LAWAMA ZOTE ZA WENGER KWA WAAMUZI MSIMU HUU HIZI HAPA

LAWAMA ZOTE ZA WENGER KWA WAAMUZI MSIMU HUU HIZI HAPA

244
0
KUSHIRIKI

LONDON, England

KOCHA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger, mapema wiki hii alinukuliwa akitoa povu kutokana na maamuzi ya refa, Anthony Taylor, baada ya kikosi chake kulazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya Chelsea kwenye mechi iliyopigwa Emirates.

Mfaransa huyo alionekana kuvurugwa na uamuzi wa Taylor kuamuru penalti ipigwe kuelekea lango la timu yake, penalti iliyowekwa kimiani na Eden Hazard, baada ya Mbelgiji huyo kuchezewa rafu na Hector Bellerin.

Bao hilo lilikaribia kuwapa ushindi Chelsea, ambao baada ya kuongoza mchezo kwa kupitia kwa beki wa kushoto, Marcos Alonso, kiungo Jack Wilshere, aliisawazishia Arsenal kabla ya Hazard kupigilia msumari wa pili kwenye lango la Petr Cech.

Lakini ‘The Gunners’ hao hawakukubali kutandikwa nyumbani kwao na ndipo walipopambana vilivyo na kusawazisha tena kupitia kwa beki wao wa kulia, Bellerin.

Lawama zake hizo sasa zimemsababishia kufungiwa mechi moja, ambapo alichagua kutokaa kwenye benchi la ufundi katika mtanange wa Kombe la FA dhidi ya Nottingham Forest ugenini, ili aweze kuwepo katika mechi ya Kombe la Carabao dhidi ya Chelsea wiki ijayo.

Hiyo si mara ya kwanza, hizi hapa lawama zake za nyuma dhidi ya waamuzi wa Ligi Kuu England msimu huu.

 

Agosti 19, Stoke 1-0 Arsenal

Wenger alishuhudia kikosi chake kikikutana na kichapo hicho wakiwa ugenini dhidi ya Stoke City, lakini kama hiyo haitoshi, bao lililofungwa na mshambuliaji wake, Alexandre Lacazette, lilikataliwa baada ya straika huyo kujenga kibanda.

Hata hivyo, marudio ya video yalidhihirisha kwamba bao lilikuwa halali, ingawa haikuwa kazi rahisi kulikataa na baada ya mechi, Wenger alishusha lawama zote kwa mwamuzi wa kati siku hiyo, Andre Marriner na wasaidizi wake kwa kusema: “Lacazette hakuotea. Wakati anaupiga ule mpira hakuwa ‘offside’ kabisa.”

 

Oktoba 14, Watford 2-1 Arsenal

Arsenal ilianza vizuri mchezo huo na kupata bao la kuongoza, lakini fowadi wa Watford, Richarlison alianguka ndani ya 18 katika harakati za kuwania mpira na beki wa Arsenal, Bellerin na mwamuzi, Neil Swarbrick, akaizawadia ‘The Hornets’ penalti.

Wenger alikuwa na haya ya kusema: “Kwa upande wangu, ile haikuwa penalti. Lakini kwa sababu aliamua refa, ndiyo maana ikawa vile. Inasikitisha. Ni uamuzi uliotolewa katika kipindi ambacho Watford walihitaji kitu cha kuwarudisha mchezoni. Bila penalti, wasingepata bao.”

 

Novemba 5, Man City 3-1 Arsenal

Washika mitutu hao wa London walishindwa kufurukuta mbele ya Man City kwenye dimba la Etihad na Wenger alikasirishwa zaidi baada ya mwamuzi kuamuru penalti dhidi ya timu yake na City wakapata bao lao la pili.

Penalti hiyo ilitokana na beki wa Arsenal, Nacho Monreal, kumwangusha Raheem Sterling ndani ya 18 na refa, Michael Oliver, akatoa uamuzi wake na baada ya mchezo kumalizika, Wenger alisema: “Waamuzi hawajafanya kazi yao kwa ufasaha. Ni maamuzi yasiyo sahihi kila kukicha. Naamini ile haikuwa penalti. Sote tunajua Sterling alijiangusha kama kawaida yake na bao lao la tatu lilikuwa la kuotea.”

 

Desemba 31, West Brom 1-1 Arsenal

Arsenal walikaribia kuondoka na pointi zote tatu kwenye uwanja wa ‘The Hawthorns’ kabla ya mwamuzi, Mike Dean, kuwapa penalti wenyeji kufuatia mpira wa krosi ya Kieran Gibbs kuugusa mkono wa Calum Chambers wa Arsenal.

Marudio yalionesha kwamba, mkono wa Chambers ulitulia kwenye eneo lake na haukuelekea kwenda kuugusa mpira ikiwa na maana kwamba, penalti haikuwa halali.

“Ninachoelewa ni kwamba waamuzi wanatakiwa kuufanya mchezo wa soka upendeze kwa kutoa maamuzi chanya yatakayowaridhisha mashabiki jukwaani, si kitu cha kupendeza kutoa maamuzi ya namna ile katika dakika za mwisho kabisa.”

 

ADHABU KALI ZILIZOWAHI KUMKUMBA WENGER

2000- Kufungiwa mechi 12 na faini kali kufuatia mkwaruzano na mwamuzi msaidizi (fourth official) katika mchezo dhidi ya Sunderland. Hata hivyo, alipunguziwa faini hadi pauni 10,000 baada ya kukata rufaa.

2007- Alitolewa nje na kufungiwa mechi moja kutokana na kuzozana na mwamuzi wakati wa mtanange wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

2011- Mwaka huo, Wenger, alikutana na adhabu ya kufungiwa mechi moja kufuatia kauli yake dhidi ya mwamuzi aliyechezesha pambano la Arsenal na Barcelona. Adhabu iliongezwa hadi mechi mbili na faini ya pauni 10,000.

2017- Msimu huu pia alikutana na adhabu ya kufungiwa mechi nne baada ya kumsukuma na kumkaripia mwamuzi dhidi ya Burnley.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU