KUMBE FEDHA ZA CHIRWA ZILITAFUNWA

KUMBE FEDHA ZA CHIRWA ZILITAFUNWA

2221
0
KUSHIRIKI
NA HUSSEIN OMAR

IMEBAINIKA kuwa kuna mchezo mchafu uliofanyika na kusababisha mvutano kati ya straika wa kimataifa wa Zambia, Obrey Chirwa na mabosi wake wa Yanga.

Chirwa alikuwa mshambuliaji pacha wa Donald Ngoma katika klabu ya FC Platinum ya Zimbabwe kabla ya wote kutua Yanga kwa vipindi tofauti.

Baada ya kusimama kwa Ligi Kuu Tanzania Bara kupisha michuano ya Chalenji, Chirwa alikwenda Zambia na baadaye kugoma kurejea Jangwani, akiwashinikiza mabosi wa Yanga kummalizia fedha zake za usajili.

Kukosekana kwa Chirwa kwenye kikosi cha Yanga, hasa kwa kipindi hiki ikiwa kwenye vita kubwa ya kutetea ubingwa wao wa Bara, kumekuwa kukiwachanganya mno watu wa Yanga kiasi cha baadhi yao kumwona kama msaliti.

Lakini taarifa za uhakika ambazo BINGWA limezinyaka, fungu la usajili wa Chirwa aliyejiunga na Yanga mwaka 2016, lilishatengwa ila wajanja wachache walizizuia na kugawana kinyemela.

Kigogo mmoja wa Yanga ambaye hakutaka jina lake liwekwe hadharani, aliliambia gazeti hili kwamba wakati nyota huyo anasajiliwa mwaka 2016, tayari alishatengewa Dola 100,000 (zaidi ya Sh milioni 200 za Tanzania), lakini sehemu ya fedha hizo zilichotwa na wapiga dili.

“Chirwa alisajili kipindi cha uongozi wa Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa zamani wa timu, Baraka Deusdedith, jamaa alitengewa fedha zake zote, lakini kuna ujanja ambao ulifanyika na fedha zake kupigwa,” alisema.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Mwenyekiti huyo bilionea wa Yanga hakuwa na muda wa kulimbikiza madeni ya fedha za usajili wa wachezaji, lakini wajanja wachache kutoka ofisi ya Mhasibu na Kamati ya Usajili ya wakati huo, ndio wanaofahamu fedha za usajili wa Chirwa zilivyopigwa.

“Kuna mambo mengi sana yanakwenda ndivyo sivyo pale klabuni, kuna ufisadi wa hali ya juu, usione wachezaji wanalalamika, wanapigwa sana kuanzia mishahara mpaka fedha zao za usajili, si Chirwa tu peke yake, hali ni mbaya,” aliongeza mtoa habari wetu huyo.

Chanzo hicho kilikwenda mbali na kumwonea huruma Katibu Mkuu wa sasa, Charles Boniface, kwa jinsi anavyohangaika kulipa madeni ya zamani, yakiwamo malimbikizo ya mishahara na fedha za usajili wa wachezaji.

“Mkwasa mwanaume, ameikuta Yanga ipo taaban kutokana na wajanja wachache kupiga dili za ndani kwa ndani, anapambana kuhakikisha timu inasafiri, inapata mishahara… kwa kweli nampa tano,” alisisitiza.

Kwa upande mwingine, BINGWA lilimtafuta Baraka ili kuzungumzia juu ya kashfa hiyo, ambapo alisema suala hilo lipo kwenye mamlaka ya uongozi wa sasa chini ya Mkwasa na kwamba hana mamlaka ya kulizungumzia kwa kuwa nyaraka zote aliziwakilisha kwake.

“Suala la Chirwa nadhani ni vyema akaulizwa Mkwasa kwa kuwa nyaraka zote niliziwasilisha kwake na ndio zinaonyesha kama alilipwa ama hakulipwa, mimi nikijibu nitakuwa nakwenda kinyume na utaratibu wa klabu,” alisema Baraka.

Licha ya sekeseke hilo, tayari Yanga wameshamalizana na Chirwa na mpachikaji mabao huyo anatarajiwa kutua nchini leo kuungana na wenzake waliopo Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Taarifa za ndani kutoka Yanga zililiambia BINGWA kwamba, nyota huyo ameshalipwa kiasi chote cha fedha alichokuwa anadai.

“Mambo mazuri sasa, tumeshamalizana naye na leo anakuja nchini kuendelea na majukumu yake,” kilisema chanzo hicho.

Hivi karibuni Chirwa alitajwa kuwa katika mpango wa kusajiliwa na klabu ya Simba mwishoni mwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, japo Wekundu wa Msimbazi hao wamekuwa wakikanusha hilo.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU