TUFUNIKE MASHIMO YA 2017 MICHEZONI

TUFUNIKE MASHIMO YA 2017 MICHEZONI

136
0
KUSHIRIKI

NA ZAINAB IDDY

LEO ni Jumatatu ya kwanza ya mwaka 2018, baada ya Mungu kutujalia kuvuka salama siku 366 za mwaka uliopita.

Yapo mengi yaliyojitokeza mwaka uliopita ambayo si mazuri kuruhusu yajirudie tena michezoni kwa mwaka huu wa 2018.

Baadhi ya mambo hayo yaliyojitokeza mwaka jana na kuathiri moja kwa moja sekta ya michezo ni kama masuala ya utakatishaji fedha, rushwa, upangwaji wa matokeo na viongozi kugombana na kuharibu uendeshaji wa vyama vyao vya michezo.

Mambo hayo yamesababisha viongozi wengine hasa wale wa soka kama aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamali Malinzi na aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Selestine Mwesigwa pamoja na Rais wa Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ kuingia mwaka huu wakiwa rumande.

Kuanzia Januari hadi Desemba, mashabiki wa michezo wamekuwa watu wa kulalamika tu, kutokana na kutopata kile wanachohitaji kwenye michezo hii, ikiwa ni jambo linalojirudia tangu nchi hii ilipopata uhuru miaka 56 iliyopita.

Pamoja na mchezo wa riadha ambao umekuwa ukiitoa Tanzania kimasomaso tangu miaka ya 1980 hadi sasa, lakini kumekuwa na kusuasua kiasi cha hata kushindwa kujua nini tunahitaji katika mchezo huo.

Ukija kwenye soka ndani ya miaka hiyo 56 ya uhuru, Tanzania imeshiriki michuano ya Mataifa ya Afrika mara moja nayo ilikuwa miaka 37 iliyopita, hadi sasa hatujaweza kupata tena nafasi hiyo tena.

Huu ni mwaka mpya wa 2018 ambao ni vigumu kutabiri utakuwa wa aina gani, lakini hatuna budi kupambana na changamoto zilizotukwamisha mwaka uliopita ili angalau tutimize ndoto tunazoziota kila siku kwenye sekta hii.

Kuna usemi wa Kiswahili unaosema kuteleza si kuanguka na kila penye kilio pana furaha, hivyo basi ni wakati wa kufunika mashimo tuliyoyachimba kwa mikono yetu mwaka uliopita na kudhamiria kutimiza yale yaliyoweza kufanyika kwa miaka 37 iliyopita.

Ni lazima Watanzania hususani wadau wa michezo, tutambue hakuna miujiza katika kuyafikia mafanikio, kikubwa ni kuamua nini tunahitaji na kwa wakati gani, kuthubutu, kutokata tamaa lakini pia umoja na mshikamano ni silaha kubwa.

Katika kufanikisha hili, lazima kila mmoja ayajue na kuyatimiza kikamilifu majukumu yake, kuanzia kwa wachezaji wa michezo mbalimbali, viongozi wa vyama vya michezo kuanzia kata hadi taifa, wizara husika na Serikali yake.

Ni wakati wa nchi kuwa na mipango yake ya uhakika ya kuhakikisha timu za Taifa za michezo zinaleta ushindani katika michuano mbalimbali na kuachana na tabia ya kuwa wasindikizaji kila mara.

Lakini pia vyama vya michezo husika kuanza mapema kuweka mikakati ya mwaka huu kuanzia leo, ukizingatia Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazoshiriki katika mashindano ya Jumuiya ya Madola, Aprili mwaka huu.

Ingawa tayari tumeshachelewa katika maandalizi ya timu zetu za Taifa, lakini kama vyama vya michezo na wachezaji mmoja mmoja kila mtu kwa nafasi yake akaamua kufanya jambo litakaloleta medali Tanzania, inawezekana kwani miezi minne si haba katika kutimiza nusu ya lengo.

Itakuwa jambo lisilopendeza kuona kifimbo cha malkia kilikuja Tanzania kushiriki kuwepo kwa mashindano hayo na kupokewa kwa shangwe, huku kila chama kikiahidi kuleta furaha kwa wadau wa michezo mwaka huu, kasha mwisho wa siku kama ilivyo kawaida wachezaji wanarejea kimya kimya kutokana na aibu tunayoipata.

Ni wakati wa kubadilika, huu ni mwaka mwingine wa kuanza maisha mapya huku kila mmoja akiwa na lengo la kuhakikisha Tanzania ya mwaka 2017 si hii ya 2018 katika sekta ya michezo na hili litawezekana iwapo tu tutakuwa tayari kufukia mashimo ya mwaka uliopita.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU