KUMBE MADRID NDIO ZAO KUSAJILI ‘MAGARASA’ JANUARI

KUMBE MADRID NDIO ZAO KUSAJILI ‘MAGARASA’ JANUARI

685
0
KUSHIRIKI

MADRID, Hispania

TAYARI presha ya usajili wa dirisha dogo la Januari imeshaanza na baadhi ya timu zimeanza kunasa saini za wachezaji zinaowataka.

Real Madrid wanaifukuzia kwa udi na uvumba huduma ya Eden Hazard wa Chelsea na wametajwa kuwa tayari kulipa zaidi ya Pauni milioni 100 kukamilisha dili hilo.

Hata hivyo, kwa upande wa Madrid, wamekuwa na bahati mbaya ya kuchukua ‘magarasa’ kila wanaposajili Januari.

Licha ya kwamba tayari wameshambeba kipa wa Athletic Bilbao, Kepa Arrizabalaga, ambaye atasaini kwa ada ya Euro milioni 20, huenda nyota huyo akashindwa kung’ara Santiago Bernabeu.

Mpaka sasa, Madrid wameshasajili jumla ya wachezaji 18 katika vipindi tofauti vya dirisha la usajili la Januari lakini wengi wao walichemsha.

Kati ya hao, Marcelo ameonekana kuepuka balaa hilo kwani bado yupo kikosini kwa msimu wa 12 licha ya kwamba alisajiliwa kwa fedha kiduchu (Euro milioni6.5) akitokea Fluminese ya Brazili.

Katika orodha ya hao waliosajiliwa Januari na kuchemsha Madrid, lipo jina la Julien Faubert ambaye alitokea West Ham na kuigharimu Madrid kitita cha Euro milioni 1.5.

Kiungo huyo raia wa Ufaransa alijizolea umaarufu mkubwa Madrid kwa kuwa mmoja kati ya wachezaji waliokuwa na nafasi ya kudumu benchi.

Lakini pia, kali zaidi ni tukio lake la kupitiwa na usingizi akiwa benchi katika mchezo ambao Madrid waliifuata Villareal.

Wengine waliosajiliwa Januari na mabosi wa Madrid na kuishia kuvuna mishahara minono ni Emanuel Adebayor, Dani Parejo, Javier Portillo, Lucas Silva na Ze Roberto.

Lakini pia, katika vipindi vyote vya usajili wa Januari, ambapo Madrid wamechukua wachezaji 18, tayari timu hiyo imetumia kiasi cha Euro milioni 142.8.

Tayari Madrid wako njiani kuchukua straika mpya Januari hii, hasa baada ya nyota wao Karim Benzema kuumia.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, mabosi wa timu hiyo wameshamalizana na Valencia na ni mpachikaji mabao Rafa Mir ndiye atakayetua Bernabeu.

Taarifa zilidai kuwa Madrid wamekubali kutoa ada ya Euro 500,000, hivyo mchezaji huyo ataelekea jijini Madrid hapo baadaye.

Je, straika huyo atakapotua Madrid atakumbana na kilichowakuta Portillo, Higuain, Adebayor, Antonio Cassano na Klaas Jan Huntelaar ambao nao walisajiliwa kipindi hiki cha usajili wa Januari?

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU