KAMARI ZA WENGER ZILIZOMFUNIKA FERUGUSON

KAMARI ZA WENGER ZILIZOMFUNIKA FERUGUSON

300
0
KUSHIRIKI

LONDON,   England

JUZI kocha Arsene Wenger aliweza kuvunja rekodi ya aliyekuwa mpinzani wake mkuu, Alex Ferguson ya kusimamia mechi 810 za Ligi Kuu baada ya kufikisha 811.

Kwa kufikisha mechi hizo ambapo juzi alikutana na West Brom na kutoka nayo sare ya bao 1-1 sasa Wenger, anakuwa ndiye kocha aliyedumu kwa muda mrefu katika michuano hiyo.

Katika kipindi hicho, Wenger amekuwa akisifika kwa kuwapa nafasi wachezaji chipukizi ambao baadaye walikuja kutamba tofauti na ilivyodhaniwa.

Lakini katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, baadhi ya mashabiki wamekuwa na wasiwasi kuhusu sera hiyo ya Arsenal ya kusajili chipukizi badala ya kusaka nyota kama zinavyofanya timu nyingine.

Vifuatavyo ni vifaa ambavyo pamoja na Wenger kulalamikiwa kwa sera hiyo ya kusajili makinda, lakini kwa hivi alikuwa amelamba dume.

PATRICK VIEIRA

Vieira alisainiwa kabla ya mpango wa Wenger kutoka katika timu ya  Grampus Eight hadi Highbury kukamilika na huku AC Milan ikiwa inamwinda. Lakini mchezaji huyo mwenye nguvu alikuja kung’ara na kuonekana kuwa tishio baada ya Arsenal kuwa chini ya Wenger.  Kutokana na umahiri wake Vieira aliweza kuiongoza Gunners kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu, manne ya Kombe la FA na akaichezea mechi 406. Mpaka anaondoka na kwenda kujiunga na Juventus mwaka 2005, staa huyo alikuwa bado ana uwezo wa hali ya juu.

 THIERRY HENRY

Henry alitua Arsenal zikiwa bado ni wiki mbili kabla ya kutimiza miaka 22 Agosti  1999 na akiwa ameshatwaa Kombe la Dunia, ingawa alikuwa mchezaji wa kutiliwa shaka kutokana na kipindi cha mwaka mmoja bila mafanikio akiwa na Juventus. Wenger alikuwa na maswali mengi ya kujibu kuhusu kuamua kutumia kitita cha pauni milioni 11 ili aweze kuchukua nafasi ya Nicolas Anelka.

Maswali hayo yalizidi zaidi baada ya staa huyo kucheza mechi nane za Gunners bila kufunga bao.

Hata hivyo, baada ya kutokea benchi na kisha akafunga bao muhimu ambalo liliwapa ushindi dhidi ya Southampton, Henry hakuweza kuangalia tena nyuma na tangu kipindi hicho        akawa mmoja kati ya mastraika tishio barani Ulaya.

Hadi mwaka 2007 wakati akiondoka na kwenda kujiunga na Barcelona, tayari alishatwaa mataji mawili ya Ligi Kuu England na Mchezaji bora wa mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari na mpaka sasa ndiye mfungaji bora wa muda wote Arsenal akiwa na mabao  228 aliyoyafunga katika mechi 377.

ROBERT PIRES

Wakati Henry akiwatikisa mabeki katika michuano ya Ligi Kuu England na Ulaya kwa ujumla, lakini msaada mkubwa alikuwa akiupata kutoka kwa Pires.

Staa huyo alisajiliwa kwa pauni milioni 6 akitokea Marseille mwaka 2000 wakiwa na Mholanzi Marc Overmars, ndio waliomwezesha Henry kutwaa tuzo hiyo ya mchezaji bora wa mwaka kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari msimu wa 2001-02.

Mbali na hilo, Gunners ikiwa na mastaa Freddie Ljungberg, Dennis Bergkamp  na Henry, ndiyo timu ilikuwa safu ya ushambuliaji hatari msimu wa 2003-04.

SOL CAMPBELL

Kati ya usajili huu wa Campbell,  Wenger hakuweza kutumia hata senti tano kutokana na kwamba alimchukua akiwa mchezaji huru kutoka kwa wapinzani wao Tottenham mwaka  2001.

Baada ya Campbell kutua Highbury aliweza kutwaa ubingwa wake wa kwanza wa Ligi Kuu ukiwa ni msimu wake wa kwanza na kisha akafanya hivyo msimu wa 2003-04. Katika kipindi hicho cha kwanza aliweza kucheza na wachezaji nyota kama vile Tony Adams  na Martin Keown kabla ya kukutana na  Kolo    Toure.

Staa huyo ndiye aliyeweza kumaliza ukame wa Arsenal wa kucheza dakika  995 bila kufunga bao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, katika mchezo ambao walifungwa mabao 2-1 dhidi ya  Barcelona mtanange ambao ulipigwa jijini Paris mwaka 2006 akiwa yeye ndiye aliyefunga bao la kuongoza.

ROBIN VAN PERSIE

STRAIKA Van Persie naye ni kati ya biashara nzuri ambayo Wenger aliifanya katika usajili wake. Aliwasili katika kikosi hicho mwaka 2004 kwa ada ndogo ya pauni milioni 2.75 akitokea  Feyenoord.

Baada ya kuwasili ilimlazimu kuchukua muda akijifunza kupitia kwa nyota kadhaa kama vile Henry kabla ya kuonesha makali yake katika safu ya ushambuliaji.

Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2005 hadi 2014, aliiwezesha kutwaa mataji kadhaa ya Kombe la FA.

Mbali na hilo, aliweza kuifunga Gunners mabao 132 katika michezo 278 na huku msimu wa 2011-12 aliweza kufunga mabao 37 katika mashindano yote jambo ambalo lilimfanya akabidhiwe tuzo ya mchezaji bora wa mwaka kwa wachezaji wanaocheza soka la kulipwa, kabla ya kuondoka na kwenda kujiunga na Man Utd.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU