatu wanashiriki michuano hiyo.

Kwa upande wa Nigeria, hii ni mara ya tano wanashiriki Kombe la Dunia na mara tatu fainali hizo zilipofanyika Marekani (1994), Ufaransa (1998) na Brazil (2014) walitolewa hatua ya 16 bora.

Morocco wanarudi tena Kombe la Dunia baada ya kuikosa kwa miaka 20 ambapo wamedhamiria kufanya vizuri zaidi ya mwaka 1986, kwani walifika hatua ya 16 bora fainali hizo zilipofanyika nchini Mexico.

Timu nyingine kutoka kaskazini inayobeba matumaini ya Afrika ni Tunisia, na mara nne ambapo imeshiriki michuano hiyo hawajavuka zaidi ya hatua ya makundi.

Ukiacha uwakilishi wa timu za Afrika katika Kombe la Dunia, ladha ya michuano hiyo itanogeshwa na uwepo wa wachezaji nyota kama vile Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Eden Hazard na Neymar.

 

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU