WAPACHIKAJI MABAO WANAOSUMBUA MAKIPA BUNDESLIGA

WAPACHIKAJI MABAO WANAOSUMBUA MAKIPA BUNDESLIGA

230
0
KUSHIRIKI

MUNICH, Ujerumani

BAADA ya Ligi Kuu England, La Liga na Bundesliga ndizo ligi zinazofuatiliwa na mashabiki wengi wa kandanda duniani.

Mbali na sifa nyingine ikiwamo soka la kutumia nguvu, kivutio kikubwa cha Bundesliga ni uwepo wa Bayern Munich, Borussia Dortmund, ambazo pia zimekuwa zikifanya vizuri kwenye michuano ya Ulaya.

Kama ilivyo England na La Liga ambazo zinatambia mastaa kama Harry Kane, Alexis Sanchez, Philippe Coutinho, Kevin De Bruyne, Paul Pogba, Bundesliga pia ina utitiri wa vipaji.

Tangu kuanza kwa msimu huu wa Bundesliga, hawa ni baadhi tu ya washambuliaji wanaotisha kwa kuwatungua walinda mlango wa timu pinzani.

Robert Lewandowski (Bayern)

Ni ngumu kuitaja orodha ya wapachikaji mabao hatari barani Ulaya na kuliweka kando jina la mwanasoka huyo raia wa Poland ambaye sasa ana umri wa miaka 29.

Ndiye anayeongoza kwenye vita ya kukiwania kiatu cha mfungaji bora akiwa amewatungua walinda mlango mara 15.

Katika mechi za michuano mbalimbali, nyota huyo ameshafunga jumla ya mabao 21 katika mechi 26.

Pierre-Emerick Aubameyang (Dortmund)

Nyota huyo wa kimataifa wa Gabon amekuwa mtambo wa mabao wa Dortmund kwa miaka mingi sasa.

Katika dakika zake 1327, Aubameyang ameshahusika katika mabao 17. Staa huyo amefunga mabao 13 na kutoa asisti nne.

Katika kikosi hicho, amekuwa akishirikiana vizuri na Christian Pulisic ambaye ameshahusika katika mabao manne.

Lars Stindl (Monchengladbach)

Ndiye silaha ya mabao ya Gladbach licha ya kwamba  amekuwa akifanya kazi kubwa kwenye eneo la kiungo. Chini ya kocha Dieter Hecking, staa huyo wa zamani wa Hannover amekuwa tegemeo kikosini.

Tangu kuanza kwa msimu huu, Lars Stindl raia wa Ujerumani amehusika katika mabao sita, akifunga manne na kutoa ‘asisti’ mbili.

Akiwa na umri wa miaka 29, Stindl anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha timu ya Taifa ya Ujerumani kitakachokwenda Urusi mwaka huu kucheza fainali za Kombe la Dunia.

Mark Uth (Hoffenheim)

Licha ya msimu uliopita alikuwa akifanya vizuri katika mechi alizokuwa anatokea benchi lakini mambo yamebadilika.

Msimu huu, tayari mchezaji huyo ameshafunga mabao tisa katika mechi 16, akionekana kuziba pengo la straika Sandro Wagner ambaye anasumbuliwa na majeraha.

Hata hivyo, mkataba wake unakaribia kumalizika na tayari amehusishwa kutimkia Schalke.

Finnbogason (Augsburg)

Msimu uliopita ulikuwa mgumu kwa staa huyo wa kimataifa wa Iceland. Lakini, katika mechi zake 16 msimu huu, tayari Alfred Finnbogasson ameshaziona nyavu mara 11.

Katika chati ya wanaokifukuzia kiatu cha mfungaji bora wa Bundesliga, amezidiwa na mastaa Robert Lewandowski (15) na Aubameyang (13).

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU