CHIRWA ATINGA ZENJI KUIPA YANGA UBINGWA

CHIRWA ATINGA ZENJI KUIPA YANGA UBINGWA

1708
0
KUSHIRIKI

NA HUSSEIN OMAR


th

WAKATI mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa, akitarajiwa kutua Zanzibar kukiongezea nguvu kikosi chake, Kocha Mkuu wa timu hiyo, George Lwandamina, ameelezea jinsi anavyotumia simu yake kumpa maelekezo msaidizi wake upande wa mazoezi ya viungo, Noel Mwandila.

Akizungumza na BINGWA kutoka nchini kwao Zambia jana, Lwandamina aliyeahidi kurejea nchini wiki hii kuendelea na majukumu yake baada ya kumaliza matatizo ya kifamilia yaliyokuwa yakimkabili, alisema japo hajawahi kuona mechi yoyote ya timu yake ya michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea Zanzibar, lakini amekuwa karibu mno na wasaidizi wake kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.

“Nashukuru nimemaliza salama matatizo yangu ya kifamilia, nategemea kurejea huko wiki ya pili ya Januari,” alisema Lwandamina na kuongeza:

“Japo nipo mbali na timu, lakini nimekuwa nikiwasiliana na wenzangu huko Zanzibar kwa simu na kutoa ushauri pale inapolazimu kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.”

Juu ya Chirwa aliyeelezewa kurejea nchini mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kumalizana na klabu yake hiyo juu ya madai yake ya fedha za usajili, anaungana na wenzake Zanzibar kuongeza nguvu kuelekea mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Singida United utakaopigwa leo.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema: “Japo mimi si msemaji wa klabu, lakini ninachofahamu Chirwa anaondoka kesho (leo) asubuhi kwenda Zanzibar kuiongezea timu nguvu kwenye mashindano ya Mapinduzi ili timu iweze kutwaa ubingwa.”

Katika michuano hiyo, tayari Yanga imejihakikishia kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kujikusanyia pointi tisa kutokana na mechi tatu, ambapo mchezo wao wa leo dhidi ya Singida utakuwa ni wa kuwania uongozi wa Kundi B.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU