MOURINHO AKISEPA, MMOJA WAO ANATUA OLD TRAFFORD

MOURINHO AKISEPA, MMOJA WAO ANATUA OLD TRAFFORD

927
0
KUSHIRIKI

MANCHESTER, England

WAKATI Sir Alex Ferguson anatangaza kuachana na majukumu yake ya kuliongoza benchi la ufundi la Manchester United, mashabiki wa timu hiyo walitaka Jose Mourinho apewe kibarua hicho.

Hata hivyo, David Moyes akakabidhiwa mikoba hiyo lakini haikuchukua muda mrefu kabla ya kuchemsha na ndipo Man United wakatua kwa Louis van Gaal ambaye pia alifeli.

Kuondoka kwa Van Gaal kukampa nafasi Mourinho ‘Special One’ aliyekuwa akitakiwa na mashabiki wengi wa Old Trafford kutokana na rekodi yake ya kubeba mataji akiwa na timu zote alizopita.

Katika msimu wake wa kwanza, Mourinho akawasajili Paul Pogba, Zlatan Ibrahimovic na Henrikh Mkhitaryan lakini kikosi chake kikamaliza ligi kikiwa nafasi ya sita, licha ya kwamba alikipa mataji mawili (Kombe la Ligi na Ligi ya Europa).

Mwaka mmoja na nusu umepita tangu alipoanza kuinoa Man United lakini mashabiki wa timu hiyo wameanza kutilia shaka uwezekano wa kuiona timu yao ikiambulia chochote msimu huu wa 2017-18.

Tayari kikosi hicho kimeshapoteza Kombe la Ligi baada ya kutolewa na Brighton. Katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England, Man United inashika nafasi ya pili.

Lakini, mbaya zaidi ni kwamba imeachwa pointi 15 na Man City waliojichimbia kileleni na pengo hilo ni kabla ya vijana wa Pep Guardiola kushuka dimbani jana kukipiga na Crystal Palace.

Kutokana na mwenendo huo, zimeanza kuibuka taarifa kuwa huenda mabosi wa timu hiyo wakamtimua Mourinho na hiyo. Lakini je, kocha gani ambaye Man United wanaweza kumgeukia endapo watafikia uamuzi huo?

Carlo Ancelotti

Muitalia huyo hana kazi kwa sasa tangu alipotimuliwa Bayern Munich. Heshima kubwa ya Ancelotti katika ulimwengu wa soka ni mafanikio aliyozipa timu zote alizofundisha.

Kati ya ligi kubwa tano Ulaya, ni La Liga (Hispania) pekee ambako alikosa taji la Ligi Kuu na amelibeba mara tatu taji la Ligi ya Mabingwa.

Alipofika Real Madrid, alikuta orodha ya majina ya makocha wakubwa walioshindwa kuipa timu hiyo ubingwa wa michuano hiyo ya Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa).

Waliokuwa kwenye orodha hiyo ni Jose Mourinho, Juande Ramos, Manuel Pellegrini na Fabio Capello, lakini Ancelotti aliweza kulipeleka taji hilo katika msimu wake wa kwanza Santiago Bernabeu.

Akiwa amezinoa Juventus, AC Milan, Chelsea, Paris Saint-Germain, Real Madrid na Bayern Munich, ni wazi ana uzoefu mkubwa unaoweza kuibeba Man United.

Mwaka 2013, alipewa ofa ya kumrithi Sir Alex Ferguson lakini alikataa na kuamua kwenda Hispania kuinoa Real Madrid.

Diego Simeone (Atletico)

Isingekuwa rahisi kwa Atletico kuzipiku Real Madrid na Barcelona na kuchukua ubingwa wa La Liga katika msimu wa 2013-14 kama si kazi nzuri ya Simeone.

Lakini pia, tangu alipoanza kazi ya kuifundisha timu hiyo, ameifikisha mara mbili fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Sifa kubwa ya mchezaji huyo wa zamani wa Atletico, ni uwezo wake wa kuisuka safu ngumu ya ulinzi.

Mauricio Pochettino (Tottenham)

Ni mmoja kati ya makocha bora Ulaya kwa sasa na tayari ametajwa kuingia kwenye rada za PSG.

Pochettino aliwahi kutakiwa Old Trafford wakati Van Gaal akiwa kocha wa Mashetani Wekundu.  Mashabiki wa Man United watavutiwa na ujio wake kutokana na aina ya soka lake la kushambulia, mfumo unaopendwa zaidi klabuni hapo.

Leonardo Jardim (AS Monaco)

Si kocha anayetajwa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari kama walivyo Jose Mourinho na Pep Guardiola, lakini ‘CV’     za Jardim zinamruhusu kuinoa timu yoyote kubwa barani Ulaya ikiwamo Man United.

Msimu uliopita, licha ya upinzani mkali kutoka kwa matajiri PSG, Jardim aliipa Monaco taji la Ligue 1 ambalo halikuwa limetua klabuni hapo kwa kipindi cha miaka 17.

Aliiwezesha kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, akifanikiwa kuzifunga Man City ya Guardiola na Borussia Dortmund. Katika michuano mbalimbali, kikosi chake kilikuwa na wastani wa kufunga mabao matatu kila kiliposhuka dimbani.

Massimiliano Allegri (Juventus)

Kwa kipindi kifupi cha miaka mitatu iliyopita, Allegri ameipa Juve mataji matatu ya Serie A na ameifikisha mara mbili fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Lakini je, ataweza kuwafanya mashabiki wa Man United wamsahau Mourinho? Wachambuzi wa soka wanaamini huenda Allgeri akapitia wakati mgumu Old trafford kwa sababu tu hana uzoefu wa kufundisha soka nje ya Italia.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU