WAMEIZINGUA LIVER KINOMA MWAKA 2017

WAMEIZINGUA LIVER KINOMA MWAKA 2017

519
0
KUSHIRIKI

MERSEYSIDE, England

HATIMAYE mwaka 2017 umekwenda zake na kuacha matukio mengi ya kukumbukwa katika ulimwengu wa michezo, hasa soka.

Achana na Neymar kwenda zake PSG. Weka mbali moto aliouwasha Pep Guardiola na vijana wake wa Manchester City. Bado yapo mengi yatakayobaki vichwani mwa mashabiki wa kandanda.

Mwaka 2017 haukuwa mzuri sana kwa kikosi cha Liverpool, kwani licha ya kuwa walimaliza msimu wa 2016-17 wakiwa ‘top four’, hivyo kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, bado hakikuweza kuchukua hata taji moja.

Lakini je, ni wachezaji gani walioikwamisha Liver kwa kiasi kikubwa mwaka jana na hata kuifanya imalize msimu bila kombe?

Daniel Sturridge 

Ni kweli amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara lakini licha ya kocha Jurgen Klopp kumpa zaidi ya dakika 500, Sturridge alishindwa kuisaidia Liver katika safu ya ushambuliaji.

Nyota huyo wa zamani wa Chelsea alipoteza nafasi nyingi za kufunga mabao na tayari ametajwa kwenye orodha ya wanaoweza kupigwa bei.

Loris Karius

Mfano mzuri wa kipa huyo kuizingua Liver mwaka jana ni katika mchezo wao dhidi ya Arsenal. Mara nyingi alionekana kutojiamini langoni, hasa pale alipokuwa na mpira.

Lakini pia, Karius aliruhusu bao jepesi katika mchezo wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Spartak Moscow.

Jordan Henderson

Mwaka 2017 haukuwa mzuri kwa nahodha huyo wa Anfield. Licha ya kucheza kwa kiwango cha juu dhidi ya Leicester City na Spartak Moscow, bado Henderson si mchezaji wa kumtegemea katika mechi kubwa.

Miongoni mwa makosa yake katika eneo la kiungo wa ulinzi ni pamoja na pasi za ovyo. Kwa kiwango chake cha mwaka 2017, tayari wachambuzi wa soka barani Ulaya wamedai kuwa Henderson hastahili kuwa nahodha.

Simon Mignolet

Mashabiki wengi wa Liver hawakumkubali kipa huyo raia wa Ubelgiji. Ni kutokana na makosa yake ya kizembe ambayo yamekuwa yakiwapotezea ushindi mara kwa mara.

Hata wachambuzi wanaamini kuwa Liver wanahitaji mlinda mlango mpya wakati wa dirisha dogo la usajili.

Kama alivyo Karius, Mignolet ambaye ndiye kipa namba moja, amefanya makosa mengi mwaka 2017. Kwa mashabiki wa Anfield, walikerwa zaidi na uzembe wake uliowagharimu katika michezo dhidi ya Arsenal na Tottenham.

Kabla ya mchezo wa jana, takwimu zilionesha kuwa Mignolet amefanya makosa 10 tangu Klopp alipotua England kuinoa Liver mwaka 2015. Kwa wachambuzi, hiyo ni hatari kwa timu yenye mipango ya kuchukua ubingwa.

Dejan Lovren

Ni mchezaji mwingine wa Liver ambaye hata anapokuwa uwanjani mashabiki wa Liver huwa na presha. Licha ya Klopp kumwamini na kumpa nafasi mara kwa mara, Lovren alivurunda mwaka 2017.

Staa huyo wa timu ya Taifa ya Croatia anatajwa kuwa ndiye beki anayeongoza kwa kufanya makosa mengi kwenye kikosi cha Klopp.

Lovren aliigharimu Liver dhidi ya Sevilla, Tottenham Hotspur, kabla ya kuwapa penalti mahasimu wao wa jijini Merseyside, Everton.

Mchezaji huyo amekaa Anfield kwa miaka mitatu sasa lakini ameshindwa kuwafanya mashabiki wa Liver wamwamini na mara nyingi anapopata nafasi ya kucheza huwa anawachefua.

Hata usajili wa Pauni milioni 75 walioufanya Liver kwa Virgil Van Dijk umetokana na majanga ya eneo la beki wa kati ambalo Lovren amekuwa akilitumia kuigharimu timu hiyo mwaka jana.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU