SIMBA SC YAMKIMBIA CHIRWA ZENJI

SIMBA SC YAMKIMBIA CHIRWA ZENJI

1273
0
KUSHIRIKI
NA MWANDISHI WETU

SIMBA imetupwa nje ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, baada ya kufungwa bao 1-0 na URA ya Uganda katika mchezo uliopigwa jana jioni kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Wekundu wa Msimbazi hao wamejikuta wakiondoka visiwani humo wakipishana na mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa ambaye alifika huko juzi jioni ili kukiongezea nguvu kikosi chake, hasa iwapo wangelazimika kukutana na watani wao hao wa jadi.

Kwa kupoteza mchezo wa jana, Simba wamebakiwa na pointi zao nne walizovuna ndani ya mechi nne wakizikodolea macho Azam na URA walizokuwa nazo Kundi A zikitinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Wakati URA ikiongoza kundi hilo kwa kuwa na pointi 10 baada ya kushinda mechi tatu na sare moja, Azam wamejikusanyia pointi tisa, wakipata ushindi mara tatu na kupoteza mmoja.

Katika mchezo huo wa jana wa mwisho wa kundi A, bao la URA lililoizamisha Simba lilifungwa na Deboss Kalama dakika ya 45 baada ya kuwalamba chenga walinzi wa wapinzani wao hao kabla ya kupiga shuti kali la chinichini lililomshinda kipa wa Wekundu wa Msimbazi hao, Emmanuel Mseja.

Mchezo huo ulianza kwa presha kubwa huku Simba wakianza kwa kasi na kushambulia zaidi dakika za mwanzo ambapo dakika ya saba tu, Shiza Kichuya alipiga shuti la kushtukiza, lakini mpira uliokolewa na kipa wa URA, Alionzi Nafia.

Dakika ya 14, mshambuliaji wa Simba, John Bocco, alishindwa kumalizi krosi murua iliyopigwa na beki Asante Kwasi na mpira kuokolewa na kipa wa URA.

URA walihamisha mashambulizi kwenda upande wa Simba ambapo dakika ya 26, Nicholas Kagaba alipiga shuti la mbali lakini liligonga mwamba.

Dakika ya 27, Moses Kitandu wa Simba, alipiga shuti kali baada ya kugeuka na mpira, lakini umakini wa kipa wa URA, ulisaidia kuokoa hatari hiyo langoni kwake.

Beki mpya wa Simba, Kwasi, alichonga krosi matata dakika ya 30 iliyomkuta Bocco ambaye hata hivyo mpira wa kichwa aliopiga uliokolewa na kipa wa URA.

URA walifanya mabadiliko dakika ya 36 kwa kumtoa Moses Sseruyide na nafasi yake kuchukuliwa na Hudu Mulikyi, huku Simba pia wakifanya hivyo dakika ya 45, akitoka Kichuya na nafasi yake kuchukuliwa na Mohamed Ibrahim ‘Mo’.

Kipindi cha pili, Simba walianza kwa kuwatoa wachezaji watatu, Nicolas Gyan, Mwinyi Kazimoto na Jonas Mkude na nafasi zao kuingia Yusuph Mlipili, Said Ndemla na James Kotei.

Dakika ya 55 ya mchezo huo, Kwasi nusura aipatie Simba bao la kusawazisha kwa mpira wa faulo, nje kidogo ya 18, lakini shuti lake lilikwenda juu kidogo ya mlingoti wa goli.

Simba waliendelea kusaka bao la kusawazisha kwa nguvu, huku kocha wao, Massoud Djuma, akiendelea kufanya mabadiliko ambapo dakika ya 56, alimtoa Muzamir Yasin na nafasi yake kuingia Laudit Mavugo.

Hata hivyo, mabadiliko hayo kwa Simba hayakuweza kuzaa matunda kwani wapinzani wao walizidi kujilinda huku dakika ya 58, URA wakimtoa mfungaji wa bao lao, Deboss  na nafasi yake kuchukuliwa na Jimmy Kulaba.

Kikosi cha Simba: Emmanuel Mseja, Nicolas Gyan/James Kotei dk46, Asante Kwasi, Jjuuko Murshid, Erasto Nyoni, Jonas Mkude/Said Ndemla dk46, Mwinyi Kazimoto/ Yusuph Mlipili dk46, Muzamiru Yassin/Laudit Mavugo dk56, Moses Kitandu, John Bocco na Shiza Kichuya/Mohamed Ibrahim dk45.

URA: Alionzi Nafia, Enock Kibumba, Brian Majwega, Allam Munaaba, Patrick Mbowa, Julius Mutyaba, Nicholas Kagaba/Steven Mponza dk90, Deboss Kalam/ Jimmy Kalaba dk 58, Peter Lwasa/Denis Kamanzi, Moses Sseruyide/Hudu Mulikyi dk36 na Kagimu Shafiq.

HAKUNA MAONI

ACHA JIBU